Vipi lengo la funga litafikiwa na kumfanya mfungaji awe mchamungu.
Funga inavyomuandaa mtu kuwa mcha-Mungu.
Tumedhihirishiwa katika Qur-an kuwa lengo la kufaradhishwa kufunga ni kuwafanya waumini wawe wacha Mungu (Muttaq). Yaani kuwawezesha waumini kutekeleza maamrisho yote ya Allah (s.w) kama inavyostahiki kwa matarajio ya kupata radhi zake, na kuwawezesha waumini kuepukana kwa unyenyekevu na kwa moyo mkunjufu na yale yote yanayokwenda kinyume na radhi za Allah (s.w) kwa kuhofia ghadhabu zake. Sasa ni vipi funga ya Ramadhani na funga nyingine za Sunnah humfikisha mja kwenye lengo hili? Swali hili litajibiwa vyema kwa kuiangalia sura ya funga yenyewe. Funga humtayarisha muumini kufikia lengo lililoku sudiwa kama ifuatavyo:
(i) Funga humzidishia mja imani na uadilifu
Funga ni ibada iliyofichikana. Ni siri ya aliyefunga na Allah (s.w) tu. Ibada nyingine kama kusimamisha swala, kutoa zaka na sadaka na kuhiji hubainika kwa wengine pindi mtu anapozitekeleza. Lakini ibada ya funga si rahisi kuonekana utekelezaji wake kwa wengine. Mtu anaweza akala, akanywa au akafanya kwa siri kitendo chochote kinachofunguza na bado akadai kuwa amefunga na akajikausha midomo yake kiasi cha kuufanya ulimwengu uamini kuwa amefungal Pamoja na hivyo, Muislamu huamua kufunga kwa kujizuilia na vyote vinavyofunguza ambavyo angalikuwa na uwezo wa kuvitumia kwa siri bila ya kuonekana na mtu yeyote.
Na wakati mwingine hushikwa na kiu ya kumkausha koo na akawa na uwezo wa kupata maji baridi na kuyanywa na hata kuyatamani. Labda tungejiuliza; ni nguvu gani iliyomfanya mtu ajizuie na kula na kunywa tangu alfajiri mpaka magharibi wakati ana uwezo wa kula na kunywa bila hata ya kusimamiwa na yeyote? Tukijua kuwa huyu mfungaji hakufanya hivyo ili kupunguza uzito au hayuko katika mgomo wa kula, bila shaka atakuwa amefunga kwa ajili ya kutekeleza amri ya Allah (s.w) na kutaraji kupata radhi yake na kupata malipo makubwa aliyomuahidi. Ni usiri huu uliopo katika funga unayoifanya ibada hii iahidiwe malipo makubwa kuliko ibada nyingine kama tunavyofahamishwa katika hadithi ifuatayo:
“Abu Hurairah (r.a) ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: “Kila amali njema anayoifanya mwanaadamu italipwa mara kumi mpaka mara mia saba”. Kisha Allah (s.w) amesema: “Ila kwa Funga kwa sababu funga ni kwa ajili yangu na ni mimi mwenyewe ndiye nitakayeilipa. Anajizuia kutosheleza matashi yake ya kimwili na kuacha chakula chake kwa ajili yangu…” (Bukhari na Muslim).
Ni dhahiri kwamba mja atakapotekeleza amri hii ya kufunga Ramadhani kwa unyenyekevu kwa kutaraji kupata radhi ya Allah (s.w)
na kuepukana na ghadhabu zake, itamzidishia mja imani juu ya Allah (s.w) na malipo ya Akhera kwa maana nyingine kufunga kwa ajili ya Allah humzoesha mja kuwa muadilifu katika utekelezaji wake wa kila siku. Kile kilichomfanya asizime njaa yake na chakula alichokuwa nacho ambacho angaliweza kula kwa siri bila ya kufahamika kwa yeyote, Kile kilichomfanya asikate kiu yake kwa maji baridi ambayo anayo chumbani mwake, na kile kilichomfanya ajizuie kufanya vitendo mbalimbali vinavyofuturisha ambavyo ana uwezo wa kuvifanya kwa siri asifahamike kwa mtu yeyote, ndicho kile kile kitakachomfanya mja huyu awe muadilifu katika kutekeleza wajibu wake katika maisha yake ya kila siku. Mja huyu atakumbuka daima kuwa Allah (s.w) ni mjuzi wa kila kitu na hapana siri inayofichikana kwake. Kwa hiyo katika kutekeleza wajibu wake hatahitajia kusimamiwa na mnyapara au polisi, bali atatenda wajibu wake ipasavyo hata akiwa peke yake porini au nyikani.
