image

Hstoria ya Nabii Yusuf

Katika makala hii utakwenda ujfunzakuhusu historiaya Nabii Yufuf katika Quran

HISTORIA YA NABII YUSUFU(A.S.)

 

Mtume Yusufu(a.s) alikuwa mtoto wa Mtume Ya’aquub bin Is- haq bin Ibrahiim. Kwa hiyo Yusufu(a.s) ni kijukuu cha (mjukuu wa mtoto wa) Mtume Ibrahiim(a.s) na mjukuu wa Mtume Is-haqa(a.s.).

Mtume Ya’aquub(a.s) alikuwa na watoto 12. Nabii Yusufu(a.s) alichangia mama na mmoja wa hao. Wengine 10 walikuwa na mama zao.


Ndoto ya Nabii Yusufu(a.s) Maisha ya Nabii Yusufu(a.s) yanaanza kusimuliwa ndani ya Qur’an pale alipomwambia babake kuwa:


 

Yusufu alipomwambia baba yake “Ewe babaangu! hakika nimeona katika ndoto nyota kumi na moja na jua na mwezi. Nimeviona hivi vikinisujudia(12:4)


 

Mtume Ya‘aquub, kwa ilimu aliyopewa na Mola wake alifahamu tafsiri ya ndoto ile kwamba inabashiri kuwa Yusufu atakuja kuwa mtu mwenye hadhi kubwa na Mtume. Akamtahadharisha kuwa:


 

Akasema (baba yake): “Ewe mwanangu! Usiwasimulie ndoto yako (hii) nduguzo wasije wakakufanyia vitimbi (kwa ajili ya husuda). Hakika Shetani kwa mwanadamu ni adui aliye dhahiri.(12:5)


 


Namna hivi Mola wako atakuchagua na kukufundisha hakika ya mambo. Na atatimiza neema zake juu yako na juu ya kizazi cha Ya‘aquub, kama alivyoitimiza zamani juu ya baba zako Ibrahim na Is-haqa. Bila shaka Mola wako ni Mjuzi na Mwenye hikima: (12:6).

 

Njama za Kumuua Nabii Yusufu(a.s)

 

Kwa tabia zake njema Yusufu(a.s) alipendwa sana na baba yake. Ndugu zake Yusufu(a.s) wakajawa chuki na husuda wakijadiliana kuwa;

 

...............Hakika Yusufu na nduguye wanapendwa sana na baba kuliko sisi, hali sisi ni kundi lenye nguvu. Hakika baba yetu yumo katika upotofu ulio wazi.(12:8)


 

Wakapanga njama za kumhujumu Yusufu (a.s) kwa kumuua ili mapenzi ya baba yao yawageukie wao. Wakapanga na kuazimia kuwa:


 

Muueni Yusufu au mtupeni nchi za mbali ili uso wa baba yenu ukuelekeeni na baada ya haya mtakuwa watu wema. (12:9)


 

Hatimaye wakakubaliana kumtumbukiza kisimani badala kumwua,wazo hili lilitolewa na mmoja wao ambaye angalau aliogopa kubeba dhima ya kufanya dhambi kubwa ya kuiua nafsi pasina haki. Akasema;


 

Msimuue Yusufu lakini mtupeni Yusufu katika(jiwe la ndani) ya kisima kirefu, watamuokota baadhi ya wasafiri, kama ninyi mnataka kufanya kitu.(12:10)


 

Yusufu anatumbukizwa kisimani

Kutumbukizwa Yusufu(a.s) Kisimani Pamoja na kuwa na dhamira ile mbaya ya kutaka kufanya kosa la kuua mtu asiyekuwa na hatia , wakaongeza kosa lingine la kusema uwongo. Wakasema:


........Ewe baba yetu, mbona hutuamini juu ya Yusufu, hakika sisi ni wenye kumtakia mema. Mruhusu kesho pamoja nasi atakula kwa furaha na kucheza; hakika sisi tutamlinda (12:11-12)


 

Ingawa mzee Ya’aquub(a.s) alionesha wasiwasi,lakini hatimaye aliwaruhusu waandamane naye. Walimtumbukiza Yusufu(a.s) kisimani kama walivyo dhamiria na wakaichukua kanzu yake na kuipakaza damu za uwongo, kisha wakamuongopea baba yao:


