image

Kuandaliwa Mtume(s.a.w) maandalizi ya kimafunzo na maandalizi ya ki ilham

Mitume huzaliwa Mitume.

Kuandaliwa Mtume(s.a.w) maandalizi ya kimafunzo na maandalizi ya ki ilham

Kuandaliwa Mtume(s.a.w) maandalizi ya kimafunzo na maandalizi ya ki ilham

Mitume huzaliwa Mitume. Mitume wa Allah wamekusudiwa kuwa walimu na viigizo katika jamii zao. Hivyo Allah(s.w) Mjuzi Mwenye Hekima, aliwaandaa kuanzia mbali kabisa, ili kuwawezesha kufikia lengo kuu lililo kusudiwa na ili kuifanya kila hatua ya maisha yao iwe ni funzo kwa Umma zao na Umma zilizofuatia.

Tukirejea historia, tunaona kuwa Mtume Muhammad(s.a.w) alipata maandalizi ya aina mbili, Maandalizi ya Ki-il-hamu na Maandalizi ya kufunzwa na kuelekezwa moja kwa moja.



Maandalizi ya Ki-il-hamu

Maandalizi ya Ki-il-hamu ni maandalizi yaliyompitia Mtume (s.a.w) katika kipindi cha miaka 40 kabla ya kupewa Utume rasmi. Katika maandalizi haya hapana maagizo rasmi yanayotolewa bali tunajifunza kutokana na matukio na mazingira kuwa palikuwa na



mpango maalum uliopangwa kumuaanda Mtume(s.a.w). Ili tuone maandalizi haya hebu tuzingatie matukio machache katika maisha ya Muhammad(s.a.w) kabla ya kupewa Utume rasmi ikiwa ni pamoja na:



(i) Kuzaliwa Makka katika kabila tukufu la Quraish.

(ii) Kupewa jina la Muhammad.

(iii) Malezi bora aliyoyapata.

(iv) Tabia njema isiyo na mfano wake.

(v) Ndoa yake na Bibi Khadija.

(vi) Kuchukia maovu na kujitenga pangoni.




(i) Kuzaliwa Makka katika kabila la Quraish


Mtume(s.a.w) kuzaliwa Makkah katika kabila tukufu la Quraish, chini ya ulezi wa Babu yake Abdul-Muttalib, aliyekuwa kiongozi wa Maquraish, ni kielelezo kuwa alistahiki kuchaguliwa kuwa kiongozi wa watu wake. Kabila la Quraish ni katika kizazi cha Nabii Ibrahim(a.s) kupitia kwa Ismail(a.s). Mtume(s.a.w) kuwa Mtume na kiongozi wa Dola ya Kiislamu ni jibu la dua ya Nabii Ibrahimu baada ya kukamilisha kazi ya kujenga upya Ka’abah:



Na (kumbukeni khabari hii pia) Ibrahimu alipoinua kuta za nyumba (hii ya Al-Kaaba) na Ismail (pia); (wakaomba wakasema) “Ee Mola wetu! Tutakabalie (amali yetu hii ya kujenga huu msikiti). Hakika wewe ndiye Mwenye kusikia, na Mwenye kujua.” (2:127)



“Ee, Mola wetu! Waletee Mtume anayetokana na wao, awasomee Aya Zako, na kuwafundisha Kitabu (chako) na hikima na awafundishe kujitakasa (na kila mabaya). Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu, na ndiye Mwenye hikima. (2:129)

(ii) Kupewa jina la Muhammad(s.a.w)


Kuzaliwa kwa Mtume(s.a.w) na kupewa jina la Muhammad na Babu yake, lililo na maana sawa na lile la Ahmad alilooteshwa mama yake ni jambo jingine linalothibitisha maandalizi haya. Jina la Ahmad lenye maana ya “mwenyekushukuriwa” lilitabiriwa katika Taurat na Injili kama tunavyojifunza katika Qur-an:



“Na (wakumbushe) aliposema Issa bin Maryamu, ‘Enyi wana wa Israil! Mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, nisadikishaye yaliyokuwa kabla yangu katika Taurat, na kutoa habari njema ya Mtume atakayekuja nyuma yangu ambaye jina lake litakuwa Ahmad. Lakini alipowajia kwa hoja zilizowazi walisema, ‘huu ni udanganyifu uliodhahiri”. (61:6).



