Njama za Kumuua Mtume(s.
Njama za Kumuua Mtume(s.a.w)
Maquraish walikasirika sana walipogundua kuwa takriban Waislamu wote wameshahamia Yathrib na walihofia kuwa wakimwacha Muhammad naye akahamia Yathrib, atajiimarisha na Uislamu utakita mizizi. Hata hivyo, tetesi kuwa Mtume naye atahamia Yathrib zilishaenea miongoni mwa Maquraish, ikabidi wakutane waamue la kufanya kabla jambo hilo halijatokea. Abu Jahl, adui mkubwa wa Uislamu, aliitisha mkutano wa vijana 14 wa koo zote za Quraysh isipokuwa vijana wa Banu Hashim tu. Katika mkutano wao huo uliofanyika katika “Dar al-Nadwa”, yalitolewa mapendekezo yafuatayo dhidi ya Muhammad(s.a.w)
(1) Wamfunge Mtume peke yake katika chumba
(2) Wamzibe mcho na wamfunge mikono barabara kisha wampandishe juu ya ngamia aliyetiwa vitunga vya kuziba macho,aachwe ahangaike naye jangwani mpaka afe kwa kiu, njaa na jua kali.
(3) Mtu mmoja ampige panga ya shingo amuulie mbali
(4) Wachaguliwe vijana watukufu kutoka katika kila tumbo la Quraish kisha kila mmoja apewe upanga mkali; wakusanyike alfajiri moja makhsus wamuue wote kwa pamoja, ili lawama ziangukie koo zote za Quraish. Hapo Banu Hashim hatakuwa, na la kufanya ila kupokea diya tu.
Hizi ndizo njama za Maquraish dhidi ya maisha ya Mtume(s.a.w) ambazo pia zinabainishwa katika Qur-an:
“Na (kumbuka Ee Muhammad) walipokufanyia hila wale waliokufuru ili wakufunge au wakuue au wakutoe (Makkah kwa namna mbaya); na wakafanya hila (zao barabara). Na Mwenyezi Mungu akapindua hila hizo. Na Mwenyezi Mungu ni mbora wa kupindua hila (za watu wabaya)”. (8:30)
Walikubaliana na ile rai ya nne, wakachaguliwa vijana watukufu kutoka kila ukoo wa kabila la Quraish na wakaizunguka nyumba ya Mtume(s.a.w) usiku ili akitoka alfajiri wamvamie wote kwa pamoja.
Katika mchana ule ambao usiku wale vijana wa Kiquraish waliazimia kumuua Mtume(s.a.w), alikuja Jibril(a.s)akamueleza Mtume(s.a.w) njama za Maquraish dhidi yake na akampa amri ya kuhamia Yathrib katika usiku ule ule. Pale pale Mtume alimwendea Abubakar na kumfahamisha kuwa safari imeshawiva na atampitia usiku wa manane waende zao.
Mtume(s.a.w) na Abubakar walishaandaa safari kabla ya amri hii ya kuhama. Walishapanga njia watakayopita na pango watakamojificha katika siku za kutafutwa. Walipanga kukaa siku tatu pale pangoni, Abubakar alikwisha nunua ngamia wawili kwa ajili ya safari; alimchukua binti yake mkubwa, Asma, kwa siri mpaka kwenye pango la Thawr mahali watakapojificha ili awaletee chakula humo usiku usiku; aliamuru mchungaji wake wa mbuzi, Bwana Amr bin Fuhayra awe akiwaletea maji na maziwa kwenye hilo pango; aliamuru mwanawe mdogo, Abdallah, awaletee habari yoyote itakayowahusu watakapokuwa pangoni na alisha mkodi Bedui mmoja, Abdullah bin Uraiqit, kwa dinar 300, atakayewaongoza kwenda Yathrib kwa njia ya siri isiyotumiwa na yeyote.
Mtume baada ya kutoka kwa Abubakar, alimwita Aly bin Abu Talib, akamfahamisha habari ya safari yake na akamkabidhi amana zote za watu alizokuwa nazo ili azirudishe kwa wenyewe na akamtaka alale kitandani mwake. Pamoja na kujua kuwa Mtume(s.a.w) atazingirwa usiku ule ili auawe, ‘Ally alilala mle kitandani mwake badala yake bila ya wasiwasi wowote.