 

Ewe baba yetu! Hakika sisi tulikwenda kushindana mbio na tukamuacha Yusufu penye vyombo vyetu, basi mbwa mwitu akamla; lakini hutatuamini ingawa tunasema kweli (12:17)

Ya‘aquub(a.s.) alikuwa na mategemeo makubwa ya kupata mrithi bora atakayeendeleza kazi yake. Hata hivyo hatumwoni mzee Ya’aquub akikata tamaa kwa kufadhaika au kukufuru. Yeye akawajibu;

......


 

“..............Nafsi zenu zimekushawishini jambo. Basi (langu mimi ni) subira njema; na Mwenyezi Mungu ndiye aombwaye msaada kwa haya mnayoyasema” (12:18).

Hii ndio tabia ya Muislamu. Kurejea na kumtegemea zaidi Allah(s.w) afikwapo na msiba.

 

Yusufu Aokotwa na Kuuzwa nchini Misri


Huko nyuma wapita njia walikisogelea kisima kwa lengo la kuteka maji. Mmoja wao katika harakati za kuteka maji,alimuibua mtoto akaruka kwa mshangao:..........Akasema: Ee,furaha njema! Huyu hapa kijana mwanaume.............. (12:19) Walimchukua hadi Misri na kumuuza kwa Al-Aziz au Waziri,


 

Wakamuuza kwa thamani chache ya pesa za kuhesabika, na hawakuwa na haja naye (12:20)

Yusufu(a.s) Apewa Utume na Kukumbana na Mtihani Alipofikia umri wa utu uzima alipewa hukumu na elimu. Yaani akapewa Utume. Qur’an inasema:-

“Na (Yusuf) alipobaleghe, tulimpa hukumu na ilimu. Na namna hivi tunawalipa wanaotenda mema” (12:22).


 

Katika kipindi hiki cha utu uzima mke wa Waziri alifanya vitimbi na hata kumshika Yusufu kwa nguvu ili azini naye. Lakini Yusufu alikataa kufanya tendo hilo ovu. Alipoambiwa ‘njoo’, Yusufu akasema:


 

Najikinga kwa Mwenyezi Mungu. Hakika yeye (mumeo) ni bwana wangu, ametengeneza makazi yangu hapa vizuri. Hakika madhalimu hawatengenekewi(12:23)


 

Al-Aziz, aliyemnunua Yusufu(a.s) alimwangalia vizuri kama mtoto wake wa kulea. Lakini kwa bahati mbaya,Yusufu(a.s)alipofikia baleghe mkeweAl-Aziz alimtamani na kutaka wazini naye. Yusufu(a.s)alimkatalia kwa hoja kuwa kufanya hivyo ni kumwasi Allah(s.w) na pia itakuwa ni kumfanyia khiyana Al-Aziz, ambaye amemkirimu makazi mazuri pale Misri (Rejea Qur’an 12:23).


 

Mkewe Al-Aziz hakutaka kusikiliza hoja za Yusfu(a.s),bali alimkazania kuwa lazima akubali kufanya kitendo hicho na akafunga mlango.

“Na (mwanamke huyo) akamkazia nia(ya kutaka kumdhuru vile alivyomkataa) na (Yusufu) akamkazia nia (ya kumpiga; akitaka kumpiga). kama (Yusufu)asingaliona dalili za (kufahamishwa na) Mola wake (kuwa kumpiga huyo mwanamke si uzuri, angelimpiga bali alikimbia tu).Tumefanya namna hivi ili Tumwepushie kila jambo la ubaya na la uovu(kama huko kuzini). Hakika yeye alikuwa katika waja wetu waliosafishwa.(12:24)


 

Yusufu(a.s) kwa kukwepa shari ile ilibidi akimbilie mlangoni na yule mwanamke akawa anamkimbiza na kuchana kanzu yake kwa nyuma. Kufika mlangoni wakakutana na Al-Aziz na kesi ikaanzia hapo:


 

