Wapinzani wa Ujumbe wa Nabii Salih(a.s)


Baada ya Nabii Salih(a.s) kufikisha ujumbe wa Allah(s.w) kwa ufasaha na kwa uwazi, watu wake waligawanyika makundi mawili.

Wachache wao waliamini, wengi katika hao wakiwa dhaifu.Wengi wao wakiongozwa na wakuu wa jamii walikufuru. Makafiri wa Kithamud waliukataa ujumbe wa Nabii Salih(a.s) kwa sababu zifuatazo:Kwanza, Walimuona Salih(a.s) kuwa ni mwongo, kuwa hapana cha kuwepo Allah wala adhabu kutoka kwake.

Wakasema wale waliotakabari “Sisi tunayakataa yale mnayoyaamini. Na wakamtumbua (wakamuua) yule ngamia na wakaasi amri ya Mola wao na wakasema: “Ee Salih! Tuletee unayotuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume. (7:76-77)Wakamchinja. Basi (Salih) akasema: “Stareheni katika mji wenu huu (muda wa) siku tatu (tu, kisha mtaadhibiwa); hiyo ni ahadi isiyokuwa ya uwongo.” (11:65)Pili,hawakuwa tayari kuacha miungu ya Babu zao:

Wakasema: “Ewe Salih! Bila shaka ulikuwa unayetarajiwa (kheri) kwetu kabla ya haya (Sasa umeharibika). Oh! Unatukataza kuabudu waliowaabudu baba zetu? Na hakika sisi tumo katika shaka inayotusugua (katika nyoyo zetu) kwa haya unayotuitia.” (11:62)Tatu, walimuona Salih(a.s) kama mtu aliyerogwa na wakamdai kuleta muujiza:

Wakasema “Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa (wakakosa akili).” “Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi; basi lete muujiza ikiwa ni miongoni mwa wasemao kweli.” (26:153-154)

Nne, walidai kuwa Salih(a.s) na wale waliomuamini pamoja naye wameleta nuksi katika nchi kwa kule kuikataa kwao miungu ya masanamu. Wakasema: “Tumepata bahati mbaya, (ukorofi) kwa Sababu yako na kwa Sababu ya wale walio pamoja nawe.” Akasema: “Ukorofi wenu uko kwa Mwenyezi Mungu (kwa ajili ya ubaya wenu;) lakini nyinyi ni watu mnaojaribiwa (na Mwenyezi Mungu kuwa mtafuata au hamfuati).” (27:47)