(iii) Malezi bora aliyoyapata


Pamoja na kuwa Muhammad(s.a.w) alizaliwa akiwa yatima, alipata malezi bora na ya huruma kupitia kwa mama yake wa kunyonya- Bibi Halima bint Abi-Dhuaby. Mama huyu wa kabila la Bani Khawaizin ambalo lina sifa ya usafi na lugha fasaha ya Kiarabu alitokea Taifu mji wenye hali nzuri ya hewa kwa kulelea watoto. Mtume alipata bahati ya kukaa miaka mine badala ya miwili kutokana na magonjwa ya mlipuko yaliyojitokeza Makkah jambo ambalo lilimuwezesha kuzungumza kiarabu kwa ufasaha zaidi kuliko watu wengine wa Makkah. Mama yake Amina bint Wahhab alimlea mpaka alipofikisha umri wa miaka 6 akafariki. Babu yake Abdul-Muttalib aliendelea kumlea na alipofikisha umri wa miaka 8 akafariki. Kisha alilelewa na ‘Ami yake, Abu - Talib ambaye aliendelea kuwa naye mpaka alipopewa utume na alikuwa akimlinda mpaka alipofariki, Mtume(s.a.w) akiwa na miaka kumi ya utume. Hii haikutokea tu kwa bahati nasibu,bali tunafahamishwa katika Qur-an kuwa ni maandalizi maalum aliyoyapanga Allah(s.w).


Je! Hakukukuta yatima akakupa makazi (mazuri ya kukaa)? (93:6).



(iv) Tabia yake njema isiyo na mfano wake


Tabia nzuri ya Mtume(s.a.w) haikuishia utotoni mwake tu bali iliendelea kwa umri wake wote. Tunajifunza katika historia kuwa hata alipokuwa mtoto hakuwahi kufanya vitendo vya kipuuzi vya kitoto na alikuwa ni mwenye haya sana. Wakati fulani kuta za Ka’abah zilifanyiwa ukarabati. Wavulana wadogo wadogo nao wakashiriki katika kazi ya ukarabati. Wavulana hawa walizitoa nguo zao za kiunoni na kuziweka mabegani ili kubebea mawe. Abu Talib alimshauri Mtume(s.a.w) naye ajiunge na watoto wenziwe. Mtume(s.a.w) alikubaliana na ushauri wa Ami yake, lakini alikuwa na haya sana hata katika umri ule wa utotoni. Hivyo, alipojaribu naye kuvua nguo yake na kubaki uchi, alishikwa na bumbuazi (butwaa) na kuanguka chini.



Mtume(s.a.w) tangu utotoni mwake aliepukana na tabia zote chafu zenye kuchukiza watu kwa ujumla. Pia aliepushwa na matendo yote maovu yenye kumchukiza Allah(s.w) ambayo yalionekana mazuri mbele za watu wa jamii yake. Kwa mfano katika umri wa ujana wake aliazimia mara mbili kuhudhuria mikesha ya ngoma za harusi za rafiki zake wawili lakini Allah(s.w) alimwepusha na mikesha hiyo kwa kumpa usingizi mzito mpaka asubuhi kwa safari zote mbili.



Tangu utotoni mwake Mtume(s.a.w) alichukia sana Ibada ya masanamu. Hakupata kuhudhuria hata mara moja ibada za masanamu wala hakupata kula kilichoandaliwa kwa ajili ya masanamu. Moyo wake pia ulichukia maovu yote mengine yaliyofanywa matendo ya kawaida na watu wa jamii yake kama vile ulevi, uzinifu, uchezaji kamari, ulaji riba, udhalimu, ulaji wa vyakula haramu, n.k.



Tangu utotoni mwake, Muhammad(s.a.w) alisifika kwa kila sifa nzuri zilizobainishwa katika Qur’an. Bibi ‘Aisha(r.a) alipoulizwa juu ya tabia ya Mtume(s.a.w) alijibu kuwa tabia yake ni Qur’an. Yaani Mtume(s.a.w) amejipamba na vipengele vyote vya tabia njema vilivyobainsihwa katika Qur’an tangia utotoni mwake. Qur’an yenyewe katika miongoni mwa aya zake za mwanzo mwanzo kushuka, inamsifu Mtume(s.a.w) kwa tabia yake tukufu:



“Na bila shaka unatabia njema kabisa” (68:4)