Na (wote wawili) wakakimbilia mlangoni na mwanamke huyo akairarua kanzu yake kwa nyuma. Na wakamkuta mume wake mlangoni; mwanamke akasema (kumwambia mumewe katika kutia chonza za uwongo): “Hakuna malipo ya mwenye kutaka kufanya ubaya na mkeo isipokuwa kufungwa gerezani au kupewa adhabu inayoumiza”(Anamsingizia uwongo Nabii Yusufu kuwa anamtaka). (12:25)


 


(Yusufu) akasema: “Huyu (mwanamke) ndiye aliyenitaka bila mimi kumtaka.” Na shahidi aliyekuwa katika jamaa za huyu(mwanamke) akatoa ushahidi(akasema): “Ikiwa kanzu yake imechanwa mbele basi (mwanamke huyu amesema kweli, naye (Yusufu) yu katika waongo. “Na kama kanzu yake imechanwa nyuma, basi (mwanamke huyu) amesema uwongo, naye (Yusufu) yu katika wakweli(12:26-27)


 

“Basi (mumewe)alipoona kanzu yake imechanwa kwa nyuma (alijua kuwa Yusufu ndiye aliyekuwa akitaka kukamatwa kwa nguvu) akasema: “Hakika hii ni katika hila zenu wanawake; bila shaka hila zenu ni kubwa. (Wewe ndiye uliyeazimia mabaya, unakwenda kumsingizia yeye!) “Yusufu! Yaachilie mbali haya (usiyasimulie nje). Na wewe (mwanamke) omba msamaha kwa dhambi zako . Hakika wewe ni katika wanaofanya makosa. (12:28 - 29)


 

Mkewe Al-Aziz badala ya kujuta kwa kosa lake lile na kuleta toba, alishabikia kwa kuwaalika wanawake wengine wa mji waliomlaumu kwa kitendo chake kile kiovu cha kutaka kumbaka mtumishi wake. Aliwaalika ili na wao washuhudie uzuri wa Yusufu na kuwahakikishia kuwa yeye hataacha kumtamani Yusufu (a.s)


 


Na wanawake wa mji ule (wakapata habari hii) wakawa wanasema:”Mkewe waziri anamtamani mtumishi wake pasi na kutamaniwa naye. Hakika amemuathiri kwa mapenzi, Bila shaka sisi tunamuona (mke wa waziri) yumo katika upotofu ulio dhahiri. (12:30)


 


Basi (mkewe waziri) aliposikia msemo wao huu aliwaita (waje waone uzuri wa Yusufu wajue kuwa mwenye kurukwa na akili kwa kumpenda Yusufu hana lawama) na akawafanyia karamu na akampa kila mmoja katika wao kisu na akamwambia (Yusufu), “Tokeza mbele yao . “Basi walipomuona waliona ni kitu kikubwa kabisa na wakakata mikono yao(kwa vile visu na wenyewe hawana habari kwa kuwa wameshughulika kumtanzama tu huyo Yusufu) hakuwa huyu ila ni malaika mtukufu. (Mkewe waziri) akasema Huyu ndiye mliyenilaumia; na hakika nilimtamani kinyume cha nafsi yake, lakini akajilinda. Na kama hatafanya ninalomuamrisha, bila shaka (nitamfanyia kila vitimbi mpaka) atafungwa gerezani na atakuwa miongoni mwa madhalili (badala ya hii hishima miongoni mwa madhalili (badala ya hii hishima anayoipata. Kisha wakaingia na wale wanawake nao kuwapeleka wajumbe kumtaka)”(12:31 - 32)


 

Lengo la mke wa Al-Aziz lilitimia kwa kuwaonesha wanawake wa mji kuwa haipaswi kulaumiwa kwa kumtamani Yusufu.

Ikumbukwe kuwa huyu alikuwa ni mke wa mtu mkubwa. Hivyo hata wanawake walioitwa walikuwa ni wake wa wakubwa au wenye hadhi katika jamii. Wanawake hawa kudhihirisha matamanio yao, bila ya aibu, ni kielelezo cha kuanguka kwa maadili katika jamii hiyo. Yaonesha ufuska ulikuwa umechanua sana kiasi kwamba aibu haikuwa ni kitu chenye nafasi tena katika maumbile yao.

