Mitihani aliyopewa Nabii Ibrahimu kutoka kwa Allah


Tumeona katika historia yake kuwa Nabii Ibrahiim(a.s) alipata majaribu mengi katika harakati za kuhuisha Uislamu alipokuwa nchini mwake Iraq. Baba yake alimfukuza nyumbani na jamii nzima ikamtenga na kumuhukumu kuchomwa moto hadharani. Bila shaka alipata madhila ya aina hiyo hiyo alipokuwa amewalingania Uislamu washirikina wa nchi nyingine alimohamia. Kama hiyo haitoshi Allah(s.w) alimuongezea mingine miwili mizito.Mtihani wa kwanza, ni pale alipoamrishwa na Mola wake, kujitenga na mkewe Hajira na mtoto wake mchanga, Ismail, na kuwaacha peke yao jangwani karibu na Ka’abah. Nabii Ibrahiim(a.s) alitii amri hii ya Mola wake na kutegemea msaada wake kwa familia yake huku akiomba dua ifuatayo:
“Mola wetu! Hakika mimi nimewaweka (nimewakalisha baadhi kizazi changu (mwanangu Ismaili na mama yake, Hajrah) katika bonde (hili la Makka) lisilokuwa na mimea yoyote; katika nyumba yako takatifu (Al- Kaaba )Mola wetu! Wajaalie wasimamishe Sala. Na ujaalie nyoyo za watu zielekee kwao (wapende kuja kukaa hapa ili pawe mji) na uwaruzuku matunda ili wapate kushukuru.” “Mola wetu! Hakika wewe unajua tunayoyaficha na tunayoyadhihirisha. Na hakuna chochote kinachofichikana kwa Mwenyezi Mungu katika ardhi wala katika mbingu.” (14:37-38)Mtihani wa pili na mzito zaidi ni pale Nabii Ibrahiim(a.s) alipoamrishwa na Allah(s.w) kuwa amchinje Ismail, mtoto wake mmoja pekee, aliyekuwa anamtarajia, amsaidie katika harakati za kusimamisha Uislamu. Vile vile katika hili Nabii Ibrahiim hakusita, bali alitii amri ya Mola wake na kulitekeleza kwa moyo mkunjufu. Pia mtoto wake Ismail, alikuwa radhi kwa hili kwa ajili ya kutafuta radhi za Mola wao.“Basi (Ismail) alipofikia (makamu ya) kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: Ee Mwanangu! Hakika nimeona katika ndoto ya kwamba ninakuchinja. (Na ndoto za Mitume ni wahay). Basi fikiri, waonaje?” Akasema: Ee baba yangu! Fanya unavyoamrishwa utanikuta Insha-Allah miongoni mwa wanaosubiri.” (37:102)Basi wote wawili walipojisalimisha (kwa Mwenyezi Mungu), na akamlaza kifudifudi (amchinje). Pale pale tulimwita: “Ewe Ibrahimu:” “Umekwishasadikisha ndoto. (Usimchinje mwanao).” Kwa yakini hivi ndivyo tunavyowalipa watendao mema. (37:103-105)Bila shaka (jambo) hii ni jaribio lililo dhahiri, (mtihani ulio dhahiri). Basi tukamkomboa kwa mnyama wa kuchinjwa mtukufu. (37:106-107)