Aya hii haielezi kuwa tabia yake ilikuwa njema tu pale alipopata utume bali inaashiria kuwa tabia yake njema anayo tangu utotoni mwake. Muhammad(s.a.w) tangu utotoni mwake tumeona kuwa alikuwa mpole, mtulivu, mwenye huruma, mwenye haya na mwenye sifa zote nzuri zilizowapendeza watu na kuwavutia. Alikuwa mashuhuri Bara Arab nzima kwa ukweli na uaminifu wake. Alikuwa mkweli mno mpaka akaitwa, “As-Sadiq” – “mkweli” na alikuwa mwaminifu mno mpaka akapewa jina la “Al-Amin”. Muhammad(s.a.w) alikuwa haitwi ila kwa majina haya: As-Sadiq Al-Amin. Wakubwa na wadogo walimheshimu na walimpa amana zao kuwawekea hata baada ya kupewa Utume. Tabia yake njemaisiyo na mfano wake katika jamii yake ni uthibitisho kuwa
Mtume(s.a.w) aliandaliwa ki-il-hamu kabla hajapewa utume.



Tabia yake njema isiyo na mfano wake kuanzia utotoni hadi utuuzima wake inaashiria wazi kuwa hakuwa zao la jamii yake, bali aliandaliwa na Mola wake awe vile ili awe kiigizo chema kwa watu wa Umma wake na walimwengu kwa ujumla.



(v) Ndoa yake na Bibi Khadija


Umaarufu wa Muhammad(s.a.w) kutokana na tabia yake tukufu ulienea Bara Arab nzima. Bibi Khadijah, mwanamke mjane miongoni kwa matajiri wakubwa wa Makkah, alivutiwa na tabia ya Muhammad(s.a.w). Bibi Khadijah alimtaka Muhammad ampelekee bidhaa zake Yemen kwa ujira wa ngamia wawili. Muhammad(s.a.w) alikubali na alirejea na faida kubwa zaidi kuliko matazamio ya Bibi Khadijah. Bibi Khadijah alivutika kwa faida hiyo kubwa na ikambidi tena amuombe Muhammad(s.a.w) ampelekee bidhaa zake Sham(Syria)kwa malipo ya ngamia wanne. Katika msafara huu, Muhammad(s.a.w) alimletea Bibi Khadijah faida kubwa zaidi ya mategemeo yake. Khadijah alikuwa hajawahi kupata faida kubwa kiasi kile tangu aanze kufanya biashara katika misafara ya Sham. Pamoja na furaha ya kupata faida kubwa kiasi hicho, Bibi Khadija alizidi kufurahi na kuvutiwa na Muhammad aliposikia sifa zake za ajabu kutokana na taarifa ya mtumishi wake Maisarah, waliyeongozana naye. Kutokana na mvuto ule Bibi Khadijah hakuweza kustahamili kukaa mbali na Muhammad(s.a w). Hivyo alimtaka radhi Muhammad na kuomba amuoe. Bibi Khadijah wakati huo alikuwa mjane mwenye umri wa miaka 40, aliyewahi kuolewa mara mbili na kujaaliwa kupata watoto watatu, wawili wanaume na mmoja mwanamke. Kabla ya hapo matajiri na machifu wengi wa Makkah walipeleka posa zao kwa Bibi Khadijah lakini aliwakatalia. Muhammad(s.a.w) akiwa na umri wa miaka 25, alikubali ombi la Bibi Khadijah baada ya kushauriana na ami yake, bila ya kujali tofauti kubwa ya umri iliyokuwepo.

Baada ya kuoana, Bibi Khadijah alimuingiza Muhammad kwa ukamilifu katika biashara, akiwa si mwajiriwa tena kama ilivyokuwa katika safari mbili za mwanzo, bali baba na

kiongozi wa familia. Muhammad(s.a.w) alifika sehemu mbali mbali za Bara Arab kwa shughuli ya biashara ikiwa ni pamoja na Bahrain na Yemen. Muhammad(s.a.w), kwa kushauriana na mkewe, alitumia sehemu ya utajiri wao katika kuwakomboa watumwa na vijakazi waliokuwa wakifanyiwa ukatili na mabwana zao. Bibi Khadijah alimzawadia Mtume(s.a.w) mtumwa wake aliyeitwa Zaid bin Harith. Mtume(s.a.w) alimpa Zaid uhuru wake na kumfanya mtoto wake wa kupanga. Pia walitumia utajiri wao katika kuwasaidia maskini na kuwalipia madeni wale waliokuwa hawana uwezo wa kulipa madeni yao.



