Masharti ya udhu
Ili udhu wa mtu ukamilike hapana budi kuchunga na kutekeleza masharti yafuatayo kabla ya kuanza kutawadha:
(i)Kuwa na “maji safi” ya kutosha kuweza kutitirika (yasiwe ya kupakaza tu) katika viungo vya udhu vinavyooshwa.
(ii)Kutokuwa na kitu kilichogandamana (kama vile lami, rangi, ulimbo, n.k) kitakachoweza kuzuia maji kufika kwenye ngozi ya viungo vya udhu. Ni lazima mtu aondoe hicho kilichogandamana ndio aanze kutawadha.
(iii)Kutokuwa na uchafu mwingineo au vumbi,la aina yoyote au kitu chochote juu ya viungo vya kutawadhia kitakachobadilisha rangi, harufu au tamu ya maji yatakayotiririka humo. Ni sharti mtu awe msafi kwanza ndipo aanze kutawadha.
(iv)Kuondoa najisi juu ya viungo vya udhu kabla ya kuanza kutawadha.
(v)Kukata kucha ndefu zinazozuia maji kufikia kona za vidole, kabla ya kuanza kutawadha.
Masharti haya haya ndiyo masharti ya kuoga katika kuondoa hadathi ya kati na kati na hadathi kubwa, bali pamoja na hayo,kwa wanawake wenye kusuka, hawana budi kufumua misuko yao isiyoruhusu maji kupenya.