image

HISTORIA YA MTUME DAUD(A.S).

Nabii Daudi(a.

HISTORIA YA MTUME DAUD(A.S).

HISTORIA YA MTUME DAUD(A.S).


Nabii Daudi(a.s) aliishi Bait-Ul-Lahm karibu na mji wa Jerusalem zaidi ya miaka 200 baada ya Mtume Musa(a.s). Nasaba yake inatokea kwa Mtume Ya‘aquub(a.s). Pamoja na kuwa Mtume wa Allah(s.w), Daudi alikuwa pia mfalme wa Mayahudi (Bani Israil).



Kupewa Daudi(a.s)Utume na Ufalme


Kiasi cha miaka mia mbili hivi baada ya Mtume Musa (a.s), Mayahudi walipigwa sana na kuonewa na Wafalastin. Waliteka Sanduku takatifu la Waisrail ambamo ndani yake walihifadhi mbao ambazo zimeandikwa amri kumi alizoteremshiwa Nabii Musa (a.s). Aidha yalikuwamo ndani yake masazo mengine ya vitu vitukufu alivyoacha Nabii Musa na Nabii Harun. Sanduku hili Mayahudi walilitukuza sana kiasi kwamba hata wakienda vitani huenda nalo na likiwa mbele ya macho yao huamini kabisa kuwa watashinda vita. Kwa hiyo kunyang'anywa sanduku lao hilo na Wafalastin kuliwavunja nguvu kabisa (Mayahudi).



Ilikuwa ni katika kipindi hicho cha kuzidiwa nguvu na Wafalastin, Mayahudi walitamani wapate mfalme atakaye watawala na awaongoze kaitka vita. Biblia inataja kuwa Mtume wao katika kipindi hicho alikuwa Samuel. Kwa hiyo walimwomba Samuel awateulie mfalme.



Qur'an inataja kuwa Twaluti alichaguliwa kuwa mfalme. Lakini Mayahudi walimkataa. Hata hivyo Twaluti alibakia kuwa kiongozi wao na akawaongoza Mayahudi waliomtii hata wakamshinda adui yao. Qur'an inarejea habari hii katika aya zifuatazo:




"Hukusikia habari ya wakubwa wa Kibanii Israil baada ya Musa walipomwambia Nabii wao: "Tuwekee mfalme ili tupigane katika njia ya Mwenyezi Mungu". Yeye (Mtume wao) akasema:

"Haielekei ya kuwa hamtapigana ikiwa mtaandikiwa kupigana?" Wakasema: "Itakuwaje tusipigane katika njia ya Mwenyezi Mungu na hali tumetolewa katika majumba yetu na watoto wetu?" Lakini walipoandikiwa kupigana waligeuka, isipokuwa wachache miongoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anawajua sana madhalimu". (2:246).



Na huyo Mtume wao akawaambia: "Mwenyezi Mungu amekuchagulieni Twaluti kuwa mfalme". Wakasema: "Vipi atakuwa na ufalme juu yetu; na hali sisi tumestahiki zaidi kupata ufalme kuliko yeye; naye hakupewa wasaa wa mali?" Akasema: "Mwenyezi Mungu amemchagua juu yenu na amemzidishia wasaa wa ilmu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa (na) Mwenye kujua". (2:247).


"Na Nabii wao akawaambia: "Alama ya ufalme wake ni kukujieni lile sanduku ambalo mna ndani yake kituliza nyoyo zenu, kitokacho kwa Mola wenu, na mna masazo ya yale waliyoyaacha watu wa Musa na watu wa Harun, walilichukua malaika. Bila shaka katika hayo mna dalili kwenu ikiwa nyinyi mnaamini" (2:248).



Katika jamii za jahiliyah nasaba ya mtu na uwezo wake wa kiuchumi ilikuwa ni vigezo muhimu katika kuteua kiongozi. Mayahudi kwa kuyatupa mafundisho ya Mitume wao na kwa ukaidi wao walivitilia mkazo vigezo hivi vile vile. Kwa hiyo alipoteuliwa Twaluti kuwa kiongozi wao, wakaona hafai kwa kuleta hoja ya mali. Hata hivyo, hoja hiyo inavunjwa na elimu na siha nzuri. Uislamu unasisitiza umuhimu wa kuiboresha akili kwa elimu na kiwiliwili kwa siha nzuri. Katika Uislamu mtu hapewi uongozi kwa sababu ya nasaba au uwezo wake wa kiuchumi bali kwa elimu na Ucha- Mungu wake.



