Nabii Ibrahiim(a.s) Afanywa Kiongozi wa Harakati za Uislamu Ulimwenguni


“Na (kumbukeni habari hii) Mola wake alipomfanyia mtihani (Nabii) Ibrahiim kwa amri nyingi; naye akazitimiza. Akamwambia: ‘Hakika mimi nitakufanya kiongozi wa watu (wote) (Ibrahim akasema): ‘Je, na katika kizazi changu pia?” Akasema: “(Ndio lakini) ahadi yangu haitawafikia madhalimu.” (2:124)Katika aya hii tunajifunza kuwa NabiiIbrahiim(a.s) alipewa uongozi na kuwa mfano wa kuigwa na walimwengu wote baada ya kufaulu mitihani mingi na mizito iliyomthibitisha kwa ulimwengu kuwa alikuwa mnyenyekevu na mtii kamili kwa Allah(s.w).“Hakika Ibrahiim alikuwa Imamu (mfano mzuri wa wema wa kuigwa), mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, mtii kamili, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.” (16:120)Kutokana na dua yake, Mitume wote waliomfuatia wametokana na kizazi chake. Kupitia kwa Is-haqa(a.s) kuna Mitume wote wa bani Israil, kuanzia kwa Israil (Yaquub(a.s)) mwenyewe hadi kwa Nabii Issa(a.s) na kupitia kwa Ismail(a.s) tunaye Mtume Muhammad(s.a.w), ambaye ni Mtume wa mwisho na Mtume wa walimwengu wote kama alivyokuwa babu yake, Ibrahiim(a.s).Katika Qur-an tunahimizwa kufuata mila ya Nabii Ibrahiim:
Na nani atajitenga na mila ya Ibrahimu (akaichukia Dini hii ya Kiislamu) isipokuwa anayeitia nafsi yake katika upumbavu? Na kwa yakini sisi tulimchagua (Ibrahimu) katika dunia; na kwa hakika yeye katika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema (kabisa). (Kumbukeni habari hii) Mola wake alipomwambia: “Nyenyekea:” Akanena “Nimenyenyekea kwa Mola wa walimwengu (wote)”. (2:130-131)Na nani aliye bora kwa Dini kuliko yule ambaye ameuelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye ni mwema, na anafuata mila ya Ibrahimu (kuwa Muislamu kweli kweli). Na Mwenyezi Mungu amemfanya Ibrahimu kuwa ni kipenzi chake. (4:125)Mila yaIbrahiim(a.s) inayosisitizwa hapa si nyingine ila ni kuwa “Mnyenyekevu na mtii kamili” kwa Allah(s.w), kiasi cha mtu kuwa tayari na kwa moyo mkunjufu kumchinja mwanawe aliye mwema na anayempenda na kumtarajia sana. Pia kufuata mila ya Ibrahim ni kuwa tayari kufanya juhudi za kusimamisha Uislamu katika jamii na kutokomeza ushirikina bila ya kujali lolote litakalotokea hata kama ikibidi kugombana na kutengana na jamii nzima.Hakika nyinyi muna mfano mzuri (wa kuiga) kwa Ibrahimu na wale waliokuwa pamoja naye, walipowambia jamaa zao (makafiri). “kwa yakini sisi tu mbali nanyi, na mbali na hayo mnayoyaabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu; tunakukataaeni, umekwisha dhihiri uadui na bughudha ya daima baina yetu na nyinyi mpaka mtakapomuamini Mwenyezi Mungu peke yake....…” (60:4)

Ili kujikurubisha na mila ya Ibrahimu, Allah(s.w) ametuamrisha na kutufundisha kupitia kwa Mtume(s.a.w) kuwa tumuombee (tumswalie) Mtume na kujiombea sisi wenyewe kwa kusema:“Ee Allah! Mrehemu Muhammad na wafuasi wa Muhammad kama ulivyomrehemu Ibrahim na wafuasi wa Ibrahim. Hakika wewe u mtukufu na msifiwa wa haki. Ee Allah! Mbariki Muhammad na wafuasi wa Muhammad kama ulivyombariki Ibrahim na wafuasi wa Ibrahiim. Hakika wewe u mtukufu na msifiwa wa Haki”.