Uchambuzi wa Neema Alizopewa Nabii Sulaiman(a.s).

(i) Kutiishiwa Upepo
Qur'an inatufahamisha kuwa Nabii Sulaiman alitiishiwa upepo akaweza kuutumia apendavyo kwa amri yake.


"Na kwa Sulaiman (Tukautiisha) upepo wa nguvu uendao kwa amri yake katika ardhi ambayo tumeibarikia. Nasi ndio tunaokijua kila kitu. Na kwa Sulaiman (Tukautiisha) upepo (uliokwenda) safari yake ya subuhi (mwendo wa) mwezi mmoja, na safari yake ya jioni (mwendo wa) mwezi mmoja" (34:12).Aya hizi zinaweka wazi kuwa, Nabii Sulaiman aliweza kufanya safari ndefu sana baharini kwa wepesi kabisa kwa vile Allah(s.w) aliutiisha upepo kiasi kwamba ulivuma katika mwelekeo wa vyombo vyake. Kwa hiyo safari ya mwezi mzima aliweza kuifanya kwa masaa machache. Na tukiwa leo katika karne ya sayansi na teknolojia ambapo madege husafiri kwa kasi ya maelfu ya kilometa kwa saa, haiwi viguvmu kwa fahamu zetu kuielewa neema hii aliyopewa Nabii Sulaiman.


(ii) Kutiishiwa Majini.
Nabii Sulaiman(a.s) alitiishiwa majini ambayo aliyatumikisha kumfanyia kazi mbalimbali.

"Na (Tukamtiishia) mashetani wenye kumpigia mbizi (ili wamletee lulu) na wakimfanyia vitendo vingine visivyokuwa hivyo. Nasi tulikuwa walinzi wao" (21:82) Tazama pia (34:12-13) na (27:17).Ilivyokuwa kawaida mwanaadamu huishi na kushirikiana na wanaadamu wenzake. Aidha viumbe wa jinsi nyingine huishi na kuhusiana wao kwa wao. Asili ya umbile la awali la mwanaadamu ni udongo. Majini wao wameumbwa kwa moto.Katika hali ya kawaida mwanaadamu hakupewa uwezo wa kumwona jinni. Lakini pamoja na tofuati hiyo ya kimaumbile Allah(s.w) Muweza wa yote alimpa Nabii Sulaiman uwezo wa kuyamiliki majini.(iii) Utawala Juu ya Ndege
Pamoja na kuwa mfalme, mwenye kutiiwa na watu, na mwenye uwezo wa kuyatumia majini kufanyia kazi, Nabii Sulaiman alipewa uwezo pia wa kuwatawala na kuwatuma kazi ndege. Hili linawekwa wazi na aya zifuatazo:

"Na alikusanyiwa Sulaiman majeshi yake katika majini na watu na ndege, nayo yakapangwa makundi makundi" (27:17).

"Na akawakagua ndege (na asimuone Hud-Hud) akasema: "Imekuwaje mbona simuoni Hud-Hud, au amekuwa miongoni mwa wasiokuwapo (hapa leo)"? (27:20).(iv) Uwezo wa kusikilizana na viumbe wengine.

Kama alivyokuwa ameneemeshwa baba yake (Nabii Daudi): Nabii Sulaiman alipewa uwezo wa kusikia lugha za viumbe wengine mbali na binaadamu. Katika Qur'an wanatajwa ndege na wadudu.


"Na Suleiman alimrithi Daudi na akasema: "Enyi watu! Tumefundishwa (hata kutambua) usemi wa ndege na tumepewa kila kitu; hakika hii ni fadhila iliyo dhahiri" (27:16).Habari ya kutambua lugha ya wadudu; inabainishwa katika tukio ambapo Nabii Sulaiman alikuwa akipita mahali na jeshi lake. Wadudu chungu wakapeana taafira wachukue hadhari Nabii Sulaiman asije akawaponda hali ya kuwa hana habari. Nabii Sulaiman alifahamu walichokuwa wanaambizana wadudu chungu. Kwa hiyo akalisimamisha jeshi lake mpaka walipoingia mashimoni mwao. Kisha akamshukuru Mola wake kwa neema hii.
Hata walipofika katika bonde la wadudu chungu; alisema mdudu chungu (kuwaambia wenziwe); "Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu; asikupondeni Sulaiman na majeshi yake, hali ya kuwa hawakuhisini (hawana habari)" (27:18).Basi akatabasamu akilichekea neno lake, na akasema: "Ee Mola wangu! Nipe nguvu nishukuru neema yako uliyonineemesha mimi na wazazi wangu, na nipate kufanya vitendo vizuri uvipendavyo, na uniingize kwa rehma yako katika waja wako wema" (27:19).Historia inaonesha kuwa mara nyingi utajiri, wingi wa watoto, uflame na mamlaka makubwa huwa ndio chanzo cha watu kutakabari na kufanya udhalimu na ufisadi katika ardhi. Tunayo historia ya Firauni, Karun, Hamana na wengineo ambao walitakabari na kufanya ufisadi kwa ajili ya utajiri na mamlaka waliyokuwa nayo. Aidha tunao kina Musolin, Stalin, Hitler, Ngueso n.k. Wapo pia Maraisi wengine ambao hawapo katika rekodi za madikteta, lakini huwanyonya, huwatesa na kuwafanyia udhalimu wa kila namna raia zao.Nabii Sulaiman(a.s) aliwatawala binaadamu wenziwe, majini hadi ndege. Lakini kwa kutambua kuwa yote aliyokuwa nayo ni neema kutoka kwa Allah(s.w) na kwamba ipo siku atasimamishwa katika mahakama tukufu ya Allah(s.w) kujibu jinsi alivyoitumia neema ile; anakuwa mnyenyekevu na mwenye kuchunga mipaka ya Allah(s.w). Anafahamu kuwa kila kiumbe kina lengo la kuumbwa kwake na kina haki ya kuishi. Kwa hiyo anajali hata maisha ya mdugu chungu.Nabii Sulaiman kwa kutambua kuwa neema zote hizo alizotunukiwa ni mtihani kwake,tunamuona akimuomba Mola wake ampe nguvu ya kuweza kushukuru neema alizompa.(Qur’an 27:19).Kwa maana amjaaliye asitakabari na kuzitumia neema hizo kwa namna ambayo itawadhuru wengine iwe ni kwa kukusudia au kutokufahamu.Ardhi yetu hii haitokuwa na amani, uhuru na salama ya kweli mpaka tuwe na viongozi wanaojali haki, uhuru na usalama wa binaadamu wenzao kama Sulaiman alivyo wajali hata wadudu chungu. Na hawa hawawezi kuwa wengine ila wale wanaomtambua Mungu mmoja na kumcha kweli kweli. Viongozi watakaoongoza si kwa kufuata miongozo na katiba zilizobuniwa na watu bali kwa kufuata Kitabu cha Allah na Sunna ya Mtume wake (s.a.w).