Yusufu(a.s.) aliwasamehe na kuwaagiza waende wakamlete baba yao mzee Yaaqub(a.s.) na wao waje wote na familia zao.
Akasema: “Hakuna lawama juu yenu leo; Mwenyezi Mungu atakusameheni, naye ni Mwenye rehema zaidi kuliko wanaorehemu. (12:92)
Nendeni na kanzu yangu hii na muiweke mbele ya uso wa baba yangu: naye atafunuka macho aone. Na nijieni pamoja na watu wenu wote(12:93)
Waliporudi nyumbani walichukuzana wote, familia nzima akiwemo baba yao, mzee Ya’aquub(a.s),wakahamia Misri.
Na walipoingia kwa Yusufu aliwakumbatia wazazi wake na akasema; “Ingieni Misri, Inshaa-Allah mumo katika amani. (12:99)
Aliwainua wazazi wake na kuwaweka katika kiti cha Ufalme. Na wote wakaporomoka kumsujudia. Na Yusufu akasema: “Ewe babangu! Hii ndiyo hakika ya ndoto yangu ya zamani. Hakika Mola wangu ameithibitisha. Na amenifanyia hisani akanitoa gerezani na akakuleteni ninyi kutoka jangwani; baada ya Shetani kuchochea baina yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu ni mwenye kulifikia alitakalo. Bila shaka Yeye ni Mjuzi na Mwenye hekima.(12:100)
Shukurani za Nabii Yusufu(a.s) kwa Allah(s.w)
“Ee Mola wangu! Hakika umenipa Ufalme na umenifundisha tafsiri ya mambo. Ewe Muumba wa mbingu na ardhi! Wewe ndiye Mlinzi wangu katika dunia na Akhera. Nifishe hali ya kuwa ni Muislamu na unichanganyishe na watendao mema (12:101)