Wakati wa kuondoka ulipofika, Mtume(s.a.w) alitoka nje akawakuta maadui zake wamelala fofofo, akawanyunyizia mchanga vichwani mwao, huku akisoma Surat Yaasin, aya ya 1-9, kisha akaondoka zake salama salimini. Ieleweke hapa kuwa kilichomkinga Mtume(s.a.w) si Surat Yaasin kama wengi wanavyoitakidi bali anayemkinga mja na janga lolote lile ni Allah(s.w). Bila shaka Mtume(s.a.w) alisoma aya hizo ili kujikumbusha na kujiliwaza kutokana na ujumbe unaopatikana humo. Mtume(s.a.w) hakuwa na wasiwasi wowote kwa kuwa alikuwa na yakini juu ya ulinzi wa Allah(s.w).
Baada ya kutoka nyumbani kwake, Mtume(s.a.w) alimpitia Abubakar wakaanza safari yao mpaka kwenye pango la mlima Thaur lililopo maili mbili kusini mwa Makka.
Huko Makka, Maquraish walipoona njama yao haikufanikiwa walikasirika sana wakawa wanakwenda huku na kule katika harakati za kumtafuta Mtume(s.a.w). Kabla hawajaenda mbali walipita kwa Abubakar wakakuta naye hayupo. Wakaamua kumkodi Bedui mmoja Abu Kurz al-Khizai, aliyekuwa hodari sana wa kutafuta nyayo za mwenye kutafutwa. Wakafuata nyuma yake wakaikagua Makka yote. Hatimaye aliweza kuitambua njia waliyoifuata Mtume(s.a.w) na mwenzake, wakaanza kutafuta kwa hadhari kubwa hata wakapanda juu ya ule mlima wenye pango walimojificha Mtume(s.a.w) na Abubakar. Walipofika juu, yule Bedui mfuata nyayo, aliwaashiria kwenye lile pango lililokuwa kiasi cha futi 40 hivi kutoka pale walipo. Abubakar alipowaona wamewakaribia kiasi kile alipatwa na wasi wasi kuwa labda wataonekana. Mtume alimtuliza na kumwambia:
........Usihuzunike, kwa yakini Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi.....”. (9:40).
Vijana wa Kiquraish walipotaka kuliendea lile pango, Umayyah bin Khafaf, mmoja wa mabwana wakubwa wa kiquraish, alipiga kelele kwa ukali na hasira akasema,
“Hamna akili nyinyi kama huyu tuliyepoteza fedha zote kumkodi? Vipi mtu ataweza kupita katika pango lile pasina kuharibu utando wa mabubui wale waliotanda pale, au vipi njiwa wataweza kukaa pale na kulalia mayai yao ikiwa pana mtu ndani ya pango lile? Wallah! Mabuibui wamelitanda pango hili hata kabla ya kuzaliwa mwenyewe Muhammad! Hajui chochote mfuataji huyu”.
Ukweli ni kwamba buibui na njiwa wale hawajakuwepo zamani kama anavyodai Humayyah bali wote walikuja alfajiri ya siku ile ile ili wapate kuwaziba macho Maquraish wasimwone Mtume na mwenzake. Buibui na njiwa walikuwa miongoni mwa askari wa jeshi la Allah(s.a.w) katika kumnusuru Mtume na Dini yake kama anavyotukumbusha katika Qur-an:
“Kama hamtamnusuru (Mtume) basi Mwenyezi Mungu alimnusuru walipomtoa wale waliokufuru, alipokuwa (mmoja tu na mwenziwe) wa pili wake (peke yake); walipokuwa wote wawili katika pango; (Mtume) alipomwambia sahibu yake: ‘Usihuzunike, kwa yakini Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi. Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamnusuru kwa majeshi msiyoyaona, na akafanya neno la wale waliokufuru kuwa chini, na neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anayeshinda na ndiye mwenye hekima”. (9:40).
Maquraish walipokata tamaa kuwa hawataweza kumuona Mtume(s.a.w) katika viunga vya Makka walitangaza kuwa atakayemleta Muhammad akiwa hai au akiwa amekufa atapata zawadi ya ngamia 100.