 

Yusufu(a.s) Atupwa Gerezani


Mkewe Al-Aziz hakumkatia tamaa Yusufu(a.s). Uovu wake ulimchochea kuzidi kumuandama Yusufu(a.s). Alimpa Yusufu chaguzi mbili: Ama akubali kuzini naye au amfanyie hila atiwe gerezani.

................Na kama hatafanya ninalomuarisha, hakika atafungwa gerezani na atakuwa miongoni mwa madhalili(12:32)

Kwa kumukhofu Allah(s.w) na kuchukia tendo chafu la zinaa, Yusufu akasema Ee Mola wangu! Nastahabu zaidi gereza kuliko haya wanayoniitia........(12:33)

 

Maisha ya Yusufu(a.s.) Gerezani

 

Yusufu(a.s) alijikuta yupo gerezani, si kama mhalifu bali aliyeonewa kwa uadilifu na uaminifu wake. Lakini pia hakusononeneka kwa dhulma ile aliyofanyiwa kwani kuwepo gerezani kulimtenga na watu waovu waliotaka kumtia kwenye uchafu.


 

Uadilifu na sifa zake njema zilikuwa zimezagaa kila mahali. Hata alipoingia gerezani wafungwa wenzake walimpa heshima ya pekee. Walikiri kwamba Yusufu(a.s) ni miongoni mwa watu wazuri.


 

Yusufu Afikisha Ujumbe wa Uislamu kwa Wafungwa

 

Ilitokea kule gerezani wafungwa wenzake wakaota ndoto na kumtaka Yusufu(a.s) awape tafsiri yake.

Na wakaingia pamoja naye gerezani vijana wawili. Mmoja wao akasema: Hakika nimeona (katika ndoto) nakamua ulevi”; na mwingine akasema: Hakika nimeona(katika) ndoto nabeba mikate juu ya kichwa changu ambayo ndege wanaila. Tuambie tafsiri yake; kwa yakini sisi tunakuona wewe ni miongoni mwa watu wazuri(12:36)


 

Yusufu(a.s) aliwakubalia ombi lao lakini kabla ya kuwatafsiria ndoto zao aliwalingania kwa Allah(s.w) kwakuwauliza:

“Enyi wafungwa wenzangu wawili! Je, waungu wengi wanaofarikiana ndio bora (kuabudiwa) au Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu (juu ya kila kitu?)” (12:39).


 


Hamuabudu badala yake (Mwenyezi Mungu) ila majina (matupu) mliyopanga nyinyi wenyewe na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuteremsha dalili kwa hayo. Haikuwa hukumu ila hii ya Mwenyezi Mungu tu; ameamrisha msimuabudu yoyote isipokuwa Yeye tu. Hiyo ndiyo Dini iliyonyooka lakini watu wengi hawajui.” (12:40).

Baada ya kuwafikishia ujumbe huu muhimu, Nabii Yusufu (a.s) akaanza kuwaeleza taawili ya ndoto zao kuwa:


 


Enyi wafungwa wenzangu wawili! Mmoja katika ninyi atarejeshwa kazini kwake akamnyweshe bwana wake ulevi. na yule mwingine atauawa kwa kusulubiwa, na ndege watamla kichwa chake. Limekwishakatwa (huko kwa Firaun) hili jambo mlilokuwa mkiuliza (12:41)


 

Kisha Yusufu(a.s) akamuomba yule atakayetolewa gerezani:

“...........Unikumbuke mbele ya bwana wako;(umwambie kuwa nimeonewa nimefungwa bure); Lakini shetani alimsahaulisha kumkumbusha bwana wake. kwa hivyo akakaa gerezani (Nabii Yusufu) baadhi ya miaka (baada ya hapa)(12:42)

 

Kufunguliwa Yusufu(a.s) Kutoka Gerezani


Yusufu(a.s) alisahauliwa gerezani kwa muda mrefu. Kilichopelekea akumbukwe ni ndoto aliyoota Mfalme. Alipoamka aliwaita makuhani na kuwahadithia:

.............Hakika mimi nimeona ng’ombe Saba wanene wanaliwa na ng’ombe Saba ving’onda. Na nimeona mashuke Saba mabichi na mengine yaliyokauka. Enyi wakubwa nitafsirieni ndoto yangu ikiwa ninyi mnaweza kutafsiri ndoto(12:43)