Mtume(s.a.w) na mkewe Khadijah waliishi maisha mazuri ya kifamilia yaliyokuwa mfano bora wa kuigwa. Upendo, huruma na wema wa Mtume(s.a.w) kwa kila mtu, licha kwa familia yake, unafahamika. Bibi Khadijah naye, kwa kumjua Mtume(s.a.w) kuwa ni mtu mtukufu hata kabla hajatangaziwa utume rasmi, alikuwa ni kiliwazo cha Mtume kabla na baada ya utume. Alimfariji na kumpa ushauri mzuri kwa kila gumu lililomfika Mtume(s.a.w) katika maisha yote walipokuwa pamoja. Katika watoto saba wa Mtume(s.a.w), watoto sita wamezaliwa na Khadijah nao ni: Qasim, Zaynab, Ruqiyyah, Umm Kulthum, Fatimah na ‘Abdullah. Watoto wote isipokuwa ‘Abdullah, walizaliwa kabla ya utume. Wanawe wa kiume walifariki wakiwa bado watoto katika kipindi cha utume cha Makkah. Mtoto wa saba wa Mtume(s.a.w) ni Ibrahim aliyezaliwa na mjakazi wake, Mariam bint Kibtiyah katika kipindi cha utume cha Madinah. Naye alifariki angali mtoto.



Hivyo ndoa ya Mtume(s.a.w) na Bibi Khadija haikutokea kwa bahati nasibu tu, bali ulikuwa mpango madhubuti wa Allah(s.w) ili kumtajirisha Mtume ili aweze kutoa mchango wake katika kuwahurumia na kuwasaidia madhaifu katika jamii yake, na ili awe mfano wa kuigwa na matajiri katika kutoa mali kwa ajili ya Allah katika kuwahurumia wanajamii. Qur-an inatufahamisha:



Na akakukuta fakiri akakutajirisha?” (93:8)

Muhammad(s.a.w) alikuwa fakiri kabla ya kumuoa Khadija na kuwa tajiri mkubwa baada ya kumuoa Khadija



(vi) Kuchukia maovu na kujitenga pangoni


Kuchukia maovu na kujitenga pangoni, ni tukio lingine linaloonesha kuandaliwa kwa Mtume(s.a.w) ki-il-hamu. Muhammad(s.a.w) tangu angali kijana alijihusisha mno na masuala ya kijamii na alikuwa akikereka sana kuona wanyonge wakidhulumiwa. Akiwa na umri wa miaka 20 alijiunga na Chama cha kuwatetea wanyonge dhidi ya Madhalimu. Mtume(s.a.w) alikosa usingizi kwa Sababu ya matatizo ya wengine na alikuwa na shauku kubwa ya kutafuta njia ya kuitoa jamii yake kwenye uovu na upotofu na kuipeleka kwenye wema na uongofu. Katika hali hiyo ilibidi ajitenge pangoni ili kutafuta msaada kwa Muumba Wake na aliupata kwa njia ya ndoto na baadaye kutumiwa Malaika Jibril. Allah(s.w) anamkumbusha Mtume wake juu ya maandalizi haya:

“Je! Hatukukupanulia kifua chako. Na tukakuondolea mzigo wako (mzito) uliovunja mgongo wako?” (94:1-3)



“Na akakukuta hujui kuongoza njia akakuongoza?” (93:7).
Mzigo uliovunja mgongo wa Muhammad(s.a.w) kipindi kile si mwingine ila ile hali ya udhalimu na uovu iliyoshamiri katika jamii yake. Alikuwa na ari kubwa ya kuiondoa ile hali na kusimamisha uadilifu katika jamii lakini hakujua ni vipi atafanikisha hilo.