(ii) Funga humzidishia mja nidhamu na utii kwa Allah (s.w)
Ukiichunguza funga ilivyo, utadhihirikiwa kuwa, haikuamrishwa ili kuwa mateso kwa waja wa Allah (s.w), bali imekusudiwa iwe zoezi maalum la kuwafanya waja wawe wacha Mungu kwa kutii kwa unyenyekevu maamrisho yote ya Allah (s.w) na kuacha kwa unyenyekevu vile vile, makatazo au makemeo yote ya Allah (s.w).
Kwanza, zoezi hili linadhihirika pale mja anapoharamishiwa katika mchana wa Ramadhani kuanzia alfajiri mpaka magharibi kula, kunywa na vinginevyo alivyohalalishiwa kuvitumia katika maisha yake yote. Kwani tumeagizwa katika Qur-an:
“Enyi watu! Kuleni vilivyo katika ardhi halali na vizuri, wala msifuate nyayo za shetani (mkala visivyo halali). Bila shaka yeye kwenu ni adui dhahiri”. (2:168).
“Enyi mlioamini! Kuleni vizuri tulivyokuruzukuni, na mumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa mnamwabudu Yeye peke yake”. (2:172).
Tunajifunza kuwa katika aya hizi na aya nyingine za Qur-an Allah (s.w) ametubainishia vilivyo halali kwetu kuvila na ametupa ruhusa ya kuvitumia maridhawa alimuradi tusivile kwa fujo au tusifanye israfu (ubadhirifu). Lakini katika mwezi wa Ramadhani vitu hivi ameviharamisha mchana kutwa kuanzia alfajiri mpaka magharibi ili kuukuza na kuudumisha utii wetu kwake. Ni kwamba, mja atakayemtii Allah (s.w) akafunga kwa kujizuia na vilivyokuwa halali siku zote na vinavyoendelea kuwa halali baada ya magharibi kuingia na kabla ya alfajiri, kwa vyovyote vile baada ya Ramadhani, haitakuwa rahisi kwake kula vilivyoharamishwa kwake siku zote.
Pili zoezi hili la utii kwa Allah (s.w) pia linapatikana katika kujizuilia kusema na kutenda maovu wakati mtu amefunga. Kama tunavyorejea katika Hadithi:
“Abu Hurairah (r.a) ameeleza kuwa Mtume wa Allah (s.a.w) amesema: “Asiyeacha kusema uwongo na kufanya vitendo viovu, Allah (s.w) si muhitaji wa kuona anaacha chakula chake na kinywaji chake (i.e. Allah (s.w) hana haja na funga yake)”. (Bukhari)
Hivyo, mja anapofunga kwa ajili ya Allah (s.w) pamoja na kujizuilia kula na kunywa vilivyo halali kwake, anajitahidi mwisho wa kujitahidi kwake kujizuilia kusema na kufanya mambo maovu na machafu kwa kuchelea kukosa malipo ya funga yake na kuambulia kiu na njaa. Kwa hiyo, funga pamoja na kukuza utii wa mja katika kujiepusha na chumo la haramu au riziki haramu, humzoesha pia mja kujiepusha na mambo yote maovu na machafu.