Wakasema: ni ndoto iliyovurugika wala sisi hatujui tafsiri ya ndoto hizi(12:44)

Yule mfungwa aliyefasiriwa ndoto na Yusufu(a.s) kuwa atatolewa gerezani alimkumbuka Yusufu na akawaambia:

........Mimi nitakwambieni tafsiri yake. basi nitumeni (12:45)


 

Alipofika gerezani, akamwita:

Yusufu! Ewe mkweli! Tueleze hakika ya ng’ombe Saba wanene kuliwa na ng’ombe Saba dhaifu. Na mashuke Sabaa mabichi na mashuke makavu, ili nirejee kwa watu wapate kujua. (12:46)

Akasema: Mtalima miaka Saba mfululizo kwa juhudi. Na mtakavyovivuna viacheni katika mashuke yake isipokuwa kidogo mnavyokula.(12:47)

Kisha itakuja baadaye miaka Saba ya shida itakayokula vile mlivyolima, isipokuwa kidogo mtakachohifadhi (12:48)

Walipopata taawili ya ndoto hii, Mfalme kwa furaha kubwa kabisa alisema

 

Mleteni kwangu nimchague awe mtu wangu mwenyewe. Basi alipozungumza naye (Mfalme) alisema, Hakika wewe leo kwetu umekwishakuwa ni mwenye hishima na muaminiwa.(12:54)


 

Yusufu alimuagiza mjumbe wa mfalme kuwa kabla hajotoka gerezani lijulikane lile shauri la wanawake waliomtaka kwa nguvu na kumchochea aingie katika maasi - Qur’an (12:50). Yusufu(a.s) alitaka hilo lifanyike ili apate kusafika kwa Al-Aziz na kwa jamii nzima kuwa hakumfanyia dhuluma ile aliyosingiziwa.

 

Mfalme aliwakusanya wanawake na kuwauliza

“...............Nini jambo lenu lilikuwa mlipomtamani Yusufu kinyume cha matamanio yake? wakasema ‘Hasha lillahi! Sisi hatukujua ubaya wowote kwake. Mkewe Al-Aziz naye akasema: Sasa haki imedhihirika, mimi ndiye niliyemtamani kinyume cha nafsi yake, na bila shaka yeye yu miongoni mwa wa kweli (kabisa)” (12:51)


 

Baada ya hapo ndipo Yusufu(a.s) alipokubali heshima ile aliyopewa na kupendekeza awe msimamizi wa hazina ya nchi.

Akasema nifanye niwe mtazamaji wa hazina ya nchi; hakika mimi ni mlinzi mzuri na mjuzi hodari (12:55)


 

Tendo hili la Yusufu(a.s) kudai kesi yake na wanawake iangaliwe na Mfalme na haki itolewe, lilinyanyua sana hadhi yake. Kwanza aliifasiri ndoto ngumu ya Mfalme ambayo iliwashinda wachawi, wanganga na watabiri wote wa kutegemewa katika nchi. Pili alipotakiwa na Mfalme atoke gerezani, alikataa mpaka kesi ifikishwe mahakamani, mkosaji abainishwe. Matokeo ya kesi yakawa wanawake kukiri mbele ya hadhara ya Mfalme kuwa Yusufu(a.s) hakuwa na hatia bali wao ndio waliokuwa waovu.


 

Ilidhihiri kwa kila mtu kuwa hakuna yeyote miongoni mwao, ila amezidiwa na Yusufu(a.s) kwa uadilifu na tabia njema kwa ujumla. Haiwi ni kitu cha ajabu basi tunapoona Yusufu anapewa dhamana ya kuangalia hazina yote ya nchi. Huu ni wadhifa unaohitajia mtu aliyepea kwa uadilifu na hakuwepo aliyemzidi Yusufu(a.s).

 

Yusufu(a.s.) Akutana na Ndugu Zake


Njaa ilitokea na ikawa hapana sehemu nyingine yoyote yenye chakula ila Misri.Watu wakamiminika Misri kuhemea chakula. Miongoni mwao wakawa ni wale ndugu zake Yusufu(a.s).


