Hadathi ya kati na kati (Janaba).
Mtu hupatwa na hadathi ya kati na kati kwa kupatwa na Janaba. Janaba ni hali inayompata mtu baada ya kufanya kitendo cha jimai (kitendo cha ndoa) au kutokwa na manii kwa kuota au kwa namna nyingineyo. Mtu mwenye janaba yuko katika hali chafu kulingana na sharia ya Allah (s.w) na ameharamishiwa kufanya ibada hizi:
(i)Kuswali (rejea Qur-an 4:43, 5:6)
(ii)Kutufu.
(iii)Kukaa Msikitini.
“Aysha (r.a) ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: Msielekeze milango ya nyumba hizi msikitini kwa sababu si halali msikiti kwa mwanamke mwenye hedhi au kwa mtu mwenye janaba ”. (Abu Daud)
(iv) Ku is oma Qur-an hata kwa moyo.
Ibn Umar ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: “Wenye hedhi na wenye janaba hawatasoma chochote kutoka kwenye Qur-an ” (Tirmidh)
Si vibaya kwa mtu mwenye janaba kula, kuongea au kugusana na watu. Pia kutokana na mafundisho ya Mtume (s.a.w) si lazima mtu kukoga mara tu baada ya kufanya kitendo cha jimai na mkewe, hasa ikiwa usiku bali anatakiwa aoshe sehemu za siri na atawadhe alale, kisha akiamka ndipo akoge kwa kujitwaharisha kwa ajili ya swala ya Alfajiri. Mafundisho haya tunayapata katika hadithi ifuatayo:
Aysha (r.a) ameeleza kuwa: Mtume (s.a.w) alipotaka kula au kulala akiwa na janaba, alikuwa kwanza akitawadha kama anavyotawadha kwa ajili ya swala. (Bukhari na Muslim).