(ii)Dai kuwa Qur-an ni zao la njozi za Mtume (s.a.w) zilizovurugika:Katika miaka ya 1960 waandishi wawili, Anderson na Watt, walikuja na dai kuwa Qur-an ni zao la dhana (Wishful Thinking).


Walidai kuwa maneno na maelezo ya habari mbalimbali yaliyomo katika Qur-an yametokana na mawazo ya Mtume (s.a.w) aliyoyatoa kwa dhana tu. Watt, kwa kutumia njia za kisasa za kuchunguza fasihi alihitimisha kuwa angelifanya makosa makubwa sana kama angeliamini kuwa Qur-an ni ujumbe wa Allah (s.w) kwani: "Kila kinachoonekana kinatoka nje ya fikra za mwanaadamu, kwa kweli hutokana na mawazo yake ya kinjozi ambayo hutokea bila ya kufikiri." Kwa hiyo alieleza Watt kuwa Qur-an ni zao la dhana (Creative Imagination)Udhaifu wa Dai hili:
Nadharia ya Anderson na Watt haina nguvu yoyote kwa sababu katika historia nzima ya mwanaadamu hapajatokea mawazo ya kinjozi hata yawe yamebuniwa kwa uhodari kiasi gani yakaunda kitabu mithili ya Qur-an au hata angalau sura moja iliyo mithili na sura yoyote ya Qur-an. Hata hivyo, jambo la kukumbuka ni kwamba dai hili la Anderson na Watt na makafiri wengine wa kisasa wenye mawazo kama hayo, si geni bali ni dai kongwe lililotolewa na jamii ya Mtume (s.a.w) mwenyewe kama tunavyofahamishwa katika Qur-an:


"Lakini (Makafiri) walisema: "(Hayo anayosimulia) ni ndoto zilizovurugika. Bali ameyabuni (mwenyewe). Bali huyu ni mtunga mashairi tu.Basi atuletee Muujiza kama walivyotumwa (Mitume) wa kwanza." (21:5)