Mtume(s.a.w) na Abubakar walibaki mle pangoni kwa muda wa siku tatu kisha waliendelea na safari yao ya Yathrib na mambo yakaenda kama walivyopanga. Katika msafara wa kwenda Yathrib Mtume(s.a.w) aliongozana na Abubakar, huru wa Abubakar, Bwana Amir bin Fuhayra, na yule Bedui aliyekodiwa kuwa mwongozaji wa msafara.
Huko Makka kila shujaa alikwenda huku na kule kumtafuta Muhammad ili aweze kujipatia ile zawadi nono ya ngamia 100. Shujaa mmoja Suraqah bin Malik alifanikiwa kuufuatia msafara wa Mtume(s.a.w), lakini kabla hajaukaribia farasi wake alijikwaa akaanguka. Alijaribu kumuinua na kuendelea kumfuatilia lakini farasi wake alianguka tena. Akamuinua tena na kukazana tena kuwakimbilia lakini farasi wake alijikwaa tena na safari hii miguu yake ilizama ardhini akazuiliwa, hawezi kuchopoka. Ilipofikia hali hiyo, Suraqah alipiga makelele ya kuomba amani na Mtume akampa.
Pale pale akachopoka akasimama pembezoni mwa Mtume na kuwaambia, “Mimi nina yakini kuwa jambo lako hili litaenea Bara Arab yote. Basi naomba unipe barua yako ambayo nikimuonyesha mtu yoyote atanipa amani na atanisaidia “. Mtume alimuamuru, Amir bin Fuhayra amuandikie barua hiyo ya amani. Suraqah alirejea Makkah na walipokutana na Abu Jahl alimpa habari juu ya yote yaliyomtokea na akamtaka Abu Jahl asilimu kama yeye alivyosilimu baada ya kuyakinisha kuwa kweli Muhammad ni Mtume wa kweli. Abu Jahl alimshangaa akamwambia; “masikini Roho yako! ndio kwanza sasa unajua kwamba Muhammad ni Mtume wa Haki?”
Mimi tangu zamani najua kuwa yeye ni Mtume wa Haki lakini sitaki kumfuata tu. Kwa nini kila utukufu wawe nao Banu Hashim peke yao? Banu Hashim wanatoa watukufu na sisi Banu Makhzum tunatoa: wanatoa mashujaa na sisi tunatoa. Hata leo farasi wao na wetu wanagusana magoti kwa kukaribiana, anatokea kwao Mtume aliyeletwa na Allah! wallah sitamfuata! Tutapata wapi Mtume wa kumlinganisha na wao? Kwa hiyo sitamuamini. Kwanini wakapewa cheo hiki Banu Hashim peke yao?
Mafunzo Yatokanayo na Hijra ya Mtume(s.a.w) na Maswahaba zake
Kutokana na Hijira ya Madinah ya Mtume(s.a.w) na maswahaba zake tunajifunza yafuatayo:
(i)Tunaona umuhimu wa kutunza na karejesha amana kwa wenyewe. Pamoja na mazingira yale ya hatari bado Mtume(s.a.w) alimbakisha Ally(r.a) ili arudishe amana za watu.
(ii)Ni muhimu kuweka mipango ya mambo tunayotaka kuyafanya kabla ya utekelezaji. Mtume(s.a.w) na Abubakar(r.a) wasingaliweka mpango wa safari yao mapema wangelikwama.
(iii)Hatunabudi kuchukua tahadhari katika kuendea harakati za kiislamu tukizingatia kuwa dini hii ina maadui wengi.
(iv)Baada ya kuchukua tahadhari kwa kadiri ya uwezo wetu, tujitegemeze (tutawakal) kwa Allah(s.w) kwani ahadi ya kuwanusuru wanaonusuru dini yake ni ya kweli.(Qur-an 47:7)
(v) Waislamu wanalazimika kufanya jitihada za makusudi za kuusimamisha Uislamu katika jamii ili waweze kumuabudu Allah(s.w) katika kila kipengele cha maisha yao ya kibinafsi na ya kijamii.
