Ghasia Sehemu Mbali Mbali za Dola ya KiislamuMisri kuwa mikononi mwa Muawiyah kulichochea upinzani dhahiri baina ya Ali na Muawiyah. Mnamo mwaka 38 A.H. gavana wa Basra Abdallah bin Abbas alikwenda Kufa kumzuru Khalifa. Wakati huu Basra ilikuwa na wafuasi wa Ali, hali kadhalika wafuasi wa Muawiyah. Kutokuwepo kwa Gavana kulipelekea Ubaidullah Ibn Hadrami mfuasi wa Muawiyah kushawishi watu na kuunda jeshi la kulipiza kisasi dhidi ya mauaji ya Uthman. Alipata jeshi na akavamia Basra. Ziyad ibn Abi Sufiyan aliyekuwa amemshikia ugavana akashindwa kuyamudu majeshi ya Hadrami na kukimbia. Hata hivyo Khalifa aliposikia uasi huo alimtuma Jariah ibn Gudumah na jeshi ambalo liliweza kuzima upinzani. Hadrami na watu wengine sabini walijificha ndani ya nyumba ambayo wafuasi wa Ali waliichoma moto.


Khawarij nao waliendesha upinzani dhidi ya Serikali ya Ali. Upinzani mkali uliendeshwa na Khirrt ambae alipigana na Ali katika vita vya ngamia na vita vya Siffin akiongoza kabila lake la Bani Najia. Jitihada za kumteka katika vita hivi zilishindikana na alikimbilia Ahwaz na Ran Hermuz. Aliwashawishi,Waajemi (Persians), Wakurd (Kurds) na Wakristo wasilipe kodi, akiwa na kundi la wafuasi wake aliendesha uasi Faris na Kirman. Khalifa alituma jeshi ambalo liliweza kuzima uasi huu, katika mapigano haya Khirrt aliuliwa. Kwa ushindi huu jimbo la kusini mwa Persia likarudia utulivu na Ziyad akateuliwa Gavana wa jimbo hili.


Muawiya bado aliendelea kutumia vikundi vya askari katika sehemu mbali mbali za Dola ya Kiislamu. Numan ibn Bashir alitumwa Ain al-Tamr lakini alishindwa na gavana wa Ali, Maliki bin Kab. Kundi lingine la watu elfu sita chini ya uongozi wa Sufiyan ibn Auf lilikwenda Ambar na Madain (Madian), walifanikiwa kumuua kiongozi wa Ambar. Khalifa Ali alimtuma Said Ibn Auf na jeshi ambalo lilimfanya adui akimbie. Askari wengine elfu tatu chini ya uongozi wa Dahak ibn Qais walikaribia Basra. Mapigano yalitokea baina ya majeshi ya Khalifa na Waasi. Waasi 19 waliuliwa na wengine wakakimbia.


Ghasia zote hizi zilitokea katika mwaka wa 39 A.H. Katika mwaka huo huo wa 39 A.H. Ali alipeleka mwakilishi wake Ibn Abbas awe kiongozi wa Hijja, na Muawiyah naye alimpeleka Yazid ibn Sanjar, awe muwakilishi wake. Ugomvi baina yao ulizuka na suluhu ikawa wote wawili wasiongoze Hijja na Shaiban ibn Uthman ibn Abi Talha aliteuliwa kuongoza Hijja. Hali hii ilidhoofisha nafasi ya Ali kama Khalifa.