image

Hstora ya Nabii Yunus

Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Yunus

HISTORIA YA MTUME YUNUS(A.S)


Nabii Yunus(a.s) ni miongoni mwa Mitume wa Allah(s.w) waliotajwa katika Qur-an. Yunus(a.s) ametajwa katika Qur-an kwa majina matatu:

(i) “Yunus” (37:139) Na hakika Yunus alikuwa miongoni mwa Mitume.


 

(ii) “Dhun-Nun”

Na (Mtaje) Dhun-Nun (Yunusi) alipoondoka hali amechukiwa, na akadhani ya kwamba hatutamdhikisha. Basi (alipozongwa) aliita katika giza (akasema): Hakuna aabudiwaye isipokuwa Wewe, Mtakatifu “Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu (nafsi zao).” (21:87)


 

(iii) “Sahibul-Hut” (Mmezwa na Chewa)

Basi subiri kwa hukumu ya Mola wako, wala usiwe kama mmezwa na Chewa (Yunusi). (Kumbuka) alipolingana, (alipomwita Mwenyezi Mungu), na hali ya kuwa amezongwa (barabara).(68:48)


 

Majina ya “Dhun-Nun” na “Sahibul-Hut” yana maana ya “Mwenye kumezwa na samaki (chewa).” Nabii Yunus (a.s) ameitwa majina hayo mawili kutokana na historia ya maisha yake ya Da’awah iliyompelekea mpaka akamezwa na samaki mkubwa (chewa) kisha akatapikwa ufukoni akiwa hai kwa uwezo wa Allah(s.w).

 

Yunus(a.s) Kulingania Uislamu kwa Watu Wake


Nabii Yunus(a.s) alitumwa kufikisha ujumbe wa Allah(s.w) kwa watu laki moja na zaidi wa mji wa Ninawah (Nineveth) katika nchi ya Assyria. Ninawah ni mji wa zamani sana ambao hauko katika ramani hivi sasa. Mji huo ulikuwa kandokando ya mto Tigris sehemu iliyo mkabala na mji wa kisasa, Mosul, kilometa 368 kaskazini ya kaskazini magharibi mwa mji wa Baghdad.


 

Nabii Yunus(a.s) aliwalingania Uislamu watu wa mji ule, lakini walimkanusha. Allah(s.w) alimuagiza Nabii Yunus awaonye watu wake juu ya adhabu itakayowafika baada ya muda maalumu uliowekwa endapo wataendelea kumuasi. Yunus(a.s) alipoona kuwa muda wa adhabu unakaribia na bado watu wake wameshikilia msimamo wao wa kukanusha ujumbe wake, alikata tamaa na kuamua kuondoka kwenye mji ule kuihami nafsi yake na adhabu ya Allah, bila ya kupewa ruhsa ya kuhama na Mola wake kama walivyopewa ruhusa Mitume wengine.


 

Watu wa mji ule walipoona adhabu inakaribia, walimuamini Nabii Yunus kuwa ni Mtume wa haki, wakamuamini Allah(s.w) na kumnyenyekea ipasavyo na kumuomba msamaha kwa maovu yao. Allah(s.w) kwa rehema yake aliwasamehe na kuwaondolea adhabu ile kama tunavyojifunza katika Qur-an:


 


Kwanini usiweko mji ulioamini (upesi kabla ya kuadhibiwa), ili imani yake iwafae? Isipokuwa watu wa Yunus (tu ndio walioamini mara walipohisi kuwa adhabu inakuja. Basi wakaokoka). Walipoamini tuliwaondolea adhabu ya hizya katika maisha ya dunia na tukawastarehesha kwa muda (tulioutaka). (10:98)


 

Nabii Yunus(a.s) hakujua yaliyopita nyuma yake. Alipoona adhabu haikushuka alichelea kuwa watu wa mji ule watazidi kumkanusha. Akakimbilia Pwani ambako alipata jahazi akaingia. Jahazi ilisheheni kiasi kwamba halikuweza kwenda. Ikapigwa kura ili itakaye muangukia atoswe baharini. Ikamuangukia Nabii Yunus(a.s) akatoswa baharini na kumezwa na chewa (samaki mkubwa)


 

Na hakika Yunusi alikuwa miongoni mwa Mitume. (Kumbukeni) alipokimbilia katika jahazi iliyosheheni.(37:139-140)


 


Na wakapiga kura. Basi akawa miongoni mwa walioshindwa (ikapasa atupwe baharini). Mara samaki alimmeza hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa. Basi isingelikuwa ya kwamba yeye alikuwa ni miongoni mwa waliokuwa wanamuabudu (Mwenyezi Mungu vilivyo). (37:141-143)

Bila shaka angalikaa tumboni mwake mpaka siku watakakayofufuliwa (viumbe). (37:144)

 

Nabii Yunus(a.s) Amuomba Allah(s.w) Msamaha


Ndani ya tumbo la samaki, Nabii Yunus(a.s) akiwa hai na akili timamu aligundua kosa lake la kuwakimbia watu wake bila ya ruhusa kutoka kwa Mola wake. Ilibidi Yunus (a.s) alalame ndani ya tumbo la samaki kumuomba msamaha Mola wake na kuomba msaada wake.