(vi)Kama Waislamu baada ya kujitahidi mwisho wa uwezo wao, watashindwa kupata mazingira yatakayowawezesha kuishi Kiislamu katika kila kipengele cha maisha, hawana budi kuhajiri kwenye eneo lingine katika ardhi ambapo wataweza kumuabudu Mola wao vilivyo.Vinginevyo hawatakuwa na udhuru mbele ya Allah(s.w) kama tunavyojitunza katka aya zifuatazo:
“Wale ambao Malaika wamewafisha, hali wamedhulumu nafsi zao, (kwa kutohajiri; Malaika) watawaambia: “Mlikuwa katika hali gani (katika jambo la dini yenu?” watasema: “Tulikuwa madhaifu katika ardhi hiyo (kwa hivyo hatukuweza kufanya ibada yetu Malaika watasema:”Ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa na wasaa na nyinyi kuhamia humo?” Basi hao makazi yao ni Jahanamu; nayo ni marejeo mabaya kabisa. Isipokuwa wale waliokuwa madhaifu kweli; katika wanaume na wanawake na watoto wasio na uweza wa hila yoyote wala hawawezi kuongoza njia (kwenda Madina) Basi hao huenda Mwenyezi Mungu akawasamehe; Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kughufiria. (4:97-99)
(vii) Kuhajiri sio ukimbizi bali ni kuhamia sehemu nyingine yenye mazingira yatakayo wezesha kusimamisha Uislamu pale na kupata nguvu ya kusimamisha Uislamu kule mlikotoka na sehemu nyingine ambapo uislamu hauja simama. Ikumbukwe kuwa Waislamu wa ummah huu wana dhima ya kusimamisha Uislamu kote ulimwenguni.
(viii)Hijra ya Madinah inatupa funzo la wazi kuwa Waislamu ni ndugu moja bila ya kujali ukabila, utaifa, rangi, n.k.
(ix) Uislamu hautasimama mpaka Waislamu wewe tayari kujitoa muhanga kwa mali zao na nafsi zao. Muhajirina waliacha makazi yao waliyoyazoea, majumba yao na kila chao wakaenda watupu kwenye makazi mapya ya ugenini. Answari nao waliwanusuru ndugu zao kwa mali zao na makazi yao.
(x) Muislamu ni haramu kabisa kuishi katika nchi ya kikafiri ila kwa sababu mbili tu; moja, iwapo yupo katika juhudi za kuondoa ukafiri na kuutawalisha Uislamu, pili, iwapo yumo katika matayarisho ya kufanya Hijra (kuhama).
Je! umeipenda hii post?
Ndio Hapana Save post
Rajabu Tarehe 2024-05-10 14:53:23 Topic: Sira Main: Post File: Download PDF Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 1396
Sponsored links
👉1 kitabu cha Simulizi
👉2 Madrasa kiganjani
👉3 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)
👉4 Kitau cha Fiqh
👉5 Kitabu cha Afya
👉6 Simulizi za Hadithi Audio
Msonge wa uongozi na siasa katika serikali ya kiislamu mafinah
Dola ya uislamu madinah (EDK form 3: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...
Kibri cha Ibilis na Uadui Wake Dhidi ya Binadamu
Ibilis ni katika jamii ya majini aliyekuwa pamoja na Malaika wakati amri ya kumsujudia Adam inatolewa. Soma Zaidi...
HISTORIA YA NABII LUT(A.S) NA WATU WA SODOMA NA GOMORA
Mtume Lut(a. Soma Zaidi...
Mafunzo yatokanayo na vita vya uhudi
Dola ya uislamu madinah (EDK form 3: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...
Uendeshaji wa dola ya uislamu madinah
Dola ya uislamu madinah (EDK form 3: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...
HISTORIA NA VISA VYA MITUME, MANABII NA WATU WEMA WALIOTAJWA KWENYE QURAN
Soma Zaidi...
HISTORIA YA NABII ISHAQA NA YAQUB
Soma Zaidi...
Mikataba ya aqabah
Bara arabu zama za jahiliyyah (EDK form 2 dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...
Mafunzo yatokanayo na kuanzishwa kwa dola ya uislamu madinah
Dola ya uislamu madinah (EDK form 3: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...
Nabii Ibrahiim(a.s) Kuulingania Uislamu kwa Jamii Yake
Nabii Ibrahim(a. Soma Zaidi...
Makubaliano ya Mkataba wa Al Fudhul
Sara na historia ya Mtume Muhammad s.a.w, sehemu ya 13. Hapa utajifunza historia ya Mkataba wa al fudhul na makubaliano yake. Soma Zaidi...
Ghasia na chokochoko za Makhawariji na kuuliwa kwa Ally
Soma Zaidi...