image

Historia ya Al-Khidhri

Jina Al-Khidhri halikutajwa mahali popote katika Qur’an.

Historia ya Al-Khidhri

Historia ya Al-Khidhri


Jina Al-Khidhri halikutajwa mahali popote katika Qur’an. Ila Hadith sahihi za Mtume(s.a.w) na vitabu kadhaa ya historia vimemtaja mja wa Allah habari zake zilizobainishwa katika Qur’an (18:60-82) kuwa ndiye Al-Khidhri. Upo utata katika kubaini uhakika wa Al-Khidhri kwamba alikuwa binadamu au malaika. Sheikh Abdallah Saleh Farsy katika tafsiri yake ya Qur’an anasema Khidhri alikuwa binadamu na Mtume ila alikuwa amepewa neema ya elimu ya ghaibu. Yaani alipewa uwezo wa kujua mambo yasiyo wazi au yasiyofahamika kwa kutumia uwezo wa milango ya fahamu ya kawaida tuliyonayo.Sheikh Abul Ala Mauduud, anasema ama Khidhri alikuwa malaika au kiumbe kingine ambacho utendaji wake hauongozwi na sheria hizi za kawaida zinazowaongoza wanaadamu. Hoja zake ni kuwa Khidhri alitoboa jahazi la mtu na akaua kijana. Japo maelezo yanatolewa kuwa alifanya hivyo kwa sababu ya elimu ya ghaibu aliyoletewa na Mwenyezi Mungu kwamba atoboe jahazi ili isije likaporwa kwa kuonekana zuri na pili amuue kijana kwa kuhofia atakuja kuwa mbaya baadae, lakini huo si ushahidi mbele ya sheria za Mwenyezi Mungu zinazowahukumu watu hapa duniani. Kwa hoja hiyo Mauduud anadhani Khidhri alikuwa malaika anayepokea amri na kufanya kama anavyoamrishwa na Allah au vinginevyo alikuwa kiumbe wa hali (nature) nyingine lakini si Mtume.Kisa cha Al-Khidhri kinaanzia pale Mtume Musa (a.s) alipoweka azma ya kufanya safari hadi afikie makutano ya bahari mbili:

Na (kumbukeni) Musa alipomwambia kijana wake: “Nitaendelea tu kwenda mpaka nifike katika maungano ya bahari mbili; au niendelee karne na karne (mpaka nikutane na huyo ninayetaka kukutana naye)” (18:60).“Basi walipofika wote wawili (mahali) zinapoungana (hizo bahari mbili) walimsahau samaki wao; naye akashika njia yake kwenda baharini; hali ya kuwa inafanya alama” (18:61).Na walipofika mbele (Musa) alimwambia kijana wake: “Tutoe chakula chetu cha asubuhi, maana tumepata uchovu (mkubwa) katika safari yetu hii” (18:62).Akasema: “Unaona! Pale tulipopumzika katika mlima basi hapo nimesahau (kukupa habari za) yule samaki. Na hakuna aliynisahaulisha isipokuwa shetani, nisikumbuke. Naye akashika njia yake baharini kwa namna ya ajabu” (18:63).(Musa) akasema: “Hapo ndipo tulipokuwa tunapataka”. Basi wakarudi nyuma kwa kufuata njia yao (ile ile)” (18:64).

Basi wakamkuta mja katika waja wetu tuliyempa rehema kutoka kwetu na tuliyemuelimisha ilimu (nyingi) zinazotoka kwetu” (18:65).Musa akamwambia: “Je! Nikufuate ili unifundishe katika ule uwongofu uliofundishwa?” (18:66).Kwa mujibu wa mafundisho ya aya hizi, yaelekea Mtume Musa(a.s) alikuwa amepewa maelekezo na Allah(s.w) amtafute Khidhri akapate mwongozo na mafundisho kadhaa kupitia kwake. Makutano ya bahari mbili yaelekea ndipo Nabii Musa alipotakiwa akutane na Khidhri.Mtume Musa(a.s) alikuwa na elimu ya kutosha kufanya kazi yake ya Utume kwa watu wake. Lakini hakuwa na elimu ya mambo yasiyo dhahiri. Kwa sababu hiyo Khidhri alikataa ombi la Mtume Musa la kutaka kuandamana naye. Hata hivyo baadaye alimkubalia ila kwa sharti kuwa asimuulize chochote katika yale atakayomuona anayafanya. Qur’an inabainisha hali hii katika aya zifuatazo:
Musa akamwambia: “Je! Nikufuate ili unifundishe katika ule uwongofu uliofundishwa?” akasema: “Hakika wewe huwezi kuvumilia kuwa pamoja nami. (Utaona usiyoweza kustahimili kuyaona)”. “Na utawezaje kuvumilia yake usiyojua hakika yake?” Akasema: “Akipenda Mwenyezi Mungu, utaniona mvumilivu, wala sitaasi amri yako”. Akasema: “Basi kama

utanifuata, usiniulize kwa lolote (utakaloliona) mpaka mimi nianze kukwambia” (18:66-70).

