Maandalizi ya Safari ya Hija
Maandalizi ya Hija hayaanzii kwenye miezi ya Hija, bali huanzia mbali katika umri wa mtu. Tunafahamu kuwa utekelezaji wa Ibada ya Hija unahitaji kuwa na uwezo wa kifedha (kimali). Hivyo Muislamu wa kweli katika kuchuma na kutumia mali yake, hana budi kuzingatia suala la nguzo ya Zaka na nguzo ya Hija. Muislamu atakapoweka mbele yake wazo la kutoa Zaka na Kuhiji, daima atachunga mipaka ya Mwenyezi Mungu (s.w) katika kuchuma kwake, kwani anafahamu wazi kuwa mali iliyochumwa kwa njia za haramu haifai kutolea Zaka au Kuhijia. Hebu tuzingatie hadithi ifuatayo:
Ibn Umar amesimulia kuwa Mtume (s.a.w) amesema: Swala haikubaliwi bila ya Twahara, wala Sadaqa haikubaliwi kama inatolewa kutokana na mali iliyochumwa kwa njia za haramu. (Muslim).
Halikadhalika, kutokana na hadithi hii, Hija haitasihi endapo mtu atahiji kwa kutumia mali iliyopatikana kwa njia za haramu. Hivyo, fikra ya kuhiji, humzoesha Muumini kuchunga mipaka ya Mwenyezi Mungu katika uchumi.
Pia fikra ya Hija humzoesha Muumini kutumia mali yake kwenye mambo muhimu tu ili kumuwezesha kuweka akiba kwa ajili ya Hija. Yaani fikra ya kutekeleza nguzo hii, humuepusha na ubadhirifu au utumiaji bila ya haja na bila ya ratiba.
Mtu anayekusudia kuhiji azidishe kutenda wema. Ajizatiti katika kusimamisha swala tano, kutoa Zaka, kufunga Ramadhani, kuwahurumia wanyonge kwa kuwapa misaada wanayohitajia na kusuhubiana vizuri na watu wote kwa ujumla. Amuombe msamaha kila aliyemkosea na amsamehe kila aliyemkosea. Pia mwenye kunuia Hija anatakiwa ajitahidi kujiepusha na maovu na azidishe kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu (s.w) kwa yote aliyokosea kwa kujua au kutojua na yaliyowazi au yaliyofichikana. Katika Qur-an Mwenyezi Mungu (s.w) anaagiza kwa wanaokusudia kuhiji:
“Na anayekusudia kufanya Hija katika miezi hiyo, basi asiseme maneno machafu, wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika hiyo Hija. Na kheri yoyote mnayoifanya Mw enyezi Mungu anajua …” (2:197)
Utaona mtu mwenye fikra ya kutekeleza ibada ya Hija daima atakuwa mwangalifu katika mwenendo wake wa kila siku. Atajitahidi kutekeleza maamrisho yote ya Mwenyezi Mungu (s.w) na kujiepusha na makatazo yake yote atajitahidi kuwatendea wema wanaadamu wenzake na kila mara atakuwa mwenye kujiandaa kuitika mwito wa Mola wake (Labbayka), kama vile mtu anayejiandaa kukutana na Mola wake kwa kifo, muda mfupi ujao.