Ushahidi wa kuthibitisha kutendeka kwa kosa la uzinifu unapatikana kwa namna tatu zifuatzo:
(i)Kushuhudia tendo hilo likifanyika kwa wakati mmoja watu wanne Mukalafu (Walio baleghe na wenye akili timamu), wakiwa ni Waislamu waadilifu.
(ii)Muhusika au wahusika kukiri kwa hiari yake/yao bila ya shinikizo au mazingira yanayopelekea shinikizo lolote.
(iii)Mwanamke kupata ujauzito nje ya ndoa.
Nje ya ushahidi huu, mtu hatahukumiwa kwa kosa la uzinifu au ubasha pamoja na kuwepo mazingira ya kutatanisha. Sana sana atahukimiwa kukurubia zinaa na kupewa nasaha na maonyo stahiki. Ila ikitokea kwa mwanandoa kumkamata mwenziwe ugoni, bila ya mashahidi wanne au muhusika kukiri kosa kwa hiari yake, wanandoa hawa watalazimika kula kiapo mbele ya kadhi kama ilivyoelekezwa katika aya zifuatazo:
Na wale wanaowasingizia wake zao (kuwa wamezini) na hawana mashahidi ila nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudilia mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu: ya kwamba bila shaka yeye ni mmoja wa wanaosema kweli. Na mara ya tano (aape) kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake ikiwa ni miongoni mwa waongo.Na (mke) itamuondokea adhabu kwa kutoa shahada mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba (huyu mume) ni miongoni mwa waongo.
Na mara ya tano (aape) ya kwamba hasira ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake kama (mumewe) yu miongoni mwa wanaosema kweli, (na yeye mke ndiye muongo)." (24:6-9)