Kusingiziwa Nabii Sulaiman Uchawi


Pamoja na Ucha-Mungu aliokuwa nao Nabii Sulaiman watu hawakuacha kumsingizia mambo machafu. Na hii imekuwa ni tabia ya watu wabaya kuwasingizia Mitume uovu ili wapate kuwapoteza watu na njia ya Allah. Nabii Suleiman katika jumla ya mambo aliyosingiziwa ni kuwa alikufuru akafundisha watu elimu ya uchawi. Qur'an inajibu shutuma hizo katika aya ifuatayo:
Wakafuata yale waliyoyafuata mashetani (wakadai kuwa yalikuwa) katika uflame wa Sulaiman; na Sulaiman hakukufuru, bali mashetani ndio waliokufuru, waliwafundisha watu uchawi (waliokuwa wakiujua wenyewe tangu zamani) na (uchawi) ulioteremshwa kwa malaika wawili; Haruta na Maruta; katika (mji wa) Babil. Wala (Malaika hao) hawakumfundisha yeyote mpaka wambwambie: "Hakika sisi ni mtihani (wa kutazamwa kutii kwenu); basi usikufuru;" Wakajifunza kwao ambayo kwa mambo hayo waliweza kumfarikisha mtu na mkewe (na mengineyo). Wala hawakuwa wenye kumdhuru yeyoyte kwa hayo ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na wanajifunza ambayo yatawadhuru wala hayatawafaa. Na kwa yakini wanajua kwamba aliyekhiari haya hatakuwa na sehemu yoyote katika Akhera. Na bila shaka ni kibaya kabisa walichouzia nafsi zao. Laiti wangalijua (hakika wasingefanya hivi). (2:102)Pamoja na aya hii kumtakasa Nabii Sulaiman na yale aliyokuwa akisingiziwa, mafundisho yafuatayo hapana budi tuyazingatie. Kwanza, tunafahamishwa kuwa elimu ya uchawi ipo; lakini ni mtihani kwa wanaadamu. Kujifundisha na kuufanyia kazi uchawi ni kufru na atakayehiari kuufuata hatakuwa na sehemu yoyote katika Akhera.Jambo la pili tunalotakiwa tulizingatie ni kuwa Muislamu hana haja ya kubabaika anapopatwa na janga lolote. Mwenyezi Mungu anatufahamisha kuwa huo uchawi hauwezi kumdhuru mtu ila kwa idhini yake Allah(s.w).".............Wala hawakuwa wenye kumdhuru yeyote kwa hayo ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu….........." (2:102).Kwa hiyo Muislamu amtegemee Allah(s.w) na alikabili tatizo lolote litakalomtokea kwa kuchunga mipaka ya Allah(s.w) na kuomba msaada wake.