Khalifa na Utungaji SheriaKhalifa kama ilivyokwishaoneshwa sio mtungaji wa sheria kama ilivyo kwa marais wa leo na mabunge yao. Khalifa ni mtekelezaji wa sheria za Mwenyezi Mungu na msimamizi mkuu wa sheria za Mwenyezi Mungu. Katika kipindi cha Ukhalifa vyanzo vya sheria vilibakia kuwa Qur’an, Sunnah na Ijmaa na baadaye Umar, Khalifa wa pili, aliongeza Qiyas. Kwa hali hii Ufalme katika Dola ya Kiislamu ulibaki kuwa ni wa Mwenyezi Mungu tu.


Siku za mwanzo za ukhalifa kuliundwa tume ya sheria (Ofisi ya Mufti) ilipotokea haja. tume hii iliitwa na kupitisha uamuzi. Tume ya sheria ya Khalifa ilifanya kazi kwa kutegemea vyanzo vya sheria vilivyotajwa katika masuala ya kawaida, maamuzi ya tume yalikidhi haja. Lakini yalipotokea masuala yasiyo ya kawaida na yenye umuhimu wa kitaifa ilikaa majlis ya Answar, Muhajirin, wawakilishi wa Aus na Khazraj na kupitisha maamuzi; kwa mfano baada ya kutekwa kwa Iraq na Syria wapo maswahaba waliotaka ardhi igawiwe kwa askari waliopigana. Majlis iliyojumuisha Ansar, Muhajirin na watu mashuhuri watano watano kutoka makabila ya Aus na Khazraj ilifanyika kuamua suala hili.


Baada ya mjadala mrefu Khalifa Umar alifanikiwa kuwaelewesha wajumbe wa majlis kwa kunukuu aya nyingi kuthibitisha kuwa katika ardhi hata vizazi vijavyo vina hisa kwa hiyo ardhi isigawiwe kwa askari waliopigana lakini waachiwe wenyewe waliotekwa na kodi itakayotokana na ardhi hii wagawiwe askari katika mfumo wa kiinua mgongo cha kila mwaka.


Hivyo ni dhahiri mkono wa Khalifa haukuwa juu ya sheria bali chini ya sheria ya Mwenyezi Mungu, kwa namna hii haikuwezekana kupendelea kundi au mtu yeyote au kuipinda sheria kwa kumpendelea kundi fulani. Hivyo kulikuwa na usawa kamili mbele ya sheria. Hali kadhalika katika masuala ya kodi kulikuwepo usawa na haki za kiraia. Hali hii ilipelekea mshikamano miongoni mwa waumini, uhuru wa maoni, haki katika jamii na kubwa kabisa ni kuwavumilia wafuasi wa dini nyingine.