(g) Kujiepusha na kufuata mambo kwa kibubusa


Waislamu wanakatazwa kufanya na kufuata mambo kwa kibubusa (kwa mkumbo) bila ya kuwa na ujuzi unaostahiki.
"Wala usifuate usiyo na ilimu (ujuzi) nayo. Hakika masikio na macho na moyo; hivyo vyote vitaulizwa." (17:36).Kila mtu wa kawaida hana budi kutumia kipaji chake cha akili (moyo) na milango ya fahamu (macho, masikio, n.k.) katika kuchukua uamuzi sahihi na kufuata utaratibu wa maisha anaoridhia Allah (s.w). Na hasa kazi ya akili na kipaji cha elimu alichotunukiwa binaadamu, ni kumuwezesha kujitambua, kumtambua Mola wake na kumuabudu inavyostahiki.Mtu atakayeishi kwa kufuata mambo kinyume na utaratibu anaoridhia Allah, ambao ni Uislamu, hatapaswa kumlaumu yeyote isipokuwa nafsi yake kwa matokeo mabaya yatakayomfika katika maisha ya dunia na akhera. Allah (s.w) anatutanabahisha juu ya hili katika aya zifuatazo:(Wakumbushe wakati) waliofuatwa watakapowakataa wale waliowafuata, na hali ya kuwa wamekwisha kuiona adhabu, na yatakatika mafungamano yao. Na watasema wale waliofuata, "Laiti tungeweza kurudi (duniani) tukawakataa kama wanavyotukataa. "Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu atakavyowaonyesha vitendo vyao kuwa majuto yao; wala hawatakuwa wenye kutoka Motoni." (2:166-167)


Na wakasema wale waliokufuru: "Hat utaiamini Qur-an hii kabisa, wala Vile (vitabu) vilivyokuwa kabla yake." Na ungewaona madhalimu watakaposimamishwa mbele ya Mola wao, wakirudishiana maneno wao kwa wao, (ungeona mambo)! Wale wanyonge watawaambia wale waliojiona wakubwa: "Kama si nyinyi bila shaka tungekuwa Waislamu." Waseme wale waliojiona wakubwa kuwaambia wale wanyonge: "Oh!Sisi tulikuzuilieni uwongofu baada ya kukufikieni? (Siyo) Bali nyinyi wenyewe mlikuwa waovu. " Na wale wanyonge waseme kuwambia wale waliojiona wakubwa: "Bali (mlikuwa mkifanya), vitimbi (hila) usiku na mchana (vya kutuzuilia tusiamini); mlipotuamuru tumkufuru Mwenyezi Mungu na tumfanyie washirika." Nao wataficha majuto watakapoiona adhabu; na Tutaweka makongwa shingoni mwa wale waliokufuru; kwani wanalipwa mengine ila yale waliyokuwa wakiyatenda?" (34:31-33)


"Na (wakumbushe) watakapobishana katika Moto huo - wakati madhaifu watakapowaambia wale waliojitukuza: "Kwa yakini sisi tulikuwa wafuasi wenu, basi je, mnaweza kutuondolea sehemu kidogo ya Moto?" Waseme wale waliokuwa wakijitukuza: "Sisi sote tumo humu; Mwenyezi Mungu amekwishahukumu baina ya viumbe; (na tumekwishastahiki Moto, hatuna la kufanya." Na wale waliomo Motoni watawaambia walinzi wa Jahanamu; "Muombeni Mola wenu atupunguzie (alau) siku moja ya adhabu." (Walinzi) wawaambie: "Je, hawakuwa wakikujieni Mitume wenu kwa hoja zilizowazi?" Waseme: "Kwa nini? (Wakitujia lakini tuliasi)" Wawaambie: "Basi ombeni; na madua ya makafiri hayawi ila ni ya kupotea bure." (40:47-50)