image

NAMNA MTUME(S.A.W) ALIVYOSIMAMISHA DOLA YA KIISLAMU MADINAH

Safari ya Mtume(s.

NAMNA MTUME(S.A.W) ALIVYOSIMAMISHA DOLA YA KIISLAMU MADINAH

MTUME(S.A.W) KUSIMAMISHA DOLA YA KIISLAMU MADINAH


Safari ya Mtume(s.a.w) na sahibu wake, Abubakar na wale walioandamana nao, ilichukua siku 7 na waliwasili Quba siku ya Jumatatu mwezi 18 Rabi al-awwal sawa na 20 Septemba, 622 A.D. Quba ni kimji kilichopo maili tatu au kilomita 4.8 kusini mwa mji wa Yathrib (Madinah). Waislamu wote wa Yathrib, wakubwa kwa wadogo, wake kwa waume, walimiminika kwenda kumpokea Mtume(s.a.w) kwa shangwe na furaha kubwa. Mtume(s.a.w) alijipumzisha Quba kwa muda wa siku nne katika nyumba ya Bwana Kulthum bin Hadm, mkubwa wa Banu Amr katika kabila la Aus. Bwana huyu hakuwa amesilimu, bali alisilimu katika siku hizo alizokaa na Mtume wa Allah.



Baadaye Waislamu walipendekeza kuwa tarehe ya Kiislamu ianzie pale Waislamu walipoanza kuhamia Madinah, mpaka sasa hivi tunahesabu tarehe ya Kiislamu kuanzia kipindi hicho na tunatofautisha na miaka ya Kikristo kwa kuongeza A.H. (Al-Hijra) mbele ya mwaka wa Kiislamu.


Kujengwa Msikiti wa Quba

Katika siku ya pili ya kukaa kwake Quba, Mtume(s.a.w) aliamuru kujengwe msikiti katika uwanja uliotolewa na mwenyeji wake, bwana Kulthum bin Hadm. Mtume mwenyewe alishiriki katika kujenga msikiti huu wa kwanza. Aliwaachia Waislamu wa pale kuumalizia alipoondoka kuelekea mjini Yathrib. Msikiti huu umetajwa katika Qur'an kwa heshima kubwa kama ifuatavyo:




"..Msikiti uliojengwa juu ya msingi wa Ucha-Mungu tangu siku ya kwanza (ya kufika Mtume Madinah) unastahiki zaidi wewe usimame humo. Humo wamo watu wanaopenda kujitakasa. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wajitakasao." (9:108)



Kila mara Mtume(s.a.w) alikuwa akiuzuru msikiti huu kama tunavyofahamishwa katika Hadhith:

"Ibn 'Umar ameeleza kuwa Mtume wa Allah alikuwa akiuzuru msikiti wa Quba kwa miguu au akiwa juu ya mnyama, kila Jumamosi na alikuwa akiswali huko rakaa mbili." (Bukhari na Muslimu).

Ujenzi wa msikiti kuwa ndilo jambo la kwanza alilolifanya Mtume(s.a.w) mara tu ya kuingia Madinah, inatupa picha juu ya umuhimu na nafasi ya msikiti katika Uislamu.



Yathrib Inakuwa Al-Madinah al-Munawwarah


Siku ya Ijumaa, mwezi 22 Rabi 'al-awwal sawa na 24 Septemba, 622 A.D, Mtume(s.a.w) aliondoka Quba kuelekea Yathrib. Swala ya Ijumaa ilimkuta njiani katika sehemu ya Banu Salim, ambapo alishuka na kuswali swala hiyo pamoja na Waislamu wote waliokuwa panoja naye. Hii ilikuwa ndio swala ya kwanza ya Ijumaa. Mtume(s.a.w) na Waislamu hawakuwa wakiswali swala hii walipokuwa Makka. Khutuba yake ya Ijumaa hii ya kwanza ilizivuta na kuziteka sana nyoyo za wakazi wa Yathrib. Mtume(s.a.w) aliitoa hutuba yake kama ifuatavyo:



Kila sifa njema zinamstahikia Allah, ninamtakasa, nataka Msaada wake, Msamaha wake na Mwongozo wake.

Ninamuamini Yeye, wala simkufuru. Nashuhudia kuwa Muhammad ni mja wake na Mtume wake. Amemtuma na mwongozo, Imani ya kweli, mwanga na hekima na akamtuma kwa watu katika wakati ambapo Mitume wamekoma kuja na watu wamesahau mafundisho ya Mitume waliotangulia na hivyo wakawa ni wenye kupotea.



