(i)Dai kuwa Qur-an ni Mashairi aliyotunga Muhammad (s.a.w):
Dai hili lilitolewa na Makuraishi katika enzi hizo za kushuka kwa Qur-an pia linaendelea kutolewa na makafiri wa karne hizi. Kwa mfano Stober, baada ya kusoma tafsiri ya Qur-an alidai kuwa itakuwa imeandikwa na Mwarabu ambaye ni mweledi wa historia ya Mayahudi na mila za nchi yake ambaye pia ni mshairi mzuri.
Udhaifu:
Wasomaji wa mashairi ya Kiarabu wanafahamu kuwa mashairi hayo yana mizani,beti na vina na yanaimbika kwa kiasi kwamba wakati mwingine inabidi hata maana au sarufi viwekwe pembeni alimradi tu shairi liimbike. Hivi sivyo kabisa ulivyo mfumo wa Qur-an. Qur-an si mashairi bali ni ujumbe wenye maana kamili ulioandikwa katika fasihi ya hali ya juu kwa kuzingatia sarufi na miiko yote ya lugha hai
.
Historia imeshuhudia kuwa Qur-an si mashairi. Ilikuwa kawaida ya washairi wakati ule wa Mtume (s.a.w) kubandika mashairi yao kwenye mlango wa Ka'aba kama changa-moto kwa washairi wengine. Ilitokea siku moja mshairi mashuhuri wa wakati huo, Labbiib ibn Rabiah, akabandika shairi lake kwenye mlango wa Ka'aba ili kutoa changamoto kwa washairi wengine. Shairi lake lilikuwa limetungwa kwa utaalamu mkubwa sana na lilikuwa zuri mno kiasi cha kutothubutu mtu yeyote kupambanisha shairi lake na hilo. Lakini baada ya kubandikwa kipande cha Sura ya Qur-an karibu na shairi lake, Labbiid mwenyewe (ambaye alikuwa Mshirikina) baada ya kusoma mistari michache ya sura hiyo alinaswa na mvuto wake na kuiamini dini iliyofunuliwa kutoka kwa Allah (s.w) na kubandua shairi lake