Twaluti baada ya kupewa uongozi aliyaongoza majeshi ya Mayahudi kupambana na Jaluti na majeshi yake. Kundi kubwa katika Mayahudi liliasi. Lakini wachache waliobaki wenye imani thabiti walifanya subira na kwa kumtegemea Allah(s.w) wakamshinda Jaluti. Nabii Daud(a.s) katika mapambano haya alikuwa katika jeshi la Twaluti na ndiye aliyemuua Jaluti. Baada ya ushindi huo Mayahudi walimchagua Nabii Daudi kuwa mfalme wao. Ni katika kipindi hicho hicho cha historia Daudi alipewa Utume kama inavyobainika katika aya zifuatazo:



Basi Taluti alipoondoka na majeshi alisema: "Mwenyezi Mungu atakufanyieni mtihani kwa mto. Basi atakayekunywa humo si pamoja nami, na asiyekunywa atakuwa pamoja nami; ila



atakayeteka kwa kiasi cha kujaza kitanga cha mkono wake (akanywa hayo tu, huyo hana makosa)". Lakini walikunywa humo isipokuwa wachache tu miongoni mwao. Basi alipovuka yeye na wale walioamini pamoja naye, walisema: "Leo hatumwezi Jaluti na majeshi yake". Wakasema wale wenye yakini ya kukutana na Mola wao: "Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wafanyao subira" (2:249).



Na walipotoka kupambana na Jaluti na majeshi yake, walisema hao watu wa Twaluti: "Mola wetu! Tumiminie subira na uithibitishe miguu yetu, na utusaidie juu ya watu hawa makafiri" (2:250).




Basi (hao watu wa Twaluti) wakawaendesha mbio (hao maadui zao) kwa idhini ya Mwenyezi Mungu; na Daudi akamwua Jaluti, na Mwenyezi Mungu akampa (huyu Daudi) ufalme na hikima (Utume). Na akamfundisha aliyoyapenda" (2:251).



Yapo mambo kadhaa muhimu ya kuzingatia kutokana na mafundisho ya aya hizi. Kwanza, ni suala la utii. Kuwa na uongozi madhubuti na utii wa wale wanaoongozwa kwa kiongozi wao ni jambo kubwa sana katika kutengemaa kwa mambo ya watu. Kama hakuna utii kwa uongozi, basi jamii ni yenye kuharibikiwa tu. Twaluti anaondoka na jeshi kubwa kupambana na adui wa kutisha. Twaluti hana hakika na utii wa jeshi lake. Basi Allah(s.w) akamwelekeza awafanyie mtihani wa kutokunywa maji hadi kukata kiu. Wasiotii asiwachukue kwenda nao huko kwenye uwanja wa vita wasije wakakhalifu amri vitani.

Ni dhahiri kuwa kama mtu hawezi kufanya subira na kuvumilia kiu yake kwa muda mdogo tu; basi hawezi kuhimili kishindo cha kutoa roho kwa ajili ya Allah kwenye medani ya vita.



Pili, fundisho lingine kubwa linalopatikana ni kuwa katika kuipigania Dini ya Allah(s.w) wingi sio hoja, bali imani thabiti, subira na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Watu wachache wa Twaluti walihisi isingekuwa rahisi kulishinda jeshi kubwa la Jaluti. Lakini wale wenye yakini hasa ya kukutana na Mola wao hawakusita. Bali walimkabili Mola wao kumwomba awamiminie subira na ujasiri wa kupambana na adui. Basi kwa idhini ya Mola wao walishinda vita.



Ni ahadi yake Allah(s.w) kwamba wakipatikana waumini wakweli wenye kusubiri, basi watawashinda maadui zao pamoja na wingi wao:


"Ewe Mtume (wa Mwenyezi Mungu)! Wahimizewalioamini wende vitani. Wakipatikana kwenu watu ishirini wanaosubiri watashinda mia mbili (katika hao makafiri. Basi nyinyi mkiwa ishirini lazima msimame mupigane na watu miteni). Na kama wakiwa watu mia moja kwenu watawashinda elfu moja ya wale waliokufuru, maana hao ni watu wasiofahamu (uhai wa Akhera, basi wanaogopa kupigana kwa ushujaa sana wasije wakafa. Basi watu mia katika nyinyi wasiwakimbie watu elfu katika wao)." (8:65).



Pamoja na ukweli huu, waumini wanatakiwa wafanye juhudi kubwa kukusanya nguvu zao na kusoma mbinu mbali mbali.


