Shirki ni kitendo chochote cha kukipa kiumbe nafasi ya Allah (s.w) katika dhati yake, Sifa zake, Mamlaka yake na Hukumu zake.
Allah (s.w) aliyemuumba binaadamu na viumbe vyote vilivyo mzunguka kwa lengo, ndiye mwenye Haki na Uwezo pekee wa kumuwekea mwanaadamu mwongozo wa maisha utakao muwezesha kuishi kwa furaha na amani katika maisha ya hapa duniani na maisha ya baadaye huko akhera.
Yeyote yule katika viumbe atakayechukua au kupewa nafasi ya Allah (s.w) katika kutoa kanuni, sheria na mwongozo wa maisha ya binaadamu katika jamii, atakuwa amechukua au amepewa mamlaka ambayo hana uwezo nayo na kwa vyovyote vile atakuwa ameitumbukiza jamii katika Kiza cha Khofu na Huzuni kinachosababishwa na dhuluma za aina mbalimbali. Allah (s.w) analiweka hili wazi katika aya zifuatazo:
"Hakuna kulazimishwa (mtu kuingia) katika dini. Uongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anayemkataa shetani na akamwamini Mwenyezi Mungu, bila shaka yeye ameshika kishiko chenye nguvu kisichokuwa na kuvunjika. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kujua.."
"Mwenyezi Mungu ni mlinzi wa wale walioamini. Huwatoa katika giza na kuwaingiza katika nuru. Lakini waliokufuru, walinzi wao ni matwaghuti. Huwatoa katika nuru na kuwaingiza katika giza. Hao ndio watu wa Motoni, humo watakaa milele." (2:256-25 7).
Hivyo kwa mnasaba wa maelezo haya na aya tulizozirejea, tunajifunza kuwa chanzo cha dhuluma zote anazofanyiwa binaadamu na binaadamu mwenziwe zimetokana na kumshirikisha Allah (s.w) ama katika Dhati yake, Sifa zake, Mamlaka yake au katika Hukumu zake.