 

Wakaja ndugu zake Yusufu, na wakaingia kwake akawajua(12:58)

Wakapewa chakula na wakarejeshewa bidhaa zao walizoleta kubadilisha na chakula. Kisha Yusufu (a.s.) akawaagiza:
 

Na alipowapatia chakula chao alisema. (mkinijia mara ya pili) Nijieni na ndugu yenu wa kwa baba. Je hamuoni ya kwamba mimi ninatimiza kipimo, na ni mbora wa wakaribishao. (12:59)

Basi waliporejea kwa baba yao, walisema: “Ewe baba yetu! Tutazuiliwa (chakula mara ya pili mpaka twende na ndugu yetu); basi mpeleke ndugu yetu pamoja nasi ili tupate kupimiwa; na yakini sisi tutamlinda.” (12:63).


 

Mzee Ya‘aquub(a.s), akasema:-Sitampeleka pamoja nanyi mpaka munipe ahadi kwa jina la Allah kwamba lazima mtamrejesha kwangu, isipokuwa nyote mzungukwe (na hatari au kufa). Basi walipompa ahadi yao alisema: Mwenyezi Mungu ndiye mlinzi juu ya haya tuyasemayo (12:66)


 

Baada ya kuchukua ahadi hii, Mzee Ya‘aquub aliwaambia wanawe kuwa wasiingie Misr kwa kutumia mlango mmoja,bali kila mmoja apitie mlango wake katika milango inayoingia humo(rejea Qur’an 12:67).


 

Kwa kuingia milango tofauti, Yusufu(a.s) alipata fursa ya kukutana na ndugu yake,Bin-Amin (wa kwa baba na mama) kabla ya wale wengine na kujitaambulisha kwake kisha kumfahamisha dhamira yake ya kumbakisha Misr-(rejea Qur’an 12:69)


 

Yusufu(a.s) alifanya hila ya kumbambikizia wizi ndugu yake kwa kuweka pishi ya kupimia ndani ya mzingo wake. Mara tu ya kuchukua mizigo yao na kuaga, palinadiwa kupotea kwa kipimo cha mfalme. Wote ndugu zake Yusufu(a.s) walikataa kuwa hawakuhusika na wizi wa chombo kile. Ikabidi ipitishwe sachi(search) na kikakutwa kwenye mzigo wa Bin Amin ambaye alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja Misr. (rejea Qur’an 12:70-75).


 

Ndugu zake Yusufu(a.s) waliporejea nyumbani walimfahamisha mzee wao mkasa uliowapata. Mzee Ya‘aquub(a.s) alizidi kupata majonzi kwa kupotelewa na watoto wawili, lakini baadae alikuwa na matumaini ya kuwapata wote, ndipo akawaagiza wanawe:


 

Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yusufu na nduguye, wala msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hawakati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu isipokuwa watu makafiri (12:87)


 

Walipofika Misri walimtaka Yusufu(a.s) awafanyie ihsan kwa kuwapa chakula bure kwa vile hawakuwa na fedha ya kulipa huku wakimkumbusha kuwa Mwenyezi Mungu huwalip a watu wanaowatendea wema mwenzao. Hapo Y usufu(a.s) akawakumbusha:


 

Akasema: Je! Mnajua mliyomfanyia Yusufu na nduguye mlipokuwa ujingani?(12:89)

Wakasema: Je! Wewe ndiye Yusufu? Akasema: Mimi ndiye Yusufu, na huyu ni ndugu yangu. Mwenyezi Mungu ametufanyia hisani. Hakika anayemcha Mungu na kusubiri , basi Mwenyezi Mungu hapotezi malipo ya wafanyao mema(12:90)


 

Nduguze wakakiri makosa yao waliyomfanyia Yusufu(a.s) na kumuomba awasamehe. Wakasema: Wallahi! Mwenyezi Mungu amekuchagua juu yetu, na hakika sisi tulikuwa wenye makosa. (12:91)

 

Ndoto ya Nabii Yusufu(a.s) Yatimia

 

Yusufu(a.s.) aliwasamehe na kuwaagiza waende wakamlete baba yao mzee Yaaqub(a.s.) na wao waje wote na familia zao.


