(vii)Dai kuwa Muhammad (s.a.w) alitunga Qur-an ili kuleta Umoja na Ukombozi wa Waarabu:Wako baadhi ya watu wanaodai kuwa Muhammad(s.a.w) aliitunga Qur-an ili awaunganishe na kuwakomboa Waarabu. Dai hili pia halina nguvu kwa sababu zifuatazo:Kwanza, lau dai hilo lingekuwa la kweli basi hapana shaka kuwa Qur-an ingetia msisitizo mkubwa sana katika mada ya umoja na ukombozi wa Waarabu. Kwa hakika hakuna aya hata moja katika Qur-an nzima inayolingania umoja na ukombozi wa taifa la Kiarabu. Itayumkinikaje basi Muhammad (s.a.w) atunge Kitabu kwa lengo la kujenga utaifa wa Waarabu na kusiweko katika kitabu hicho hata aya moja juu ya suala hilo?Pili, msingi wa umma (taifa) unaofundishwa na Qur-an umejengwa juu ya itikadi ya haki na Qur-an inapinga hisia zote za utaifa kwa kufuata misingi ya rangi au kabila. Kila anayekubali itikadi ya Uislamu anakubalika katika umma wa Waislamu bila ya kujali rangi au kabila, au damu. Umoja uliodhihiri Arabia baada ya kushamiri kwa Uislamu ulikuwa umejengwa juu ya misingi ya Uislamu na siyo utaifa wa Kiarabu.Tatu, lau umoja wa Waarabu ungekuwa ndilo jambo lililomsukuma Muhammad (s.a.w) hapana shaka angekubali kuwa mfalme wa Waarabu ili atumie fursa hiyo kujenga umoja wa taifa la Waarabu. Lakini tunaona alikataa ufalme pale wakuu wa Kikuraysh walipotaka kumrubuni ili aache kuutangaza Uislamu.Nne, zipo aya katika Qur-an zinazolikanusha dai hilo. Aya mojawapo ya Qur-an yasema:


"Na (kumbuka) Malaika waliposema: Ewe Maryamu! Kwa hakika


Allah amekuchagua na kukutakasa na kukutukuza kuliko wanawake wa ulimwengu (wote)." (3:42)
Aya hii inamzungumzia Maryamu, mama yake Nabii Isa (a.s). Maryamu alikuwa ni Myahudi.Na Wayahudi walikuwa wanadharau Waarabu kuwa ni taifa duni. Muhammad (s.a.w) alikuwa ni Mwarabu na Qur-an imeshuka kwa lugha ya Kiarabu na watu wa mwanzo kusomewa hii Qur-an walikuwa Waarabu.Swali ni hili: Ikiwa Muhammad (s.a.w) alitaka kukuza hisia za utaifa wa Waarabu vipi basi aweke katika Qur-an aya hii inayomsifu mwanamke wa Kiyahudi kuwa amechaguliwa, ametakaswa na kutukuzwa na Allah(s.w) kuliko wanawake wote? Kwa nini asimsifie mama yake au mwanamke mwingine yeyote wa Kiarabu?
Aya nyingine ni hii ifuatayo:


Enyi kizazi cha Israili (Mayahudi)! Kumbukeni neema zangu nilizokuneemesheni, na nikakutukuzeni kuliko viumbe wengine. (2:47)
Mifano hii yaonesha kuwa haiingii akilini kuwa Muhammad (s.a.w) awe ametunga Qur-an kwa lengo la kuleta umoja na utukufu wa taifa la Waarabu halafu ndani ya hiyo hiyo Qur-an akasifia kwa sifa za kipeo cha juu kabisa watu walio maadui wa Waarabu!