Tatu, pia katika funga tunapata zoezi la kumtii Allah (s.w) kwa kule kutekeleza kwa ukamilifu masharti na nguzo za funga. Hatufungi Ramadhani mpaka uonekane mwezi au mwezi wa Shaaban utimie siku 30, na hatufungui Ramadhani mpaka mwezi wa Shawwal uandame au Ramadhani ikamilishe siku 30. Tunajizuilia kula, kunywa, kujimai na kufanya vyote vinavyofunga kwa wakati maalum, kuanzia alfajiri mpaka magharibi. Ili kuona kuwa kufunga si mateso bali ni mazoezi tu ya kukuza utii wetu kwa Allah (s.w), ni vyema turejee msisitizo wa Mtume (s.a.w) juu ya kula daku na kuichelewesha na juu ya kufuturu mapema mara tu linapotua jua. Tunapata msisitizo wa kuharakisha kufuturu katika Hadithi nyingi, ifuatayo ikiwa miongoni mwa hizo:
“Abu Hurairah (r.a) ameeleza kuwa Mtume wa Allah (s.w) amesema: Allah (s.w) amesema: “Walio bora kuliko wote mbele yangu miongoni mwa waja wangu ni wale wanaoharakisha kufuturu ”. (Tirmidh).
Msisitizo wa kula daku na kuichelewesha tunaupata katika Hadithi ifu atayo:
“Anas (r.a) ameeleza kuw a Mtume w a Allah (s.w) amesema: “Kula daku kabla ya alfajiri kwa sababu daku ina baraka”. (Bukhari na Muslim).
Pia tunafahamishwa kuwa Mtume (s.a.w) aliwazoesha masahaba kuchelewesha daku kama tunavyojifunza katika Hadithi zifuatazo: Amesimulia Aysha (r.a): “Bilal alikuwa akitoa adhana usiku, kwa hiyo Mtum e w a Allah (s.w) akasem a: ‘Endeleeni kula mpaka Ibn Um Makhtuum aadhini. Kw ani haadhini mpaka alfajiri iw e imeshaingia ”. (Bukhari).
Anas (r.a) amesimulia: Zaid bin Thabit (r.a) amesema: “Tulikula daku pamoja na Mtume (s.a.w). Kisha akasimama kwa swala. “Nikauliza; Nikitambo gani kati ya (kumaliza kula) daku na adhana (ya alfajiri?” Alijibu: “Kitambo cha kutosha kusoma aya 50 za Qur-an”. (Bukhari).
Bila shaka katika Hadithi hizi tumepata msisitizo wa kuwahisha futari, kula daku na kuichelewesha. Hekima yake ni kufupisha muda wa kufunga na kuibakisha miili yetu na afya. Tunalolipata hapa kwenye kuwahi kufuturu na kula daku na kuichelewesha ni zoezi kubwa la utii kwa Allah (s.w). Hebu mfikirie mja huyu anayeitekeleza Sunnah hii ya Mtume (s.a.w) ya kuwahi kufuturu mara tu baada ya kuchwa jua. Bila shaka mja huyu atacha shughuli zake na mapema kidogo na kujitayarisha kwa swala ya magharibi, akiwa na tende au maji karibu naye ili mara tu jua linapotua afuturu pale pale. Je, huoni hali hii hukuza nidhamu ya mja na utii wake kwa Allah (s.w) na Mtume wake kama kengele ya kuingia darasani inavyokuza nidhamu na utii wa mwanafunzi kwa mwalimu wake wa somo au wa darasa? Tofauti tu iliyopo ni kwamba ambapo nidhamu na utii wa mwanafunzi unapatikana kwa kuogopa adhabu ya mwalimu wake wa darasa au somo, nidhamu na utii kwa mwenye kufunga hupatikana kwa kumuogopa Allah (s.w).
Hali kadhalika kula daku na kuichelewesha nako hukuza nidhamu na utii wa mfungaji kwa Allah (s.w). Hebu mfikirie mtu anayekatisha usingizi wake usiku wa manene au karibu na alfajiri ili ale daku jambo ambalo si la kawaida kabisa katika miezi mingine. Mfikirie vile vile yule anayekula daku katika saa za mwisho mwisho kabisa huku akiwa na saa mkononi akikazana kula chakula chake haraka kabla ya muadhini wa Alfajir. Bila shaka utaona kuwa kitendo hiki cha kuamka kula daku na kuichelewesha, kikifanywa kwa ajili ya kufuata Sunnah
ya Mtume (s.a.w) na hata kama mtu atakunywa angalau maji tu au kipande kimoja cha tende, kitakuza nidhamu na utii wa mfungaji kwa Allah na Mtume wake (s.a.w).
