Ibrahiim(a.s) Aomba Kupata Kizazi Chema


Nabii Ibrahiim na mkewe Sarah walikaa mpaka wakawa wazee bila ya kupata mtoto. Ibrahim(a.s) alinyoosha mikono ya maombi kwa Mola wake, kuomba watoto wema watakao msaidia katika harakati zake za kusimamisha Uislamu katika jamii. Aliomba:
“Ee Mola wangu! Nipe (mtoto awe) miongoni mwa watenda mema.” Ndipo tukampa habari njema ya (kuwa atapata) mtoto mpole. (Basi akapata. Naye ndiye Nabii Ismaili). (37:100-101)Aliamua kuoa mke wa pili, Hajirah, aliyekuwa mjakazi wa mkewe Sarah. Dua yake ilipokelewa na Hajirah akajifungua mtoto Ismail (a.s) akiwa mtoto wa kwanza wa Ibrahim (a.s). Baadaye pia Allah(s.w) alimruzuku mtoto wa pili, Is-haqa, kutoka kwa Sarah, wote wawili wakiwa wazee vikongwe:

“Tena tukambashiria (kumzaa) Is-haqa. Nabii, miongoni mwa watu wema (kabisa)” (37:112)
(Mkewe Ibrahiim akastaajabu) akasema: Ee mimi We! Nitazaa na hali mimi ni mkongwe, na huyu mume wangu ni mzee sana? Hakika hili ni jambo la ajabu.” Wakasema (wale wajumbe- Malaika): Je! Unastaajabu amri ya Allah? Rehema ya Allah na Baraka zake ziko juu yenu, enyi watu wa nyumba hii! Hakika (Allah) ndiye anayestahiki kusifiwa na kutukuzwa.” (11:72-73).Nabii Ibrahiim(a.s) aliwalea watoto wake kiharakati na aliwausia kumcha-Allah na kuendeleza harakati mpaka mwisho wa maisha yao.
(Kumbukeni habari hii) Mola wake alipomwambia: “Nyenyekea;” akanena “Nimenyenyekea kwa Mola wa walimwengu (wote)”. Na Ibrahimu akawausia haya wanawe; na Yaakubu (pia akawausia wanawe): “Enyi wanangu! Hakika Mwenyezi Mungu amekuchagulieni Dini hii; basi msife ila nanyi mmekuwa wanyenyekevu.” (2:131-132)