Kiyama kinakaribia na inakaribia siku ya malipo. Yeyote anayemtii Allah na Mtume wake hupata uongofu na anayekataa kuwatii, hupotea upotevu wa mbali. Nawausia kumcha Mwenyezi Mungu. Kwani ushauri mwema kuliko ushauri mwingine wowote ambao muislamu angeweza kumpa ndugu yake Muislamu ni kumuusia akumbuke maisha ya akhera na kumtaka amche- Mwenyezi Mungu. Hapana ukumbusho (mawaidha) ulio bora kuliko huu na hakuna kukumbuka kuliko bora kuliko huku. Hakika kumuogopa Allah kwa kutenda na kuchunga mipaka ya Allah, ni nyenzo ya kweli ya kukupelekea kupata maisha mazuri ya akhera. Yeyote yule anayetekeleza lile lililo kati yake na Allah, kwa siri au kwa dhahiri, kwa tegemeo tu la kupata radhi za Allah, atapata heshima katika muda mfupi ujao na atapata malipo makubwa huko akhera ambapo mwanaadamu atahitajia kupata kila amali njema aliyoichuma na atatamani kuwa mbali na amali nyingine yoyote ile.



Allah anawatanabahisha juu yake na Allah ni mpole kwa waja wake. Yeye ni yule ambaye maneno yake ni ya kweli na yule atekelezaye ahadi yake. Hapana mabadiliko katika ahadi yake na hakika amesema: "Neno langu halibadiliki na mimi si dhalimu kwa waja! Kwa hiyo muogope Allah katika mambo yako sasa na baadaye yakiwa ya siri au ya wazi. Kwani kwa yule amuogopaye Allah, Allah atamsamehe dhambi zake na kukuza malipo yake. Yeyote yule amuogopaye Allah atafuzu kufuzu kukubwa. Hakika kumcha-Allah (kumuogopa Allah) kutakuepusha na ghadhabu zake na kutakuweka mbali na adhabu yake na laana yake. Na hakika kumuogopa Allah kunaung'arisha uso, kunamridhisha Allah na kunapandisha daraja.




Kwa hiyo, kamata sehemu yako na usichupe mipaka katika dini ya Allah ambayo amekufundisheni kwa kuwaletea kitabu na amewaandalia njia (amekuongozeni katika njia) inayokufikisheni kwake, ili awatambue waumini wa kweli na wale wasioamini.



Kwa hiyo, fanya wema kama Allah alivyokufanyia wema. Kuwa katika uadui na maadui zake na pigana katika njia ya Allah kama inavyostahiki. Ni yeye aliyekuchagueni na kukuiteni Waislamu, ili wale wanaotaka kuangamia waangamie baada ya kuwafikia dalili zilizowazi. Hapana hila wala nguvu, ila itokanayo na Allah. Na ili wale wanaoishi baada ya kuwafikia dalili zilizo wazi wazi waishi. Hapana hila wala nguvu ila itoknayo na Allah.



Hivyo mkumbukeni Allah mara kwa mara kwa kadiri ya uwezo wenu na jiandaeni kwa maisha ya Akhera. Kwani anayetengeneza yake yaliyo baina yake na Allah(s.w), atamtosheleza kwa yale yaliyo kati yake na watu. Hii ni kwa sababu mamlaka ya Allah yako juu ya watu na wao hawana nguvu yoyote juu yake. Allah ni mkubwa, na hapana uwezo au nguvu, ila itokanayo na Allah, Aliye juu, Aliye Mkuu".18



Hutuba hii ya mwanzo katika kipindi cha Madinah imesisitiza Waislamu kumcha-Allah(s.w) na kupigania dini yake kwa matarajio ya kupata malipo mema ya huko akhera. Pamoja na maudhui ya hutuba hii pia tunapata funzo la tabia anayotakakiwa awe nayo mlinganiaji Uislamu. Kwa kipindi cha miaka 13 Mtume(s.a.w) aliteseka sana kutokana na vitimbi vya maquraish, ikiwa ni pamoja na kumtukana na kumkatisha tamaa, kumpiga, kumtenga na kula njama za kumuua. Mateso yote haya hayakumfika kwa kosa lolote lile zaidi ya kuwaita watu kwenye dini ya Allah(s.w). Kutokana na mateso aliyopata yeye na Waislamu waliokuwa pamoja naye, kibinaadamu baada ya kupata makazi ya salama, Mtume(s.a.w) angetegemewa aseme lolote juu ya maovu aliyofanyiwa katika hutuba yake hii ya kwanza. Lakini twaona katika hutuba hii Mtume(s.a.w) hakutoa neno lolote la ukali wala la shutuma dhidi ya makafiri wa Makka. Si hivyo tu, hakuzungumzia kabisa lolote lililomhusu yeye kama Muhammad (kama mtu binafsi). Muda wake wa hutuba aliutumia katika kuwahimiza watu wamuamini Allah na kumcha inavyostahiki, wapiganie dini ya Allah kwa kutarajia malipo ya akhera.



Jambo la kuzingatia hapa ni kuwa Muislamu katika kuufikisha ujumbe wa Allah kwa watu anatakiwa ajali zaidi kuona ujumbe unawafikia watu kuliko kujali hali yake binafsi. Kama kudhurika Muislamu binafsi kutakuwa ndio sababu ya kufanikisha kazi ya kuufikisha ujumbe wa Allah, basi hanabudi kujitoa muhanga kuikabili dhana hiyo.