Nne, pia katika funga ya Ramadhani kuna Sunnah nyingi zilizoambatanishwa kama vile kusimama usiku katika swala ya Tarawehe, kuzidisha kusoma Qur-an, kukaa Itiqaf katika kumi la mwisho na kutafuta siku ya Lailatul Qadr kwa kuzidisha ibada za usiku ili kuzidisha au kukuza ucha-Mungu wa mfungaji. Ni maratajio ya kila mwenye kufunga Ramadhani kwa ajili ya Allah (s.w) na akajitahidi kutekeleza kwa ukamilifu masharti yote, nguzo zote na sunnah za funga pamoja na kutekeleza funga zilizoambatanishwa na mwezi wa Ramadhani, kuwa baada ya Ramadhani atakuwa na nidhamu na utii wa hali ya juu kwa Allah (s.w) na Mtume wake (s.a.w) katika kutekeleza maamrisho na hukumu zote za Allah (s.w) katika kuendesha maisha yake ya kila siku.
(iii) Funga humzoesha mja kumiliki matashi ya Unyama wake
‘Funga pia inatupa zoezi la kuumiliki unyama wetu. Tumeshaona kuwa japo mwanaadamu ana mwili kama wanyama na ana matashi ya kinyama kama vile kula, kunywa, kujamii, kupumzika, kulala na kadhalika, si mnyama bali ni mtu ambaye umbile lake ni mchanganyiko wa mwili ambao asili yake ni udongo na roho ambayo hutoka kwa Allah (s.w). Ambapo mwili humng’ang’aniza mwanaadamu kurudi chini katika ardhi ili kujipatia maslahi ya kinyama yatokayo ardhini. Roho humnyanyua mwanaadamu juu ili kukidhi mahitaji ya kiutu au mahitaji ya kimaadili yapatikanayo kutoka kwa Allah (s.w).
Ilivyo ni kwamba, iwapo matashi ya kimwili yatamtawala mwanaadamu, basi mwanadamu hapa ulimwenguni ataishi kama mnyama au hali duni zaidi kuliko ile ya mnyama japo atakuwa analala ndani ya nyumba, analala kitandani na anakula vyakaula vizuri vilivyopikwa vizuri na kuandaliwa vizuri. Kwa upande mwingine iwapo maadili ya kiroho ndiyo yatakayomtawala mwanaadamu, basi mwanaadamu ataishi kama Khalifa wa Allah (s.w) hapa ulimwenguni na hadhi yake mbele ya Allah (s.w) itakuwa ya juu kuliko ile ya malaika. Ni vyema vile vile tufahamu kuwa mwanaadamu ana uhuru kamili wa kuamua ama kujishusha hadhi yake kuwa chini kuliko walio chini au kuipandisha hadhi yake kuwa juu kuliko ile ya malaika. Mwanaadamu atakapoamua kuyafanya matashi ya unyama wake kuwa ndio Mungu wake na kuyaabudu na kuyanyenyekea basi hadhi yake hapa duniani itakuwa chini kuliko ile ya wanayama. Rejea Qur-an:
“Je, umemuona yule aliyefanya matamanio yake kuwa mungu wake? Basi je utaweza kuwa mlinzi wake, au je, unafikiri ya kwamba wengi katika wao wanasikia au wanafahamu? Hawakuwa hao ila ni kama w anyama, bali w ao w amepotea zaidi njia.” (25:43-44)
Na mwanaadamu atakapomfanya Allah (s.w) kuwa ndiye Mola wake, akamtii kwa unyenyekevu yeye pekee, basi hadhi yake itakuwa ni ile ya ukhalifa (ya mtawala wa ulimwengu kwa niaba ya Allah (s.w)) yenye daraja kuliko hadhi ya malaika. Rejea Qur-an (2:30-34)
