Mbinu za Mtume Salih(a.s) Katika Kulingania Uislamu


Kama Mitume waliotangulia, Nabii Salih(a.s) naye kwa kuzingatia mazingira ya watu wake, alitumia mbinu zifuatazo katika kuulingania Uislamu:Kwanza, alijieleza kwa uwazi kuwa yeye ni Mtume wa Allah(s.w)“Bila shaka mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.” (26:143)

Pili, aliwakumbusha watu wake neema za Allah(s.w) zilizo juu yao ili waone umuhimu wa kumshukuru na kumuabudu ipasavyo:
“Na kumbukeni (Mwenyezi Mungu) alivyokufanyeni makhalifa baada ya ‘Ad na kukuwekeni vizuri katika ardhi mnajenga majumba makubwa ya kifalme katika nyanda zake, na mnachonga majumba katika majabali (yake). Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu, wala msifisidi katika ardhi kwa kufanya uharibifu.” (7:74)“Je (mnafikiri kuwa) mtaachwa salama katika haya yaliyopo hapa (kwenu):” “Katika mabustani na chemchem, (mito).” “Na mimea na mitende yenye makole mazuri.” “Na mnachonga milimani majumba mkistarehe tu basi.” (26:146-149)Tatu, aliwanasihi na kuwasisitiza watu wake wamche Allah(s.w)
na kumtii yeye badala ya kuwatii watu:“Mcheni Allah na mtiini. Wala msitii amri za wale maasi (wenye kupindukia mipaka ya Allah). Ambao wanafanya uharibifu tu katika ardhi wala hawaitengenezi.” (26:150-152)

Nne,alisisitiza kutohitajia ujira kwa watu wake, kama walivyozoea kutoa ujira kwa viongozi wao kwa ajili ya manufaa na starehe zao binafsi.“Wala sikutakini ujira juu yake, ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.” (26:145)

Tano, alionyesha muujiza wa jabali kuzaa ngamia jike kama dalili za Utume wake baada ya watu wake kumtaka afanye hivyo kwa uwezo wa Allah(s.w).Akasema: “Enyi watu wangu! Mnaonaje, kama ninazo dalili zilizo wazi zitokazo kwa Mola wangu (za kunionyesha ukweli wa haya), naye amenipa rehema kutoka kwake, basi ni nani atakayeninusuru kwa Mwenyezi Mungu kama nikimuasi? Basi hamtanizidishia kwa hayo mnayonitakia ila khasara.(11:63)Enyi watu wangu! Huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu ni Ishara kwenu (mliyoitaka kwangu ili kuonyesha ukweli wa Utume wangu). Basi muacheni ale katika ardhi ya Mwenyezi Mungu; wala msimguse kwa ubaya isije ikakuangamizeni adhabu iliyo karibu (na kukufikieni).” (11:64)