24. Kuwa na HayaKuwa na haya ni miongoni mwa tabia njema. Mtu mwenye haya ni yule anayejichunga na maovu na mambo ya aibu. Kuhusu umuhimu wa kuwa na haya, tunajifunza katika Hadithi zifuatazo:Abu Hurairah amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: Haya ni sehemu ya imani na imani mahali pake ni Peponi; na uchafu (uovu) ni sehemu ya ugumu wa moyo na ugumu wa moyo mahali pake ni Motoni. (Ahmad, Tirmidh).Ibn Mas ’ud amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: Miongoni mwa ujumbe watu waliopokea kutokana na mafundisho ya mwanzo ya Utume ni: Wakati unapokuwa huna haya, fanya ulitakalo. (Bukhari).Hapa ina maana kuwa mtu asiye na haya hachagui la kufanya au la kusema. Pia Mtume (s.a.w) amesema katika Hadithi iliyosimuliwa na Imran bin Husain kuwa:
Haya haileti kitu kingine ila uzuri na katika maelelezo mengine; Haya ni nzuri katika kila hali. (Bukhari na Muslim).
Mtume (s.a.w) ambaye ndiye kiigizo chetu alikuwa ni mwenye haya sana kama Hadithi ifuatayo inavyobainisha:


Abu Said al-Khudri (r.a) ameeleza kuwa Mtume wa Allah alikuwa na haya zaidi kuliko wasichana vigori ndani ya mitandio yao. Alipoona kitu kisichopendeza kwake tulikuwa tunakigundua kutokana na uso wake. (Bukhari na Muslim).Muislamu anatakiwa awe na haya katika maongezi, katika kuangalia na katika kujisitiri uchi na katika kufanya kila jambo. Haya ni ngao ya kumuepusha mja na mambo maovu na machafu. Wa kwanza anayestahiki kuonewa haya ni Allah (s.w) kwani mwanaadamu hana kificho chochote cha kumsitiri asionekane kwake. Hivyo mja anayemuamini Allah (s.w) atamuonea haya na kujiepusha na maovu na machafu katika maisha yake yote popote atakapokuwa.