Wajibu wa Kufanyakazi
Uislamu siyo tu unawahimiza watu kufanya kazi na kutokuwa wavivu bali kufanya kazi ni Ibada. Kila jambo lenye manufaa kwa watu binafsi, familia, jamii (n.k) laweza kuhesabiwa kuwa ni Ibada kwa Allah yakitimia masharti mawili; usafi wa nia (Ikhlasi) na kutenda jambo kwa kuzingatia mipaka ya sheria ya Kiislamu. Hivyo kazi ni Ibada. Kufanya kazi ni wajibu alionao mtu mbele ya Allah.Qur-an inawahimiza Waislamu kutenda kazi nzuri zenye manufaa katika eneo lolote lile.


Na sema: Tendeni mambo (mazuri). Mwenyezi Mungu atayaona mambo yenu hayo na Mtume wake na Waislamu. Na mtarudishwa kwa mjuzi wa siri na dhahiri; naye atakwambieni (yote) mliyokuwa mkiyatenda.” (9:105) Katika aya hii Mwenyezi Mungu amefungua milango kwa watu kutenda mambo yote mema katika eneo lolote la uchumi au siasa na yeye ataliona na atalilipa.Uchaguzi wa kazi
Uislamu umempa mtu uhuru wa kuchagua kazi yoyote aipendayo maadamu kazi hiyo ni ya halali kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Na ni wajibu wa serikali ya Kiislamu kuhakikisha kuwa watu wanapata fursa ya kufanya kazi wazipendazo. Watu watafanya kazi kwa mujibu wa vipaji vyao, kwani Mwenyezi Mungu amewajaalia watu vipawa mbali mbali:“Na amewanyanyua baadhi yenu juu ya wengine daraja kubwa ili akufanyieni mtihani kwa hayo aliyokupeni.” (6:1 65).
Kila mtu anafanyiwa mtihani kwa neema au kipawa alichopewa. Katika maisha yetu ya kila siku wanaadamu ni viumbe wanaotegemeana kila mmoja ananufaika kwa kazi ya mwenzake. Daktari atamhitaji Muashi kumjengea nyumba yake na Muashi atamhitaji Daktari kumtibu maradhi yake n.k. Katika Uislamu kazi hutegemea uwezo tu hakuna kazi zilizotengwa kwa ajili ya watu wa ukoo au kabila au nasaba fulani.Tofauti ya malipo
Tofauti ya mapato au malipo ipo kwa sababu ya utendaji, uwingi au ubora wa bidhaa zilizozalishwa. Ni halali kwa fundi aliyetengeneza mashati kumi, hasa amzidi kipato yule aliyetengeneza matano. Au yule aliyetengeneza kitu bora lazima amzidi yule aliyetengeneza kitu duni. Aidha tafauti ya mapato pia ni halali iwepo kutokana na muda mrefu wa mafunzo baadhi ya kazi zikilinganishwa na nyingine. Kwa mfano ikiwa mtu ataajiriwa kufuta mavumbi katika madirisha ya ofisi atahitajia siku moja tu ya kuelekezwa namna ya kuifanya kazi hiyo.


Lakini mtu akiajiriwa kutengeneza madirisha hayo atahitajia muda mrefu zaidi katika kujifunza useremala hawezi kuelekezwa kwa siku moja tu halafu akaweza kuunda dirisha. Hivyo malipo ya mfutaji na mtengenezaji wa madirisha hayawezi kuwa sawa. Malipo yao yakiwa sawa basi watu wanaweza kuzikwepa kazi zinazohitaji mafunzo ya muda mrefu kama udaktari, usanifu majengo uhandisi (n.k.) na kukimbilia zile zenye mafunzo ya muda mfupi kama utarishi, uhudumu, kufagia ofisi n.k.
Aidha malipo hayatakuwa halali iwapo shughuli anayoifanya Muislamu ni faradhi. Kwa mfano; si halali kwa Imamu kupokea mshahara kwa ajili ya kusalisha swala za faradhi, si halali kupokea malipo kutokana na kumhudumia maskini, n.k.Hifadhi ya Wafanyakazi
Uislamu pia umeweka taratibu za kuhifadhi haki na maslahi ya Wafanyakazi. Kwanza kila mfanyakazi lazima awe na mkataba na mwajiri wake. Mkataba huo uweke wazi malipo yake na kazi yake na makubaliano yao mengine. Mkataba huo ni bora uwe kwa maandishi lakini waweza pia kuwa kwa mdomo.
Mwenyezi Mungu ameagiza katika Qur-an kuwa watu watekeleze kikamilifu ahadi zao za halali.


“Enyi mlioam ini tekelezeni w ajibu …” (5:1)
Katika Hadith iliyosimuliwa na Bukhari, Mtume (s.a.w) amesema kuwa miongoni mwa watu watatu ambao Mtume (s.a.w) atawakataa siku ya Kiyama ni yule anayemwajiri mfanyakazi halafu asimpe haki zake.Katika Hadith nyingine amesema;Mlipeni mtu mliyemuajiri kabla ya jasho lake halijakauka. Mradi wa Hadith hii ni kuwa mtu asicheleweshewe malipo yake. Kama mapatano ni kila wiki au kila mwezi n.k. basi muda huo ukifika tu mtu alipwe.Vivyo hivyo kwa mfanyakazi malipo ya kazi yatakuwa ni halali iwapo atatimiza kipimo walichoafikiana na mwajiri kwa mshahara huo. Kutegea kazi humfanya mtu achukue sehemu ya malipo isiyo haki yake. Kwa hiyo, kipato kinachotokana n a kazi iliyotegewa kimechanganyika na kipato cha haramu. Uislamu unamtaka kila muumini awe mwaminifu na muadilifu katika kazi baada ya kupatana na kukubaliana na muajiri.