Basi waandalieni(wawekeeni tayari)nguvu mziwezazo (silaha) na mafarasi yaliyofungwa(kufuga)tayari tayari(mipakani),ili kwazo nguvu hizi muogopeshe maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zenu,(mnawajua) na pia (maadui zenu)wengineo wasiokuwa wao, msiowajua nyinyi(lakini) Mwenyezi Mungu anawajua. Na chochote mtakachokitoa katika njia ya Mwenyezi Mungu(kama hii misaada ya vita vya Jihadi)mtarudishiwa (kamili) sawasawa wala hamtadhulumiwa." (8:60).



Hata hivyo, silaha kubwa zaidi ni kuziunganisha nyoyo za waumini chini ya lengo moja tu la kuihami Dini ya Allah(s.w). Maadui wa Dini ya Mwenyezi Mungu pamoja na wingi wao wanashindwa kuikabili nguvu ya waumini, kwa sababu nyoyo na malengo yao ni mbali mbali.



"Hakika nyinyi (Waislamu) mnaogopwa zaidi katika nyoyo zao kuliko wanavyomuogopa Mwenyezi Mungu, maana wao ni watu wasiofahamu (lolote"). "Hawatapigana nanyi kwa mkusanyiko isipokuwa katika vijiji vyoa vilivyohifadhiwa, au nyuma ya kuta. Vita vyao baina yao vikubwa. Utawadhani kuwa wako pamoja, kumbe nyoyo zao ni mbali mbali. Hayo ni kwa sababu wao ni watu wasio na akili" (59:13-14).

Kwa hiyo suala zima la kuwaelemisha Waislamu na kisha kuwaunganisha chini ya lengo moja tu la kuisimamisha na kuilinda Dini ya Allah, ni jambo la msingi sana.



Tatu, jambo lingine la msingi ambalo tunapaswa tulizingatie, ni mazingira yaliyopelekea Nabii Daudi (a.s) kupewa ufalme na utume. Qur'an inatufahamisha kuwa Daudi alipewa Ufalme na Utume baada ya kumwua Jaluti. Hii inatudhihirishia kuwa heshima na jaza njema haipatikani ila kwa juhudi ya mtu binafsi katika kutekeleza majukumu. Hapana heshima pasi na kuwajibika. Aidha katika malipo ya kesho Akhera yatategemea pia juhudi ya mtu na kuwajibika kwake mbele ya Allah(s.w).



                   





           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Rajabu Tarehe 2024-05-10 14:53:23 Download PDF     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 1274


Sponsored links
👉1 Kitabu cha Afya     👉2 kitabu cha Simulizi     👉3 Kitau cha Fiqh     👉4 Madrasa kiganjani    

Post zifazofanana:-

HISTORIA YA KUZALIWA KWA MTUME MUHAMMAD (S.A.W) NA MAMA AMINA MKE WA ABDALLAH MTOTO WA ABDUL-AL MUTALIB
KUZALIWA KWA MTUME (S. Soma Zaidi...

Mbinu na njia walizotumia maadui wa uislamu dhidi ya waislamu na dola ya kiislamu madinah
Dola ya uislamu madinah (EDK form 3: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...

Vita vya Al Fijar na sababu zake
Historia na shida ya Mtume Muhammad S.A.W, sehemu ya 12. Hapa utajifunza kuhusu kutokea kwa vita vya al fijar. Soma Zaidi...

Kulingania Uislamu kwa Jamii Nzima
Baada ya miaka mitatu ya Utume, Muhammad(s. Soma Zaidi...

Shukurani za Nabii Ibrahiim(a.s) kwa Allah(s.w)
Kwa neema hii ya kuruzukiwa watoto wawili - Ismail na Is- haqa(a. Soma Zaidi...

Mbinu walizotumia makafiri wa kiqureish katika kuupinga uislamu makkah
Bara arabu zama za jahiliyyah (EDK form 2 dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...

Kuingia Kwa Uislamu Tanzania na Afrika Mashariki
Soma Zaidi...

Waliomuamini Nabii Nuhu(a.s)
Waliomuamini Nuhu(a. Soma Zaidi...

tarekh 01
NASABA YA MTUME (S. Soma Zaidi...

Mawazo Tofauti Kuhusiana na Uchaguzi wa Abubakar
Soma Zaidi...

Khalifa na Utungaji Sheria, na utiifu juu ya sheria na usimamiaji wa haki
Soma Zaidi...

Darsa za Sira historia ya Mtume (s.a.w) Jaribio la 04
Soma Zaidi...