Na kwa yakini Tulimpa Luqmani hikima, tukamwambia Mshukuru Mwenyezi Mungu; na atakayeshukuru, kwa yakini anashukuru kwa ajili ya nafsi yake; na atakaye kufuru,
Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Asifiwaye, (hahitaji kushukuriwa na yeye). (31:12)
Na (wakumbushe), Luqmani alipomwambia Mwanawe; na hali ya kuwa anampa nasaha.Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu, maana kushirikisha ndiyo dhulma kubwa. (31:13)
Na tumemuusia mwanaadamu (kuwafanyia ihsani) wazazi wake - mama yake ameichukuwa mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na (kumnyonyesha na kuja) kumwachisha kunyonya katika miaka miwili - ya kwamba unishukuru Mimi na wazazi wako; marejeo yenu ni Kwangu. (3 1:14)
Na (wazazi wako) wakikushurutisha kunishirikisha na (yale) ambayo huna ilimu nayo, usiwatii; lakini kaa nao kwa wema hapa duniani (maadamu ni wazee wako, ila usiwafuate tu mwendo wao mbaya); shika njia ya wale wanaoelekea Kwangu, kisha marejeo yenu ni Kwangu, hapo Nitakuambieni mliyokuwa mkiyatenda. (31:15)
Ewe mwanangu! Kwa hakika jambo lolote lijapokuwa na uzito wa chembe ya hardali, likawa ndani ya jabali au mbinguni au katika ardhi, Mwenyezi Mungu Atalileta (amlipe aliyefanya); bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo yaliyofichikana, (na) Mjuzi wa mambo yaliyo dhahiri. (31:16)
Ewe mwanangu! Simamisha Sala, na uamrishe mema, na ukataze mabaya, usubiri juu ya yale yatakayokusibu (kwani mwenye kuamrisha mema na kukataza mabaya lazima zitamfika tu taabu); Hakika hayo ni katika mambo yanayostahiki kuazimiwa (na kila mtu). (31:17)
Wala usiwatazame (usiwafanyie watu jeuri), kwa upande mmoja wa uso, wala usende katika nchi kwa maringo; hakika Mwenyezi Mungu Hampendi kila ajivunae, ajifahirishaye. (31:18)
Na ushike mwendo wa katikati, na uteremshe sauti yako; bila shaka sauti ya punda ni mbaya kuliko sauti zote (kwa makelele yake ya bure). (31:19)
Mzazi wa Kiislamu mwenye hekima ni yule atakayekuwa mstari wa mbele kutenda mema na kuwalea watoto wake wafuate nyayo zake pamoja na kuwausia na kujiusia yeye mwenyewe kufanya yafuatayo: