Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Nabii Isa(a.s)


Kutokana na Historia ya Nabii Isa(a.s) tunajifunza yafuatayo:

(i) Mtoto aliyezaliwa ndani ya ndoa ataitwa kwa ubini wa Baba yake na si vinginevyo na mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa ataitwa kwa ubini wa Mama yake.(ii) Waumini wanaharakati hawanabudi kumuomba Allah(s.w) awape watoto wema watakaofanya jitihada za makusudi za kuutawalisha Uislamu katika jamii.(iii) Tuwalee na kuwaelimisha watoto elimu ya mwongozo na mazingira (elimu juu ya fani mbali mbali) si kwa kutaraji maslahi ya dunia bali kwa ajili ya kusimamisha ukhalifa katika ardhi.(iv) Wanaharakati wanaposingiziwa au kupakaziwa maovu wasitengeneze majukwaa ya kujitetea na kujisafisha bali washitakie kwa Allah(s.w) na kumuomba awasafishe na kuwatakasa hapa hapa duniani.

- Allah(s.w) anawaasa waumini wasijali matusi na fitina za wanafiki na makafiri, bali waendelee kutenda inavyostahiki.Na sema (uwaambie): “Tendeni mambo (mazuri) Mwenyezi Mungu atayaona mambo yenu hayo na Mtume wake na Waislamu. Na mtarudishwa kwa Mjuzi wa siri na dhahiri; naye atakwambieni (yote) mliyokuwa mkiyatenda.” (9:105)(v) Msingi wa mafundisho ya Uislamu ni Tawhiid. Yaani tunatakiwa tuufundishe Uislamu kwa mujibu wa Qur-an na Sunnah na kwa lengo la kumuabudu Allah(s.w) katika kila kipengele cha maisha ya binafsi na jamii na kusimamisha Ukhalifa katika jamii – Hii ndio njia sahihi ya kufundisha Uislamu.(vi) Ukitafakari vizuri utagundua kuwa maumbile yote ya Allah (s.w)yaliyotuzunguka pamoja na nafsi zetu ni miujiza.
Hivyo kuletewa muujiza maalumu, haitakuwa ni sababu ya kumfanya mtu amuamini Allah(s.w) ipasavyo kama atashindwa kutafakari maumbile mbali mbali yaliyomzunguka.(vii) Kama mbinu ya kulingania Uislamu katika jamii hatunabudi kuunda kundi la harakati litakalokuwa tayari kuufundisha Uislamu kwa usahihi wake, kuamrisha mema na kukataza maovu – Qur’an (3:104).(viii) Nyakati zote wapinzani wakuu wa kusimama kwa Uislamu katika jamii ni washika dau (Al-Malaau) wa Dola za kitwaaghuut.(ix) Tunapoamua kujiingiza kwenye harakati za kuhuisha na kusimamamisha Uislamu katika jamii hatunabudi kujiegemeza (kutawakali) kwa Allah(s.w) na kuomba msaada wake na kutegemea ulinzi wake.(x) Mwanaharakati muda wote anatakiwa awe tayari kukabili au kukabiliwa na misukosuko au kufa kwa ajili ya Allah(s.w),Mtume wake na kusimamisha Dini yake.