Baada ya swala ya Ijumaa Mtume(s.a.w) aliendelea na safari yake. Kila ukoo ulimkaribisha Mtume akakae kwao, lakini aliwajibu kwa wema kuwa mahali atakaposhukia pameelekezwa na Allah(s.w) na ni pale atakaposimama ngamia wake. Mtume(s.a.w) alipokaribia kufika pale mahali palipokusudiwa, aliachia huru khatamu za ngamia wake ili aende mwenyewe mpaka alipoelekezwa na Mola wake. Ngamia wa Mtume alisimama mbele ya nyumba ya Abu Ayyub Ansari ambapo mbele yake palikuwa na kiwanja kikubwa kilichokuwa wazi. Kiwanja hicho kilikuwa cha yatima wawili, Sahl na Suhail. Mtume(s.a.w) aliamuru kiwanja hicho kununuliwe baada ya kukubaliana na wenyewe kwa ajili ya msikiti na makazi yake.



Abu Ayyub alifurahi sana kushukiwa na bahati hiyo ya kuchaguliwa na Allah(s.w) kukaa pamoja na Mtume wake. Alimpokea Mtume kwa furaha na alijitahidi kumtendea Mtume kila linalomfurahisha. Nyumba yake ilikuwa na ghorofa moja na akamuomba sana Mtume akae sehemu ya juu. Mtume(s.a.w) alimtaka radhi na kumwambia kwamba yeye mwenye nyumba ndiye mwenye kustahiki zaidi kukaa sehemu ya juu, pia alipendelea sehemu ya chini kwa ajili ya urahisi wa kuwapokea wageni wake tukizingatia kuwa nyumbani kwake sasa ndio ikulu ya muda. Mtume(s.a.w) alikaa kwa Abu Ayyub kwa kipindi cha miezi saba, baada ya ujenzi wa msikiti na nyumba za Mtume kukamilika. Alikaa kwa Abu Ayyub na familia yake ikiwa ni pamoja na mkewe, Bibi Sauda (aliyemuoa akiwa Makka baada ya kufariki Bibi Khadijah) na binti zake, Fatimah na Umm Kulthum.



Tokea siku ile Mtume(s.a.w) alipoanza kuishi mjini Yathrib mji huo ulipewa majina mapya. Kuanzia pale uliitwa Madinatun-Nabii (mji wa Mtume) na al-Madinah al-Munawarah (mji ung'arao). Hivi sasa inajulikana kwa ufupi kama mji wa β€œMadinah”.





                   





           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Rajabu Tarehe 2024-05-10 14:53:23 Topic: Sira Main: Post File: Download PDF     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 802


Sponsored links
πŸ‘‰1 Madrasa kiganjani     πŸ‘‰2 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)     πŸ‘‰3 Kitabu cha Afya     πŸ‘‰4 kitabu cha Simulizi     πŸ‘‰5 Simulizi za Hadithi Audio     πŸ‘‰6 Kitau cha Fiqh    

Post zifazofanana:-

HISTORIA YA NABII NUHU
Soma Zaidi...

Hatua na Mambo (Taasisi za Kisiasa) za msingi alizotumia Mtume (s.a.w) katika kuanzisha Dola ya Kiislamu Madinah
Kuanzishwa kwa Dola ya Kiislamu Madinah. Soma Zaidi...

Upinzani Dhidi ya Ujumbe wa Mtume(s.a.w)
Mtume(s. Soma Zaidi...

HISTORIA YA MTUME YUNUS(A.S)
Nabii Yunus(a. Soma Zaidi...

NI UPI MKATABA WA AL-FUDHUL NA ASILI YAKE, ATHARI ZAKE NA WALOHUSIKA
MKATABA WA AL-FUDHULBaada ya vita hivi viongozi wa pande mbili hizi waliamuwa wakae chini na wakubaliane kuweka kanun i na utaratibu utakaozuia kutotokea uonevu kama huuu tena. Soma Zaidi...

Mafunzo kutokana na vita vya badri
Dola ya uislamu madinah (EDK form 3: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...

Imam Malik Ibn Anas
Soma Zaidi...

Historia ya Luqman mtu aliyesifika kuwa na Hikma
Luqman ni katika watu wema kabisa waliopita zama za nyuma. Soma Zaidi...

HISTORIA YA MAISHA YA MTUME S.A.W KABLA YA UTUME
MAISHA YA MTUME (S. Soma Zaidi...

HISTORIA YA KUZALIWA KWA MTUME MUHAMMAD (S.A.W) NA MAMA AMINA MKE WA ABDALLAH MTOTO WA ABDUL-AL MUTALIB
KUZALIWA KWA MTUME (S. Soma Zaidi...

Mtume kumuoa bi khadija
Sara na historia ya Mtume Muhammad s.a.w, sehemu ya 15. Hapa utajifunza kuhusu chimbuko la ndoa ya Mtume s.a.w na bi Khadija. Soma Zaidi...

TAREKH, HISTORIA NA SIRA YA UISLAMU NA MTUME MUHAMMAD KUTOKA KUZALIWA MPAKA KUFARIKI NA HARAKATI ZAKE
1. Soma Zaidi...