Muumini anapofunga huyakandamiza matashi ya unyama wake kama vile kula, kunywa, kujamii na kadhalika kwa ajili tu ya kumtii Allah (s.w). Kitendo cha mja kuamua kwa hiari yake kuacha kula, na huku ana njaa, kuacha kunywa na huku ana kiu na kuacha kutumia vitu mbali mbali na huku anavihitajia, huudunisha unyama wake na kuuweka chini ya utawala wa maadili ya kiroho yanayotoka kwa Allah (s.w). Ni vyema tukumbuke kuwa katika sheria ya kawaida ya maumbile, kuwa kila mwili unapokuwa dhaifu ndivyo matashi na matamanio ya kimwili (kinyama) yanavyopungua au kuwa dhaifu. Kwa mfano mtu mwenye matamanio makubwa ya kujamii ameshauriwa afunge. Pia vijana wasiopata uwezo wa kuoa wameshauriwa wafunge ili wakate matamanio yao yatakayoweza kuwapelekea kuzini. Hebu turejee ushauri huu katika hadithi ifuatayo:
“Amesimulia Alqama (r.a): “Nilipokuw a ninatembea pamoja na Abdullah (r.a) alisema: Tulikuwa pamoja na Mtume (s.a.w) akasema: “Yule mwenye uwezo wa kuoa na aoe kwa sababu itamsaidia kujizuilia kuangalia wanawake (kwa matamanio) na itamsaidia kuhifadhi tupu yake kutoiendea zinaa, na yule asiyemudu kuoa anashauriwa afunge kwani funga itapunguza nguvu ”. (Bukhari)
Allah (s.w) ndiye aliyetuumba na matashi ya kimwili tuliyonayo. Hivyo ni yeye pekee anayefahamu ni namna gani tutayamiliki matashi yetu ili pamoja na kuyatosheleza tubakie na utu wetu. Basi ametuwekea funga kama njia ya kumiliki matashi ya unyama wetu.
Mja aliyefunga mwezi wa Ramadhani kwa ajili ya Allah na kwa kuzingatia masharti na nguzo za funga, anatarajiwa awe na uwezo wa kukandamiza matashi ya unyama wake pale yanapompelekea kuchupa mipaka ya Allah (s.w). Muislamu mwenye kufunga Ramadhani vilivyo, hatarajiwi kabisa kutosheleza matashi yake kinyume na utaratibu aliouweka Allah (s.w).
(iv) Funga humzoesha mja kuwahurumia wanaadamu wenzake
Funga pia inatoa mafunzo ya huruma. Kwa fukara au masikini kushinda njaa na kula mara moja kwa siku si jambo kubwa wala ajabu sana. Lakini kwa tajiri ambaye anavyo vyakula vingi na vizuri vilivyomzunguka na ambaye ana wasaa wa kuvila, kushinda njaa na kiu ni ajabu kubwa na jambo zito kwake. Hivyo tajiri anayefunga kwa ajili ya Allah atapata wasaa wa kuona hali ya njaa wanayokuwanayo mafakiri, masikini. Mayatima, wasafiri walioharibikiwa kwa sababu ya kukosa uwezo wa kujipatia chakula. Mafunzo haya aliyoyapata katika funga yatampa msukumo wa kuwahurumia fukara, masikini, mayatima, wasafiri walioharibikiwa na wengine waliokumbwa na njaa na kuwalisha chakula kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah (s.w) tu.
Vile vile kuzidisha kutoa sadaqa katika mwezi wa Ramadhani na kuwafuturisha waliofunga ni miongoni mwa sunnah zilizokokotezwa. Kama tulivyojifunza katika hadithi ya Ibn Abbas(r.a), Mtume (s.a.w) alikuwa mpole na mkarimu sana katika mwezi wa Ramadhani kuliko kawaida yake katika miezi mingine. Hapakuwa na muombaji yeyote aliyekuja kwake akarudi mikono mitupu kutoka mlangoni kwake.
Pia Ibn Abbas (r.a) ameeleza kuwa mwezi wa Ramadhani ulipoingia alikuwa akiwaacha huru watumwa - mateka wa vita - na alikuwa akitoa sadaqa kwa kila muombaji (Baihaqi).
Mfungaji tajiri akijitahidi kutekeleza Sunnah hizi katika mwezi mzima wa Ramadhani, atapata zoezi la kumwezesha kuwahurumia watu wengine na kuwalisha masikini kwa kadri ya uwezo wake katika miezi kumi na moja ya mwaka inayofuatia Ramadhani.