 


Akasema: “Hakuna lawama juu yenu leo; Mwenyezi Mungu atakusameheni, naye ni Mwenye rehema zaidi kuliko wanaorehemu. (12:92)


 

Nendeni na kanzu yangu hii na muiweke mbele ya uso wa baba yangu: naye atafunuka macho aone. Na nijieni pamoja na watu wenu wote(12:93)

Waliporudi nyumbani walichukuzana wote, familia nzima akiwemo baba yao, mzee Ya’aquub(a.s),wakahamia Misri.

Na walipoingia kwa Yusufu aliwakumbatia wazazi wake na akasema; “Ingieni Misri, Inshaa-Allah mumo katika amani. (12:99)


 

Aliwainua wazazi wake na kuwaweka katika kiti cha Ufalme. Na wote wakaporomoka kumsujudia. Na Yusufu akasema: “Ewe babangu! Hii ndiyo hakika ya ndoto yangu ya zamani. Hakika Mola wangu ameithibitisha. Na amenifanyia hisani akanitoa gerezani na akakuleteni ninyi kutoka jangwani; baada ya Shetani kuchochea baina yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu ni mwenye kulifikia alitakalo. Bila shaka Yeye ni Mjuzi na Mwenye hekima.(12:100)


 

Shukurani za Nabii Yusufu(a.s) kwa Allah(s.w)

 

Yusufu(a.s)alimshukuru Mola wake kwa kuleta dua ifuaatayo:

“Ee Mola wangu! Hakika umenipa Ufalme na umenifundisha tafsiri ya mambo. Ewe Muumba wa mbingu na ardhi! Wewe ndiye Mlinzi wangu katika dunia na Akhera. Nifishe hali ya kuwa ni Muislamu na unichanganyishe na watendao mema (12:101)

 

Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Nabii Yusufu(a.s)


 

“Kwa yakini katika (kisa cha) Yusufu na ndugu zake yako mazingatio mengi kwa wanaouliza (mambo wapate kujua)”. (12:7).

Baadhi ya mazingatio kutokana na kisa hiki ni haya yafuatayo:


 

(i) Mitume huzaliwa Mitume na maisha yao yote kuanzia utotoni ni kiigizo cha tabia njema kwa waumini


 

(ii) Wazazi hatunabudi kuwafunza watoto wetu tabia njema na kuwalea hivyo mpaka utuuzima wao.


 

(iii) Watoto wenye tabia njema tuwapende na tuwashajiishe kubakia na mwenendo huo.


 

(iv) Si vema kutangaza neema tulizo nazo kwa watu hata wale wa karibu yetu ili kujikinga na husuda.


 

(v) Uislamu ni neema kubwa, hivyo kila atakayejaaliwa kufuata Uislamu vilivyo na kufanya jitihada za kuusimamisha katika jamii,ajiandae kuhusudiwa na makafiri na wanafiki.


 

(vi) Hila za watu wenye roho mbaya na husuda dhidi ya watu wema wenye kujitahidi kusimamisha Uislamu katika jamii mwisho wake huwafedhehesha wenyewe hapa hapa duniani kama walivyofedheheka ndugu zake Yusufu na mkewe Al-aziz.


 

(vii) Kutenda mema, ukweli na subira humnyanyua mtu daraja hapa duniani na huko akhera.


 

(viii) Ukweli ukidhihiri uwongo hujitenga kama tulivyoona kwa nduguze Yusufu na mkewe Al-Aziz.


 

(ix) Muungwana katika watu ni yule anayekiri makosa yake na kuomba msamaha kama walivyofanya nduguze Yusufu(a.s).


 

(x) Waumini wanatakiwa wamuige Yusufu(a.s) kwa kuwa wepesi wa kusamehe na kulipa wema badala ya kulipiza kisasi baada ya kufanyiwa ubaya na kisha kuombwa msamaha. Pamoja na Yusufu kuwasamehe ndugu zake, aliwapatia chakula wakati wa njaa na kuwakaribisha Misr katika makazi ya Kifalme.


 

(xi) Ngao dhidi ya mahasidi, mafatani, n.k. ni kumcha – Mungu, subira,kujitegemeza kwa Allah(s.w) na kuomba kinga yake.


