“Na wasiape wale wakarimu na wenye wasaa miongoni mwenu, kujizuia kuwasaidia jamaa zao, maskini na wale waliohama kwa ajili ya Dini ya Allah; na wasamehe na waachilie mbali (wapuuze yaliyopita). Je, nyinyi hampendi Allah akusameheni? Na Allah ni msamehevu, mrehemevu. ”(24:22)
Tukirejea historia, Bi 'Aisha (r.a) amesema kuwa baada ya kuteremshwa aya za (24:11-21) zilizomtakasa na uzushi wa wanafiki, baba yake, Abu Bakr (r.a) aliapa kuwa hatamsaidia tena kwa mali Mistah bin Uthatha, miongoni mwa watu waliokuwa mstari wa mbele katika kueneza uzushi dhidi ya Bi 'Aisha (r.a).
Katika kufanya kitendo cha kueneza uzushi, Mistah hakuonyesha kabisa kujali mahusiano wala ihsani ambazo Abu Bakar (r.a) daima alikuwa anamfanyia yeye na familia yake. Hili lilimkasirisha sana Abu Bakar mpaka kumfikisha kwenye kuchukua kiapo cha kusitisha msaada wake kwa Mistah. Baada ya kushushwa aya hii, Abu Bakar aliomba msamaha kwa Allah (s.w) na akaanza tena kumsaidia Mistah kwa moyo mkunjufu zaidi kuliko hata hapo awali.
Kwa mujibu wa 'Abdullah bin 'Abbas (r.a), waumini wengine miongoni mwa maswahaba pia waliapa kuwa hawatawasaidia tena wale wote walioshiriki katika kusambaza masingizio dhidi ya Bi 'Aisha (r.a). Lakini baada ya kuteremshwa aya hii, wote walivibatilisha viapo vyao, na uhasama wote uliosababishwa na hayo 'masingizio' ukaisha.
Kwa mujibu wa aya hii na maelezo haya ya kihistoria tunajifunza kuwa:
(i) Katika maadili mema, hatuna budi kuendelea kuwafanyia wema wale waliotukosea, maadamu hatudhuriki tukiendelea kuwafanyia hivyo. Hekima ya kufanya hivyo Allah (s.w) anaibainisha katika aya zifuatazo:
"Mambo mazuri na mabaya hayawi sawa. Ondosha ubaya (unaofanyiwa) kwa wema, tahamaki yule ambaye baina yako na baina yake kuna uadui, anakuwa kama jamaa (yako) mwenye kukufia uchungu" Lakini jambo hili hawatapewa ila wale wanaosubiri, wala hawatapewa ila wenye hadhi kubwa (Mbele ya Allah (s.w))." (41:34-35)
(ii) Hatuna budi kuwa wepesi kuwasamehe wale walio tukosea ili iwe sababu na sisi kusamehewa makosa yetu na Allah (s.w)"
Je, nyinyi hampendi Allah akusameheni?……" (24:22)