Imam Malik bin AnasKwa mujibu wa “Kitab al-Ansab na Dhahabi, Tadhkirah al- Huffaz” juzuu ya kwanza, Imam Malik alizaliwa mwaka 93 A.H. Baadhi ya vitabu vimetaja pia mwaka 94 na 95 A.H. Wazazi wa Imam Malik walitoka katika familia ya kifalme ya Kiarabu toka Yemen ambayo ilihamia Madinah. Wakati anazaliwa Imam Malik dola ya Kiislamu ilikuwa chini ya uongozi wa Khalifa Walid bin Abd- al-Malik na japo makao makuu ya dola yalikuwa yamehamishiwa Damascus, Syria, lakini mji wa Madinah ulibakia mashuhuri na kitovu cha elimu ya Uislamu. Familia ya Imam Malik ilizungukwa na ndugu na jamaa wa karibu waliokuwa na elimu ya kutosha.


Hivyo alianza kupata elimu yake katika mazingira ya nyumbani. Zaidi ya hapo alisoma kwa waalimu wengine saba mashuhuri wa fani mbalimbali, miongoni mwao alikuwa Jafar al-Sadiq, kitukuu cha Imam Hussein. Pamoja na kujikusanyia elimu nyingi, umaarufu wa Imam Malik ulizidi kuvuma kutokana na unyenyekevu na ucha Mungu wake. Watu walitoka masafa ya mbali kuja Madina kuhudhuria darsa za Imam Malik.


Sehemu kubwa ya muda wake aliitoa kwa kufundisha na akiifurahia kazi hii. Japo Imam Malik alikuwa mtaalam mzuri wa Hadith, lakini alikuwa dhaifu kidogo katika mambo ya sheria na kutoa fa-twa za kifiqh. Hata hivyo alikuwa mtu madhubuti na mwenye msimamo. Hakukubali kutolewa katika haki kwa hali yoyote iwayo. Wakati fulani alitoa fa’twa ambayo ilikuwa kinyume na matakwa ya Gavana wa Madinah. Gavana alimuonya asitoe fa’twa hiyo hadharani, lakini kwa kuridhika kuwa ndio haki, Imam Malik alitoa maoni yake hadharani na akachapwa viboko hadharani kwa tendo hilo. Katika kazi muhimu alizoziacha Imam Malik ni kitabu chake al-Muwatta chenye mjumuiko wa Hadith na mafundisho ya Mtume(s.a.w) ya ibada na mas’ala mbalimbali ya Kiislamu. Imam Malik alitawafu mwaka 179A.H.Madinah.