(iii)Jinsi Mtume Muhammad (s.a.w) alivyoipokea Qur-an:



Tumejifunza kuwa Allah (s.w) huwasiliana na wanaadamu kwa njia ya Wahyi (ufunuo) kwa kutumia njia za mawasiliano zifuatazo:
- Il-hamu.
- Kutumwa Malaika.
- Kuongeleshwa nyuma ya pazia.
- Maandishi (yaliyoandikwa tayari)
- Ndoto za kweli.



Qur-an ilishushwa kwa Mtume (s.a.w) kwa njia hii ya wahyi kupitia kwa Malaika Jibril.
Kuonesha kuwa Qur-an ni neno la Allah (s.w) na wala si tungo za Mtume Muhammad (s.a.w) ni ile hali aliyokuwa nayo wakati wa kupokea wahyi. Wakati wa mwanzo mwanzo wa kuanza kushushiwa wahyi Mtume (s.a.w) alikuwa akiyarudia haraka haraka yale aliyokuwa anasomewa na Malaika Jibril kwa wasi wasi kuwa atasahau. Ndipo Allah (s.w) akamtoa wasi wasi huo kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:


Usiutikise ulimi wako kwa (kuufanyia haraka) wahyi (unapoteremka. Wewe sikiliza tu. Usiseme kitu). Kwa hakika ni juu yetu kuukusanya na kuusomesha (kukukusanyia na kukusomesha). Wakati tunapokusomea, basi fuata kusomwa kwake. Kisha ni juu yetu kuubainisha (kukubainishia). (75:16-19)


Tutakusomesha (tutakusomea) wala hutasahau. Ila Akipenda Mwenyezi Mungu; Yeye anajua yaliyodhahiri na yaliyofichikana. (87:6-7)
Kwa hiyo kutokana na aya hizi Qur-an si maneno ya Mtume Muhammad (s.a.w) aliyoyatoa kichwani mwake. Kwani yangelitoka kichwani mwake asingelikuwa na wasi wasi wowote kuwa atakuja yasahau. Alikuwa na wasi wasi kwa sababu yeye akiwa ni Mtume wa Allah(s.w) alijua fika kuwa jukumu lake kubwa ni kuufikisha ujumbe wa Allah kwa watu kama ulivyo bila ya kupunguza au kuzidisha hata chembe.