 

Na (Mtaje) Dhun-Nun (Yunusi) alipoondoka hali amechukiwa, na akadhani ya kwamba hatutatamdhikisha. Basi (alipozongwa)aliita katika giza (akasema):“Hakuna aabudiwaye isipokuwa Wewe Mtakatifu hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu (nafsi zao).” (21:87)


 

Allah(s.w) alimsamehe mja wake Yunus(a.s) na kumuokoa katika janga lile kwa kumuelekeza samaki amrudishe pwani na kumtapika.


 

“Basi tukampokelea (toba na dua yake) na tukamuokoa katika huzuni ile. Na namna hivyo ndivyo tuwaokoavyo walioamini.” (21:88)


 

Lakini tukamtupa ufukoni (kwa kutapikwa na huyo samaki) hali ya kuwa mgonjwa.” (37:145)


 

Baada ya kufikishwa pale pwani, Yunus (a.s) alikuwa mgonjwa na dhaifu asiyejiweza kwa lolote. Mola wake alizidi kumrehemu kwa kumuoteshea mti wa mbarikhi ambao aliula ukampa afya ya kumuwezesha kuwarudia watu wake ambao aliwakuta wameshaamini na wanamngojea kwa hamu ili awape mafunzo na maelekezo waweze kumuabudu Mola wao inavyostahiki:


 

Na tukamuoteshea mmea wa mbarikhi (akawa anakula). (37:146) “Na tulimpeleka kwa (watu) laki moja au zaidi, (wale wale watu wake). Basi wakaamini na tukawastarehesha mpaka muda wao wa kufa.” (37:147-148)

 

Mafunzo yatokanayo na Historia ya Nabii Yunus(a.s)

Kutokana na Historia ya Nabii Yunusi(a.s) tunajifunza yafuatayo:

(i) Allah(s.w) ni mwingi wa kusamehe na mwingi wa kurehemu, hivyo waumini wamuelekee Allah kumuomba msamaha hata kama wamefanya kosa kubwa kiasi gani.


 

(ii) Toba inayokubaliwa pamoja na sharti nyingine ni ile inayoletwa kabla ya muda wa hukumu ya adhabu ya Allah (s.w) au kabla ya kufikwa na mauti:

Hawana toba wale ambao hufanya maovu mpaka mauti yamemhudhuria mmoja wao, (hapo) akasema: “Hakika mimi sasa natubu.” Wala (hawana toba) wale ambao wanakufa katika hali ya ukafiri. Hao tumewaandalia adhabu iumizayo. (4:18)

 

(iii) Katika kazi ya Da’awah (kulingania Uislamu) tusiwakatie tamaa watu bali tuendelee nao kwa kubadilisha mbinu mpaka mwisho wa uhai wetu au mpaka Allah(s.w) apitishe hukumu yake. Tumuige Nabii Nuhu(a.s) kwa subira (alilingania kwa miaka 950) na tusirudie kosa la kukosa subira la Nabii Yunus(a.s).


 

(iv) Matendo mema na ucha-Mungu, huwa ni sababu ya dua na toba ya mja kuwa kabuli mbele ya Allah(s.w).

“Basi isingelikuwa ya kwamba yeye (Yunus) alikuwa miongoni mwa waliokuwa wanamuabudu (Allah(s.w) vilivyo) bila shaka angalikaa tumboni mwaka (huyo samaki) mpaka siku watakayofufuliwa (viumbe)”. (37:143-144)





           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Rajabu Tarehe 2024-06-27 16:36:34 Topic: visa vya Mitume Main: Masomo File: Download PDF     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 308


Sponsored links
👉1 kitabu cha Simulizi     👉2 Simulizi za Hadithi Audio     👉3 Kitabu cha Afya     👉4 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)     👉5 Madrasa kiganjani     👉6 Kitau cha Fiqh    

Post zifazofanana:-

Historia ya Nabii Musa
atika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Musa Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Hud katika Quran
Katika makala hii utakwenda kujifunzahistoria ya Mtume Hud katika Quran Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Ayyuub
Katika somo hiliutakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii ayyuub Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Yunus
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Yunus Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Ya'qub
Katika somo hili utawenda ujfunz ahstoraya Nabii Ya'qub na familia yake Soma Zaidi...

Hstora ya Nab Ishaqa katika quran
Katika post hii tutakwenda kujifunza historia ya Mtume Ishaqa Soma Zaidi...

Histora ya Nabi Zakariya
Katika somo hili utakwenda ujfunza kuhusu hslistoria ya Nabi Zakariya Soma Zaidi...

Hstora ya Nab Sulaman
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Sulaman Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Muhammad (s.a.w) wa ufup
Huu n ufupisho wa Historia ya Mtume Muhammad s.a.w. Tumekuandalia histori hii kwa urefu zaidi kwenye Makala zetu zinazofuata Soma Zaidi...

Hstoria ya Nabii Yusuf
Katika makala hii utakwenda ujfunzakuhusu historiaya Nabii Yufuf katika Quran Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Ismail katika quran
KKatika somohili utakwenda kujifunzahistoriaya Mtume Ismail Mtoto wa Nabii Ibrahim Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Ibrahimu
Katika post hii utakwenda kujifunza historia ya Mtume Ibrahim katika quran Soma Zaidi...