Mafunzo Yatokanayo na Maandalizi ya Ki-il-hamu


Kutokana na matukio haya yanayoashiria kuandaliwa kwa Mtume(s.a.w) kabla ya kupewa Utume rasmi, tunajifunza kuwa katika kuhuisha na kusimamisha Uislamu katika jamii hatuna budi kuzingatia haya yafuatayo:



Kwanza, hatunabudi kuwaandaa watoto wetu kuwa Makhalifa wa Allah(s.w) mapema kabla hata hawajazaliwa. Maandalizi haya yanawezekana pale wazazi wote wawili watakapokuwa na mtazamo huo wa Ukhalifa. Kisha baada ya watoto kuzaliwa tuwaadhinie na kuwakimia,tuwafanyie aqika na kuwapa majina mazuri, tuwalee kwa mapenzi na huruma na kuwafunza tabia njema tangu wangali wachanga. Tuwasomeshe watoto wetu katika shule na vyuo vyenye kufuata mfumo wa elimu wa Kiislamu wenye lengo la kuandaa Makhalifa wa Allah(s.w).



Pili, hatunabudi kuandaa Waalimu na Madaiyah watakao fundisha Uislamu na taaluma nyingine kwa lengo la kusimamisha Ukhalifa katika jamii.



Tatu, Mume na Mke (Baba na Mama) katika familia hawanabudi kushirikiana na kusaidiana kwa huruma na mapenzi ili kupata uwezo wa kuwalea watoto vilivyo na kupata wasaa wa kuyaendea masuala ya jamii.



Nne, Wanawake wa Kiislamu, hawanabudi kumfanya Bibi Khadijah, Mkewe Mtume(s.a.w), kuwa kiigizo chao katika kuwasaidia na kuwaliwaza waume zao hasa wanapokuwa katika harakati za kuhuisha na kusimamisha Uislamu katika jamii.



Tano, hatunabudi kuchukia maovu na dhulma wanazofanyiwa wanyonge na madhaifu wengine katika jamii na kuwa tayari kuondoa maovu na dhulma kwa mikono yetu pale tunapoweza. Na pale ambapo hatuna uwezo wa kutumia mikono, tutoe makemeo, vinginevyo tuingie “Pangoni Hira” tutafute msaada wa Allah(s.w).



Sita, hatunabudi kujipamba na tabia njema kwa kadiri iwezekanavyo. Mtu mwema hutambulika na kukubalika kwa watu kwa urahisi.



Saba, hatunabudi kuimarisha uchumi wetu kwani uchumi ndio nyenzo kuu ya kuusimamisha Uislamu katika jamii.



Nane,Katika kuchagua viongozi wa jamii hatunabudi kuzingatia historia zao pamoja na kuzingatia sifa nyingine za kiongozi bora.



                   





           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Rajabu Tarehe 2024-05-10 14:53:23 Topic: Sira Main: Post File: Download PDF     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 923


Sponsored links
👉1 kitabu cha Simulizi     👉2 Kitabu cha Afya     👉3 Kitau cha Fiqh     👉4 Simulizi za Hadithi Audio     👉5 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)     👉6 Madrasa kiganjani    

Post zifazofanana:-

Nasaba ya Mtume Muhammad S.A.W na familia yake.
Sura na historia ya Mtume Muhammad S.A.W sehemu ya 1 Soma Zaidi...

Kuhifadhiwa kwa Quran
Quran (EDK form 2: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...

Kifo cha Khalia Uthman kilivyotokea
Soma Zaidi...

Historia ya Dhulqarnain
Dhulqarnain sio jina la mtu bali cheo, maana yake ikiwa: “Mwenye Pembe Mbili”. Soma Zaidi...

Uasi katika dola ya kiislamu na matokeo yake
Uasi katika dola ya kiislamu na matokeo yake. Soma Zaidi...

tarekh 08
KULELEWA NA MAMA YAKE ALIPOFIKA MIAKA MINNEMtume (s. Soma Zaidi...

Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Nabii Salih(a.s)
Mafunzo tuyapatayo hayatofautiani na yale yatokanayo na Historia ya Nabii Hud(a. Soma Zaidi...

Hitimisho juu ya Historia ya maimam wanne
Soma Zaidi...

Mafunzo yatokanayo na maandalizi ya mtume ki-wahay
Bara arabu zama za jahiliyyah (EDK form 2 dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...

fadhila za kusoma quran
Fadhila na umuhimu wa kusoma quran 1. Soma Zaidi...

HISTORIA YA KUPASULIWA KWA KIFUA AU TUMBO CHA MTUME MUHAMMAD (S.A.W) AKIWA MTOTO KWA BI HALIMA
KUPASULIWA KWA KIFUA MTUMEWAKATI AKIWA MTOTO. Soma Zaidi...

HISTORIA YA NABII IBRAHIM
Soma Zaidi...