Ni haramu kwa Waumini kuwaoa au kuolewa na Wazinifu, Washirikina na Mahabithi


Mwanamume mzinifu hafungamani ila na mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina; na mwanamke mzinifu hafungamani naye ila mwanamume mzinifu au mshirikina; na hayo yameharamishwa kwa waumini" (24:3)


Wanawake habithi (wabaya) ni wa wanaume habithi na wanaume habithi ni wa wanawake habithi; na wanawake wema ni wa wanaume wema na waume wema ni wa wanawake wema ….. " (24:26)Aya hizi zinatuweka wazi kuwa ili kujenga jamii iliyoinukia kimaadili, waumini hawanabudi kuwa macho katika uchumba. Waumini wahakikishe kuwa katika ndoa ya kwanza binti muolewaji ni bikra na kijana muoaji ni bikra vile vile. Kadhalika katika ndoa ya pili, waumini wasiidhinishe ndoa mpaka wawe na uhakika pasina tone la shaka, kuwa waoanaji wawili ni watwaharifu na wacha-Mungu. Mwanamume mzinifu ni mshirikina kwa mujibu wa Qur'an kwa kuwa ameyafanya matamanio ya nafsi yake kuwa Mungu badala ya Allah (s.w)


"Je, umemuona yule aliyefanya matamanio (ya nafsi) yake (kila anachokipenda), kuwa Mungu wake? Basi je, utaweza kuwa mlinzi wake (ukamhifadhi na hayo, na hali ya kuwa hataki)? (25:43)


Kukiukwa kwa maagizo ya Allah (s.w), katika aya hizi (24:3, 26), imekuwa ni sababu kubwa ya mtafaruku katika familia nyingi za Waislamu na jamii kwa ujumla. Familia za waumini zitaishi kwa furaha na amani endapo ujumbe wa aya hizi utafuatwa vilivyo tangu mapema katika kuanzisha familia hizi.