(i) Kubisha hodi katika nyakati za faragha katika familia



“Enyi mlioamini! Nawakupigieni hodi wale iliyowamiliki mikono yenu ya kuume, (ya kulia), na wale wasiofikia baleghe miongoni mwenu, mara tatu: kabla ya Sala ya Alfajiri na mnapovua nguo zenu Adhuhuri, na baada ya Sala ya Isha; hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya juu yenu wala juu yao baada ya nyakati hizo (kuingia bila ya kupiga hodi:) mnazungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu Anavyokuelezeni Aya (zake); na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hikima.



“Na watoto miongoni mwenu, watakapobaleghe basi nawapige hodi kama walivyopiga hodi wale wa kabla yao. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyokubainishieni aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hikima. (24:58-59)



Katika aya hizi tunapewa maelekezo ya kinidhamu na kimaadili juu ya watoto na watumishi kuwatembelea wazazi wakiwa nyumbani mwao kama ifuatavyo:
(i)Waumini wanatakiwa wawaelekeze watoto wao ambao hawajafikia baleghe kuwa wabishe hodi wanapotaka kuingia vyumbani katika nyakati tatu za faragha zilizoainishwa:
1.Kabla ya Swala ya Al-fajiri
2.Kabla ya Swala ya Adhuhuri wakati wa kujitayarisha kwa swala.
3.Baada ya Swala ya Al-Ishaa.
(ii)Mida mingine nje ya hii watoto wanaruhusika kuingia bila ya hodi. Kwa maana nyingine wazazi wawe katika hali ya sitara ambayo haitakuwa ni chukizo watakapokutwa na watoto.
(iii)Watoto waliofikia baleghe hawaruhusiwi kuingia chumbani mwa wazazi wao pasina kubisha hodi katika nyakati zote.