Halikadhalika utoaji wa Zakatul-fitri hutupa zoezi hilo hilo la kuwahurumia wengine, kwamba mtu akipata kiasi cha chakula kinachotosha kwa siku moja pamoja na wale walio chini ya uangalizi wake, anawajibika kutoa ziada iliyobakia kwa jirani yake ambaye hana kabisa. Zoezi hili ni muhimu sana kwani hatutakuwa waumini endapo tutashiba na ilihali majirani zetu wanalala njaa. Ibn Abbas (r.a) am e s im u lia:
“Nimemsikia Mtume wa Allah akisema: “Si muumini yule ambaye anashiba na ili hali jirani yake pembeni analala njaa.” (Baihaqi).
Hata kufunga kwenyewe bila ya kuambatanisha na utoaji wa sadaqa na zakatul fitr, kunamlainisha tajiri na kuwa mpole kwa wengine na kuwa mnyenyekevu kwa Mola Karim. Ilivyo ni kwamba katika kawaida ya maisha mtu mnyonge na dhaifu daima hujidhalilisha mbele ya matajiri na wenye uwezo. Kwa upande mwingine matajiri na wenye uwezo hutakabari na hujiona bora zaidi kuliko wanyonge. Tajiri na mwenye uwezo anapofunga njaa na kiu humfanya awe mnyonge na dhaifu, na hujiona yeye bora chochote, bali aliye bora kuliko wote ni Allah (s.w) pekee. Kwa hiyo, tajiri mwenye nguvu na mwenye hadhi katika jamii, atakapofunga kwa ajili ya Allah (s.w) atapata zoezi la kumzuia na takaburi juu ya wanyonge na atapata zoezi la kuwahurumia wengine. Funga huwakumbusha matajiri, wenye wadhifa na wenye nguvu mawaidha ya aya ifuatayo:
“Enyi watu! Kwa hakika tumekuumbeni (nyote) kwa (yule) mwanaume (mmoja) Adam na (yule yule) mwanamke (mmoja Hawwa). Na tumekufanyeni mataifa na makabila (mbali mbali) ili mjuane (tu basi). Hakika aheshimiw aye sana miongoni mw enu mbele ya Mw enyezi Mungu ni yule aliye Mcha Mungu zaidi katika nyinyi. Kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mwenye habari za mambo yote. (49:13)
(v) Funga humpatia mfungaji siha
Mtume (s.a.w) amesema: “Fungeni mtakuwa na afya”. (Tabrani).
Imethibitika katika utafiti wa madaktari kuwa kufunga ni matibabu ya baadhi ya maradhi na kwamba funga ni kinga ya baadhi ya maradhi.
Kwanza, mwili wa mwanaadamu unahitaji mapumziko baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu. Baada ya mapumziko, mtu hupata nguvu mpya wakati anaporejea kazini na ufanyaji wake unakuwa na ufanisi zaidi. Hali kadhalika matumbo yetu yanahitaji mapumziko kidogo kwa mwaka kwa muda tunaofunga, ili yaweze kuifanya kazi yake kwa ufanisi zaidi na kuupatia mwili afya inayostahiki Madaktari wengi katika sehemu mbali mbali huwashauri wagonjwa wa baadhi ya magonjwa ya kudumu kujiepusha na baadhi ya vyakula, kujizuia kulal kula ovyo, na kupunguza kula ili kujilinda na magonjwa yanayotokana na kula kula ovyo au kula lma kwa mara vyakula mchanganyiko.
Pili, imegunduliwa katika utafiti kuwa tumboni kuna aina Fulani ya dawa (acidities) ambazo hutokea kutokana na njaa na kiu, ambazo huua vijidudu vya magonjwa ya aina mbali mbali. Takwimu zinaonyesha kuwa magonjwa mengi yanayotokana na usagaji wa chakula, hayapatikani kwa wingi kwa watu wenye kawaida ya kufunga mwezi mmoja kila mwaka.