 

(xii) Hatunabudi kutumia fursa zinazojitokeza katika kulingania Uislamu, kama Yusufu(a.s) alivyoitumia fursa ile alipokutana na wale wafungwa wawili.


 

(xiii)Matwaaghuuti daima hawawezi kuhukumu kwa uadilifu na kutoa haki sawa hasa pale kesi itakapokuwa ni baina ya mdau wa nchi na raia wa kawaida. Ilidhihirika kwa ushahidi wa wazi kuwa Yusufu(a.s) ndiye aliyekosewa na yule mkewe Al-Aziz, lakini kwa kumlinda na kashfa ile ilibidi Yusufu(a.s) ahukumiwe kwenda gerezani.


 

(xiv)Waumini wanapobambikiziwa maovu na machafu kutokana na husuda na chuki ya makafiri na wanafiki, wasitengeneze majukwaa ya kujitetea bali waendelee kufanya wema kama Allah(s.w)anavyoagiza:


 


Na sema(uwaambie): “Tendeni mambo (mazuri). Mwenyezi Mungu atayaona mambo yenu hayo na Mtume Wake na Waislamu. Na mtarudishwa kwa Mjuzi wa siri na dhahiri; naye atakwambieni (yote) mliyokuwa mkiyatenda.” (9:105)

 

(xv)Tunapokubalika na kuhitajika kuongoza jamii hatunabudi kupendekeza tukabidhiwe kuongoza katika maeneo tunayoyamudu vizuri kitaaluma, kiuzoefu na kiuadilifu na hasa pale tutakapoona hapana watu wengine wa kuongoza kwa uadilifu katika maeneo hayo.


 

(xvi)Tuchague viongozi waadilifu na wenye tabia njema bila ya kujali ukabila, utaifa, n.k. Yusufu(a.s) alikuwa mtu wa kuja na mtumwa lakini alipewa Uongozi Misr kutokana na elimu yake, tabia yake njema na uadilifu wake.


 

(xvii)Kiongozi Muumini ni yule anayekumbuka na kuzingatia kuwa wadhifa alionao ni amana aliyokabidhiwa na Allah (s.w) kwa manufaa ya jamii, hivyo hujiepusha na kibri,

majivuno, kujikweza au tabia yoyote inayoashiria dharau kwa wenzake. Funzo hili tunalipata kwenye dua ya Nabii Yusufu(a.s).

           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Rajabu Tarehe 2024-06-27 12:29:30 Download PDF     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 80


Sponsored links
👉1 Kitabu cha Afya     👉2 Kitau cha Fiqh     👉3 Madrasa kiganjani     👉4 kitabu cha Simulizi    

Post zifazofanana:-

Historia ya Nabii Idrisa
Katika somohili utakwenda kujifunza historia ya Nabii Idrisa (amani iwe juu yake) Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Nuhu katika Quran
Katika somo hili utakwenda kujifunza historia ya Mtume Nuhu kulingana na melezo yaliyo kwenye Quran Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Yunus
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Yunus Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Muhammad (s.a.w) wa ufup
Huu n ufupisho wa Historia ya Mtume Muhammad s.a.w. Tumekuandalia histori hii kwa urefu zaidi kwenye Makala zetu zinazofuata Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Adam
ata post h utawenda ujfunza hstora ya Nabii Adam ulngana na Quran navyoeleza Soma Zaidi...

Hstoria ya Nabii Yusuf
Katika makala hii utakwenda ujfunzakuhusu historiaya Nabii Yufuf katika Quran Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Ya'qub
Katika somo hili utawenda ujfunz ahstoraya Nabii Ya'qub na familia yake Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Ismail katika quran
KKatika somohili utakwenda kujifunzahistoriaya Mtume Ismail Mtoto wa Nabii Ibrahim Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Ibrahimu
Katika post hii utakwenda kujifunza historia ya Mtume Ibrahim katika quran Soma Zaidi...

Hstoria ya Nabi Daud
Katika somo hili utawenda ujifunza uhusu historia ya Mtume Daud Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Ilyasa
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Ilyasa Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Yahya
Katika somo hili uatkwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Yahya Soma Zaidi...