Kustawi kwa Kampeni ya Kudhibiti Uzazi
Miongoni mwa sababu zilizosaidia kustawi kwa kampeni hii ni matokeo ya mapinduzi ya viwanda (Industrial revolution) ya huko Ulaya. Viwanda vilihitaji wafanyakazi kwa maelfu ambao japo walifanyishwa kazi sana, sehemu kubwa ilikwenda kwa wenye viwanda, hivyo wafanyakazi hawakuweza kuzikimu familia zao. Bidhaa za viwandani pia zikabadili mahitaji ya watu. Vitu ambavyo hapo awali havikuwepo sasa vikawa ni mahitaji ya lazima.Pili, kwa kuwa pato Ia mfanyakazi halikumwezesha kuihudumia familia yake, mke na watoto walilazimika pia kufanya kazi viwandani ili kupata riziki zao. Matokeo ya utaratibu huu ni kuwa familia ziliparaganyika na yale malezi muhimu ambayo mtoto aliyapata kwa wazazi wake sasa yakakosekana. Kwa kuwa mke asingeweza kuishi bila kuajiriwa kiwandani na asingeweza kumudu zile kazi ngumu za kiwandani akiwa mjamzito au akiwa na mtoto mchanga, kuzaa kukaanza kuwa nuksi kubwa. Kwani kipindi chote ambacho mwanamke alishindwa kufanya kazi kwa sababu ya udhaifu wa afya hakulipwa kitu. Ndio maana kampeni hii ya kudhibiti uzazi ilianzishwa na kupiganiwa sana na wanawake. Kujiepusha na kuzaa kukaonekana kuwa ni ukombozi wa ama yake.Tatu, mapinduzi hayo yaliambatana na utamaduni wake. Utamaduni ambao ulihimiza sana maendeleo na ustawi wa mtu binafsi. Ustawi kwa maana yakuwa na vitu vingi vya anasa na fahari. Matokeo yake yakawa watu walijiepusha sana na kila kitu ambacho walidhani kingeliweza kwa namna fulani kuathiri ustawi wao wa binafsi. Moyo wa ukarimu na kuhurumiana ukafa. Ikafikia hadi mtu akawaona wazazi wake kuwa ni mzigo mkubwa kuishi nao watampunguzia anasa zake. Kwa hoja hiyo kuzaa watoto kukawa balaa kubwa. Na aliyezaa akaishia mtoto mmoja au wawili.Nne, kuparaganyika kwa familia kukapelekea kuondoka kwa uadilifu. Na hivyo uadilifu wa ndoa ukaonekana ni hekaya za watu wa kale. Badala yake falsafa za uhuru wa mtu binafsi zikapata nguvu. Kwa mujibu wa falsafa hiyo mtu anao uhuru wa kufanya analotaka na kazi ya serikali ni kuusimamia na kuudumisha uhuru huo. Hivyo kwa upande wa mahusiano ya ndoa falsafa hiyo iliona kuwa hilo ni suala Ia watu binafsi wanahiari ya kufanya lolote wapendalo. Na kampeni zote za kudhibiti uzazi katu hazijishughulishi kabisa na suala zima Ia uadilifu katika ndoa. Bali hujishughulisha tu na kuwasaidia watu wasipate mimba. Na kama tutakavyoona baadaye hii ni dosari mojawapo kubwa ya kampeni hii.