“Allah (s.w) humwingiza katika rahma zake amtakaye na kumwacha kupotea amtakaye”




Muradi wa aya zenye melekeo huu ni kuwa Allah(s.w) ametoa sifa za waumini kama zilivyoaminishwa katika Qur’an mf.( 23: 1-1 1), (25: 63-77), (8:2-4), (49: 1-13,15), (70:19-3 5), n.k.
Hawa ndiyo “anaowataka” basi anayetaka awepo katikakundi hilo hana budi ajipambe kwazo. lakini pia ametoa sifa za wafiki, washirikina, makafiri, .n.k kama zilivyoanishwa katika qur’an (33:12-20), (2:8-20), (3:166-171), (4:135-1 52), n.k.
Watu watakojipamba na sifa hizi basi Allah huwaacha ( akawaelekezea huko) kupotea, Allah (s.w) ni mwadilifu, humrahisishia mja kila akitakacho cha kheri au cha shari, ndiyo maana pia anasema,”Haakhirishi ya watu mpaka watu wabadilishe yayokuwa katika nafsi zao ”Mbona kuna Uovu na Mateso Duniani? Kuna baadhi ya watu ambao huuliza hivi: Iwapo Mwenyezi Mungu anawapenda waja wake mbona anaacha maovu na mateso yaendelee duniani? Kwa nini asiyazuie?
Kwanza: ni makosa kumhukumu Mwenyezi Mungu ambaye ni Mjuzi wa kila kitu kwa vipimo vya kibinaadamu.



Hii ni kwa sababu binaadamu mara nyingi anaathiriwa na hisia zake binafsi na maslahi yake katika kufanya maamuzi yake. Kwa mfano tunaamuaje kuwa kitu fulani ni chema au kibaya? Tuchukue mifano rahisi. Mvua ikinyesha mkulima aliyepanda mazao anamshukuru Mwenyezi Mungu lakini mtu anayekwenda pikiniki au anayefanya sherehe ya harusi, mvua hasa ikinyesha kutwa nzima ni nuksi kubwa kwake! Au tuseme mtu amekodi teksi anawahi ndege uwanjani kwenda kumzika mama yake. Kwa sababu ya msongamano wa magari barabarani amechelewa kufika uwanjani na hivyo ndege imemwacha na safari kaikosa.



Atalaani mtu huyo na kudai kuwa huo ni mkosi mkubwa. Baada ya nusu saa akisikia kuwa ndege ile imeanguka na watu wote wamekufa utamsikia anamshukuru Mungu kwa bahati njema aliyoipata! Binaadamu hawana haki ya kumuuliza Mwenyezi Mungu kama tunavyofahamishwa katika Qur-an:


Haulizwi (Mwenyezi Mungu) anayoyafanya lakini wao (viumbe wataulizwa). (21:23)


Hii haina maana kuwa binaadamu wanakatazwa kujaribu kutafuta hikima ya Mwenyezi Mungu katika kuamrisha au kukataza kwake mambo, La! Kinyume chake wanahimizwa kufanya hivyo. Wanachokatazwa ni kujaribu kumhukumu Mwenyezi Mungu au kuyakataa na kuyapinga yale ambayo hikima yake hawaijui. Hivyo katika hizo jitihada za kujaribu kubahatisha kuona hikima ya kuyaacha maovu na mateso yawepo baadhi ya watu wanasema kuwa lau si kuwepo kwa uovu watu wasingejua nini wema, bila kuwepo maradhi watu wasingejua thamani ya afya na bila ya mauti watu wasingeyathamini maisha.
Wengine wanasema hata wadudu wabaya tunaodhani wanawabughudhi binaadamu, tunadhani hivyo kwa sababu tu hatujajua thamani yao kwetu.
Jambo la kukumbuka ni kuwa kwa mujibu wa Qur-an binaadamu katika kipindi chote cha maisha yake hapa duniani yupo katika majaribio. Na majaribio hayo yatachukua sura mbali mbali za heri na shari.