Tatu, binaadamu anapokula chakula mwili hutumia kiasi tu cha chakula kinachohitajika kwa wakati ule. Ziada yoyote ya chakula hubadilishwa kutoka hali yake ya kawaida na kuwa katika hali ambayo kitafaa kutunzwa na kuwekwa akiba kwa matumizi ya baadaye. Hali hii ya mwili ya kuweka akiba huendelea siku hadi siku. Lakini mwili wa binaadamu unakikomo cha uwezo wa kutunza chakula hiki cha akiba. Kama miaka kwa miaka akiba zitazidi kurundikana tu bila kutumiwa, akiba ya zamani huharibika na kuwa sumu kwa mwili.
Mfungaji wa Ramadhani hawezi kudhuriwa na akiba hizi za chakula mwilini mwake, kwani akiba zote zilizotunzwa mwilini kwa miezi kumi na moja hutumika katika mwezi mmoja wa Ramadhani. Hii ni kwa sababu katika masaa 12 hadi 14 ya kufunga, ambapo mfungaji hali wala hanywi, mahitaji ya mwili ya chakula hutoshelezwa na ile akiba. Tukumbuke kuwa aliyetuumba ni Allah (s.w) na ndiye aliyetuamrisha kufunga mwezi mmoja kwa mwaka katika masaa hayo ya kufunga. Hivyo kiasi hicho cha funga katika mwaka kinatosha kusafisha akiba ya chakula cha mwaka ambayo ikiendelea kubakia itadhuru miili yetu kwa njia moja au nyingine.
Umuhimu wa siha hauna budi kuzingatiwa ipasavyo. Ni kwamba kipando cha kuifikisha roho kwenye lengo lake ni mwili. Mwili ukiwa hauna afya nzuri, basi roho yenyewe haitaweza kuusimamisha ufalme wa Allah (s.w) hapa ulimwenguni. Ni katika msingi huu Mtume (s.a.w) amesema: “Waumini wote ni bora mbele ya Allah (s.w), lakini aliyebora ziadi miongoni mwenu ni yule mwenye siha nzuri”.
Umma wa Waislamu katika mwezi wa Ramadhani huzidisha kufanya wema na kuamrisha wengine kufanya hivyo, pia hujitahidi
kuacha maovu na kukataza maovu, hujitahidi kusaidiana na kuhurumiana na kuufanya ulimwengu kuwa na furaha na amani zaidi. Mwenendo huu wa Waislamu kuamrisha mema na kukataza maovu, kuhurumiana na kupendana ndio mwenendo wanaotakiwa wawe nao Waislamu ili waweze kuwa Makhalifa wa Allah (s.w) hapa ulimwenguni.
Je! umeipenda hii post?
Ndio Hapana Save post
Rajabu Tarehe 2024-05-10 14:53:23 Download PDF Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 733
Sponsored links
👉1 Kitau cha Fiqh
👉2 Kitabu cha Afya
👉3 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)
👉4 kitabu cha Simulizi
👉5 Madrasa kiganjani
Kwa nini waislamu wanaoa mke zaidi ya mmoja
Post hiibitakugundisha hekima ya kuruhusiwa kuoa mke zaidi ya mmoja katika sheria za kiislamu. Soma Zaidi...
Suluhu na kupatanisha kati ya mke na mume
Soma Zaidi...
Kumuandaa maiti kabla ya kufa na baada ya kufa, mambo muhimu anayopasa kufanyiwa maiti wa kiislamu
3. Soma Zaidi...
IBADA YA HIJA NA NAMNA YA KUITEKELEZA
Soma Zaidi...
Ni watu gani wanaopewa Zaka
Soma Zaidi...
Namna ya kuswali swala ya maiti: nguzo zake, sunnah zake na maandalizi juu ya maiti
3. Soma Zaidi...
Ni yapi mambo yanayoharibu Swaumu na Mambo yanayobatilisha funga
Soma Zaidi...
Namna ya kurithisgha hatuwa kwa hatuwa.
Hspa utajifunza sasa jinsi ya kugawa mirathi kutokana na viwango maalumu. Soma Zaidi...
Sunnah za swaumu, sunnah ambazo zinaambatans ns kufungabmwezi wa Ramadhani
Yajuwe mambo ambayo yanapendeza kuyafanya wakati ukiwa umefunga Ramadhani. Soma Zaidi...
Namna ya kuswali
2. Soma Zaidi...
Haki za viumbe na mazingira
Haki na uadilifu katika uislamu (EDK form 3: Dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...