Kwa makubaliano hayo Nabii Musa(a.s) akafuatana na Khidhri. Lakini kama Khdhri alivyoonesha wasiwasi, Musa hakuweza kustahimili matendo ya Khidhri. Awali Khidhri alitoboa jahazi waliyopanda. Musa hakustahimili ikabidi aulize kulikoni:


Hata walipopanda jahazi (yule Khidhri) aliitoboa. (Musa) akasema, “Je! Umeitoboa ili uwazamishe waliomo? Hakika umefanya jambo baya”. (18:71).

Khidhri ilibidi amkumbushe sharti la kuandamana naye. Musa akaomba msamaha wakaendelea. Mbele ya safari wakamkuta kijana mdogo Khidhri akamuua. Hili nalo Musa hakuweza kuhimili. Ikabidi amuulize Khidhri kwanini amemuua kijana asiye na hatia. Qur’an inatuambia:Basi wote wawili wakaendelea kwenda. Hata wakamkuta kijana mdogo, na (yule Khidhri) akamuua. (Musa) akasema: “Ala! Umemuua mtu asiye na kosa wala hakumuua mtu? Bila shaka umefanya jambo baya kabisa” (18:74).

Nabii Musa(a.s) akakumbushwa tena makubaliano yao na akaomba msamaha.

Hatimaye walifika katika mji ambapo waliomba chakula lakini wakanyimwa. Wakakuta ukuta wa moja ya nyumba za mjini hapo

unakaribia kuanguka. Khidhri akausimamisha. Hapa Musa aliuliza tena. Hii ikiwa ni mara ya tatu Musa kukhalifu makubaliano yao; Khidhri hakumsamehe tena. Khidhri akamsimulia hikma na tafsiri ya yote aliyoyafanya kisha wakafarikiana. Qur’an inatuambia:


(Khidhri) akasema: “Huku ndiko kufarikiana baina ya mimi na wewe. Hivi sasa nitakwambia hakika ya yale ambayo hukuweza kuyavumilia”.“Ama ile jahazi, ilikuwa ya masikini wafanyao kazi baharini, na nilitaka kuiharibu kwani mbele yao kulikuwa na mfalme anayekamata kila jahazi (zuri) kwa jeuri”. “Na ama yule kijana, wazazi wake walikuwa Waislamu kamili, tukahofia kwamba asije akawapelekea (wazee wake hao) katika uasi na ukafiri. Basi tulitaka Mola wao Awabadilishie mtoto aliye bora kuliko yeye kwa kutakasika, na aliye karibu zaidi kwa huruma”. Na ama ukuta ulikuwa wa watoto wawili mayatima mjni pale, na chini yake kulikuwa na khazina yao, na baba yao alikuwa mwema, kwa hivyo, Mola wako alitaka wafikie baleghe yao na wajitolee khazina yao. Hiyo ni rehema inayotoka kwa Mola wako. Nami sikufanya haya kwa amri yangu. Hiyo ndiyo hakika ya yale ambayo hukuweza kuyavumilia” (18:78-82).Mafunzo yatokanayo na historia ya Khidhr:


Kwanza, Ni hali ya kawaida kwa binaadamu kupitisha maamuzi yake kutokana na taafira za wazi na matukio bayana. Undani na hikma ya matukio hufahamika kwa wale tu waliotunukiwa hikma na fikra zilizotulizana. Katika maisha ya kila siku wafalme na watawala jeuri hupita katika ardhi wakifuja neema za Allah(s.w) huku wakiwadhalilisha wengine kwa jeuri. Watu wema na watiifu kwa Mola wao wakati mwingine waweza kuonekana dhalili wasio na mali wala cheo katika jamii. Wasiomuamini Allah(s.w) wakiwa na mali na vyeo hutakabari na kumkana Mwenyezi Mungu. Wakaona maguvu yao ndio kila kitu kwa hiyo wakazidisha fisadi katika ardhi.Pili, Kwa waumini uangalifu wahitajika vile vile kwa mtu anayetenda mema lakini hali yake kiuchumi kila siku inazidi kushuka ilhali makafiri wanazidi kujilimbikizia mali; aweza kuvunjika moyo na kukata tamaa.Tatu, Kisa hiki cha Musa(a.s) na Khidhri kinatubainishia kuwa zaidi ya elimu hii tunayoidhibiti kwa milango yetu ya fahamu ipo hikma ya mambo mengi ambayo hatuijui mpaka tufunuliwe na Allah(s.w) Mtu aweza kuwa na neema fulani kumbe neema hiyo ni yenye shari na yeye. Na kinyume chake.Nne, Ili Mtume Musa(a.s) apate kufahamu japo sehemu ndogo ya elimu aliyonayo Khidhri ilibidi afunge safari ndefu. Elimu yote ni milki ya Allah na humkunjulia amtakaye kiasi atakacho. Lakini pia juhudi kubwa sana inahitajika katika kutafuta elimu.Tano, Kisa hiki ni kiashiria cha upana wa elimu ya Allah(s.w). Mtume Musa(a.s) alikuwa Mtume na aliletewa Wahay akafahamu mambo mengi sana. Hata hivyo anakutana na Khidhri mwenye elimu ambayo kwa Musa(a.s) inaonekana kama miujiza.Sita, Mambo matatu aliyoyafanya Khidhri akiwa na Mtume Musa(a.s) yanatupa mafundisho yafuatayo: Mosi; hasara au uharibifu wa jambo fulani yaweza kuwa ndio kheri yenyewe. Kutobolewa kwa jahazi kulilifanya lionekane si zuri. Hii ilifanya kinga kumzuia mfalme asilipore. Pili; ukatili wakati mwingine waweza kuwa ndio amani na msaada kwa watu. Maisha hutolewa muhanga kwa faida ya Ummah. Tatu; matendo ya wema si lazima yazae matunda hapo hapo. Wema unahimizwa hata pale ambapo hakuna dalili ya kulipwa wema.                              

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Kama unahitaji kuuliza maswali Bofya hapa

Mwandhishi Tarehe 2018-08-01     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 565


Download our Apps
👉1 Kitabu cha Afya     👉2 Madrasa kiganjani     👉3 kitabu cha Simulizi     👉4 Kitau cha Fiqh    

Post zifazofanana:-

Mtume Muhammad alelewa na mama yake mzazi akiwa na umri wa miaka 4.
Sura na historia ya Mtume Muhammad S.A.W sehemu ya 8. Hapa utajifunza malezi ya Mtume kutokakwa Halimavkuja kwa mama yake. Soma Zaidi...

tarekh
MAPIGANO YA AL-FIJAR (MAPIGANO YA UOVU). Soma Zaidi...

Watu wa Mji Waliomuua Muislamu kwa Kuwa Amewasadikisha Wajumbe wa Allah(s.w)
Katika Suratul Yassin Allah(s. Soma Zaidi...

Hatua mbili kuu za kushuka kwa Quran
Quran (EDK form 2: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...

Historia ya Luqman mtu aliyesifika kuwa na Hikma
Luqman ni katika watu wema kabisa waliopita zama za nyuma. Soma Zaidi...

Mfumo wa ulinzi na usalama katika fola ya uislamu madinah
Dola ya uislamu madinah (EDK form 3: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...

Mtume(s.a.w) Kulingania Uislamu Siku za Hija
Baada ya Mtume(s. Soma Zaidi...

Kuandaliwa kwa Muhammad kabla ya kupewa utume
Bara arabu zama za jahiliyyah (EDK form 2 dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...

Mitihani aliyopewa Nabii Ibrahimu kutoka kwa Allah
Tumeona katika historia yake kuwa Nabii Ibrahiim(a. Soma Zaidi...

Ijuwe Dua ya Ayyuub(a.s)
Nabii Ayyuub(a. Soma Zaidi...

MAMA YAKE MTUME MUHAMMAD (S.A.W) ANAMLEA MTUME MUHAMAD AKIWA NA UMRI WA MIAKA MINNE (4)
KULELEWA NA MAMA YAKE ALIPOFIKA MIAKA MINNEMtume (s. Soma Zaidi...

Uchaguzi wa Ali bin Abu Twalib kuwa Khalifa wa nne na chanzo cha Makundi katika Uislamu
Soma Zaidi...