Na jingine ni kwamba ili mtihani huo uwe na maana yoyote watu lazima wawe na hiari ya uchaguzi.
Hii ina maana kuwa watu wanaweza kuchagua uovu pia. Hivyo iwapo Mwenyezi Mungu atawapa watu hiari ya uchaguzi lakini atahakikisha hawachagui kufanya ufisadi na uovu nini maana ya kutoa mtihani? Hii haina maana kuwa baada ya kuumbwa ulimwengu Mwenyezi Mungu ameususa na kuuacha uende vyovyote utakavyokwenda, La! Bali kila kitu kipo katika Qadar yake.



Maana ya Kuamini Qadar katika Maisha ya Kila Siku





Kwanza, Kwa kujua kuwa fursa, bahati, vipaji na neema zote alizonazo hakuzipata kwa uwezo wake, hanabudi kuvitumia vitu hivi kama amana aliyokabidhiwa na Mola wake. Hanabudi kuitumia amana hii vizuri ili kumuwezesha kufikia lengo la kuumbwa kwake. Muumini wa kweli ana yakini kabisa kuwa atakapo khini amana aliyokabidhiwa na Mola wake, atakuwa ni mwenye kukosa shukrani na atastahiki kuadhibiwa.Kisha kwa hakika mtaulizwa siku hiyo juu ya neema (mlizopewa mlizitumiaje)” (102:8)




Pili, Kwa kujua pia kuwa fursa, bahati, vipaji na neema zote zinatoka kwa Allah (s.w), halalami pale atakapokuwa amekadiriwa vitu hivi kwa uchache Yaani hatalalama na kukata tamaa pale atakapokosa fursa mbali mbali, atakapofikiwa na bahati mbaya, atakapodhikishwa vipaji na neema mbali mbali. Bali ataridhika na alichokadiriwa na Mola wake na pia atamshukuru Mola wake kwa kumpangia amana ndogo anayoiweza kuitunza, kwani huenda kama angelikabidhiwa amana kubwa zaidi ya hiyo aliyonayo, angelishindwa kuitunza na kuwa miongoni mwa waliofeli mtihani.




Tatu, atajitahidi kutumia fursa, bahati, vipaji na neema zote alizotunukiwa na Mola wake kwa kadiri ya uwezo wake, kisha matunda ya jitihada hizo huyategemeza kwa Mola wake. Akipata matunda mazuri yaliyotarajiwa hafurahi kupita kiasi, bali atakuwa na furaha ya kawaida ikiambatana na kumshukuru Mola wake kwa kuzidisha kutenda wema kwa kuswali Sunnat-shukra, kutoa sadaqa, kufunga sunnah, n.k. Akipata matunda dhaifu asiyoyategemea, hatakata tamaa na kusononeka, bali ataridhika na matokeo hayo, na ataona ndio makadirio ya Allah (s.w) na ndiyo yenye manufaa naye. Atashukuru na kusema “Al-hamdulillah ‘Alaa kullihaali”
Nne, anapotokewa na misuko suko mbali mbali iliyo nje ya uwezo na jitihada za binaadamu, huwa ni mwenye kutulizana na kusubiri akijua kuwa:“Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwisha andikwa katika kitabu kabla hatujaumba. Kw a yakini hilo ni sahali kwa Allah, msihuzunike sana juu ya kitu kilichokupateni. Na Allah hampendi kila ajivunaye, ajifaharishaye. ” (57:22-23)Muumini wa kweli anajua kuwa misiba na misuko suko mbali mbali ni katika qadar ya Allah (s.w) kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:



“Na tutakutieni katika misuko suko na hofu, njaa, upungufu wa mali na watu na matunda.Na wapashe habari njema wale wanaosubiri. (2:155)
Tano, Mtu anayeamini Qadar ya Allah (s.w), siku zote huyaweka mategemeo yake yote kwa Allah (s.w) ambaye ndiye mdhibiti wa kila jambo. Huendelea kutimiza wajibu wake kwa ujasiri na subira hata anapokuwa katika mazingira magumu kwa kuwa anayakini kuwa:“... Halitatusibu ila alilotuandikia Mwenyezi Mungu,Yeye ni Mola wetu. Basi waislamu na wamtegemee Mwenyezi Mungu tu ”. (9:51) 279