Muawiyah Ateka Jimbo la Misri



Khalifa Ali alimteua Qais bin Sad awe gavana wa Misri. Qais alichukua ahadi ya utii kwa niaba ya watu wa Misri, lakini watu wa jimbo la Khartaban hawakutoa ahadi ya utii kwa Khalifa Ali na Qais aliwaacha kwa kuwa kulikuwa na amani.



Hali hii ya kuwaacha watu wa Khartaban iliwafanya baadhi ya watu wamuone Qais sio mtiifu kwa Khalifa. Khalifa alikusudia kumjaribu Qais kwa kumuamuru awapige vita watu wa Khartaban. Qais hakuona sababu ya kupigana na watu wa Kharaban hivyo akaondolewa kwenye ugavana na nafasi yake akateuliwa Muhammad bin Abubakar.


Muhammad alikuwa kijana hivyo aliwalazimisha watu wa Khartaban wakubali Ukhalifa wa Ali. Watu wa Khartaban hawakukubali na walisubiri hadi vita vya Siffin vilipomalizika waliamua kujilinda dhidi ya majeshi ya gavana Muhammad bin Abubakar na mapigano yakazuka. Majeshi ya gavana yakashindwa mara mbili. Khalifa aliamua kumbadilisha Muhammad na kumtuma Ushtar kuwa gavana wa Misri.


Lakini Ushtar alikufa alipofika mpakani mwa Misr hivyo Khalifa alimtaka Muhammad aendelee kushikilia ugavana wa Misri akamtumia askari 2,000 ambao aliwapata kwa taabu. Lakini kabla askari wa Khalifa hawajafika Muawiya alimtuma Amri bin al As na jeshi la kutosha, likayashinda majeshi ya gavana na yeye mwenyewe kuuliwa. Kwa ushindi huu Misri ikawa chini ya Muawiyah na Amr bin al As akawa gavana wa Muawiyah Misri. Hii ilikuwa katika mwaka wa 38 A.H.