image

Hstora ya Nabii Adam

ata post h utawenda ujfunza hstora ya Nabii Adam ulngana na Quran navyoeleza

Kuumbwa kwa Adam (a.s)

 

Adam(a.s) ni mtu na Mtume wa Allah(s.w) wa kwanza. Adam(a.s) ameumbwa kwa udongo uliofinyangwa ukafanywa kuwa sanamu la mtu kisha likapuliziwa roho na kuwa mtu kamili kama tunavyofahamishwa katika Qur-an:

Na (kumbuka) Mola wako alipowaambia Malaika, “Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo mkavu unaotoa sauti, wenye kutokana na matope meusi yaliyovunda.”“Basi nitakapomkamilisha na kumpulizia roho inayotokana na Mimi, basi mumuangukie kwa kumtii.” (15:28-29)

(Kumbuka) Mola wako alipowaambia Malaika: Hakika mimi nitaumbwa mtu kwa udongo. Na nitakapomkamilisha na kumpulizia roho inayotokana na mimi basi msujudieni (kama ishara ya kumheshimu). (38:71-72).


Hadhi ya Adam(a.s) na Kizazi Chake
Kabla ya Adam(a.s) kuumbwa, Allah(s.w) aliwafahamisha Malaika kuwa atamleta Khalifa (kiongozi) katika ardhi atakayesimamisha Ufalme wa Allah(s.w) (Dola ya kiislamu) kwa kufuata mwongozo wake Allah(s.w). Mazungumzo baina ya Allah(s.w) na Malaika wake juu ya ukhalifa wa Adam(a.s) na kizazi chake tunayapata katika aya zifuatazo:


(Wakumbushe watu khabari hii): Wakati Mola wako alipowambia Malaika: “Mimi nitaleta Khalifa katika ardhi.”

Wakasema (Malaika): “Utaweka humo watakaofanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutukuza kwa sifa zako na kukutaja kwa utakatifu wako?” Akasema (Mwenyezi Mungu): “Hakika Mimi nayajua msiyoyajua.”(2:30)

Na (Mwenyezi Mungu) akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya Malaika, na akasema (kuwaambia Malaika): “Niambieni majina ya vitu hivi ikiwa mnasema kweli (kuwa nyinyi ndio wajuzi wa mambo).”(2:31)


 

Wakasema (Malaika): “Utakatifu ni wako! Hatuna ilimu isipokuwa ile uliyotufundisha; bila shaka wewe ndiye Mjuzi na ndiye Mwenye hikima.” (2:32).

Akasema (Mwenyezi Mungu): “Ewe Adam! Waambie majina yake.” Alipowaambia majina yake alisema (Mwenyezi Mungu) “Sikukwambieni kwamba mimi najua siri za mbinguni na za ardhi; tena najua mnayoyadhihirisha na mliyokuwa mnayaficha?”.(2:33)

Na (wakumbushe watu khabari hii): Tulipowaambia Malaika “Msujudieni Adam”. Wakamsujudia wote isipokuwa Iblis; akakataa na akajivuna; na (tokea hapo) alikuwa katika makafiri(2:34)


Kutokana na aya hizi tunajifunza yafuatayo:

Kwanza ,Adam(a.s) na kizazi chake(wanaadamu) wamekusudiwa kuwa Makhalifa wa Allah (s.w) katika ardhi, yaani kuwa wasimamishaji wa Ufalme wa Allah(s.w) katika ardhi (Dola ya Kiislamu) kwa niaba yake pamoja na kuwa yeye mwenyewe ni Muweza wa kuusimamisha kwa kusema: “kuwa” na “ukawa”.

Pili, ili kuweza kusimamisha ukhalifa katika ardhi watu hawanabudi kuwa na ujuzi wa kutosha juu ya mazingira ya ardhi na namna ya kukabiliana nayo. Nabii Adam(a.s) kufundishwa “majina ya vitu vyote” ni kielelezo kuwa alifunzwa fani zote za elimu zinazohitajika katika kuendea kila kipengele cha maisha ya binafsi na ya jamii ya mwanaadamu hapa ardhini. Pamoja na elimu ya vitu mbali mbali (elimu ya mazingira), Adam(a.s) na kizazi chake waliahidiwa kuletewa mwongozo kutoka kwa Allah(s.w) utakaowawezesha kusimamisha ukhalifa na kuvuna matunda yake ambayo ni kuishi kwa furaha na amani na kupata radhi za Allah(s.w) hapa duniani na huko akhera kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:


 

“Tukasema: Shukeni humo nyote (kutoka peponi) na kama ukikufikieni uwongozi utokao kwangu, wale watakaoufuata uwongozi wangu huo, haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.(2:38)


 


Lakini wenye kukufuru na kuyakadhibisha maneno yetu, hao ndio watakaokuwa watu wa motoni, humo watakaa milele”. (2:39)

Tatu, kusimamisha ukhalifa katika ardhi au kusimamisha Uislamu katika jamii ni jambo linalompandisha mwanaadamu hadhi na daraja mbele ya Allah(s.w) kuliko ile hadhi na daraja ya Malaika mbele ya Allah(s.w). Hili linadhihirika pale Malaika walipoamrishwa kumsujudia Adam(a.s). Sijda ni kitendo cha heshima ya hali ya juu kinachomstahiki Allah(s.w) peke yake, lakini kama ishara ya kuonesha hadhi ya Khalifa (Naibu) wa Allah(s.w), hapa ardhini, Allah(s.w) aliwaamrisha Malaika wamsujudie Adam na wakatii. Ubora wa kusimamisha Ukhalifa (Uislamu) katika jamii pia unadhihirishwa katika aya zifuatazo:


 


“Enyi mlioamini! Je! Nikujulisheni biashara itakayokuokoeni na adhabu iumizayo?(61:10)


 

(Biashara yenyewe ni hii);- Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na piganieni Dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu, haya ni bora kwenu ikiwa mnajua”. (61:-11)

 

Adam(a.s) na Mkewe Katika Pepo

 

Adam(a.s) aliumbiwa mkewe kutokana na asili ile ile kama tunavyojifunza katika Qur-an:


 

Enyi watu! Mcheni Mola wenu ambaye amekuumbeni katika nafsi (asili) moja. Na akamuumba mkewe katika nafsi ile ile. Na akaeneza wanaume wengi na wanawake kutoka wawili hao...........” (4:1).

Adam(a.s) na mkewe waliwekwa katika Bustani (Pepo) na wakapewa uhuru wa kufurahia wapendavyo ndani ya bustani hiyo na kula matunda yote wapendavyo lakini

wasikurubie matunda ya mti moja tu waliobainishiwa. Iblis (shetani), alimlaghai Adam(a.s) na mkewe wakala matunda ya mti ule waliokatazwa.


 

(kisha Allah akasema): “Na wewe Adamu! Kaa Peponi pamoja na mkeo, na kuleni mnapopenda, lakini msiukaribie mti huu msije kuwa miongoni mwa waliodhulumu (nafsi zao).” (7:19)


 

Basi Shetani; (naye ni yule Iblisi), aliwatia wasiwasi ili kuwadhihirishia aibu zao walizofichiwa, na akasema: “Mola wenu hakukukatazeni mti huu ila (kwa sababu hii) msije kuwa Malaika au kuwa miongoni mwa wakao milele (wasife).(7:20)


 


Naye akawaapia (kuwaambia): “kwa yakini mimi ni mmoja wa watowao shauri njema kwenu.” Basi akawateka (wote wawili) kwa khadaa (yake). Na walipouonja mti ule, aibu zao ziliwadhihirikia na wakaingia kujibandika majani ya (miti ya huko) Peponi. Na Mola wao akawaita (akawaambia) “Je, sikukukatazeni mti huu na kukwambieni ya kwamba Shetani ni adui yenu aliye dhahiri?” (7:21-22)
Tofauti na Iblis ambaye baada ya kumuasi Mola wake hakujuta

hata baada ya kukumbushwa, Adam(a.s) na mkewe walijuta sana kwa kumuasi Mola wao kisha wakalalama kwake kuleta toba:


 

“Mola wetu! Tumedhulumu nafsi zetu; na kama hutatusamehe na kuturehemu, bila shaka tutakuwa miongoni mwa wenye khasara (kubwa kabisa)”. (7:23).

Kisa cha kulaghaiwa Adam na Hawwah na adui yao Ibilis mpaka wakamuasi Mola wao kwa kula matunda waliyokatazwa, kinatufunza kuwa kuna maadui wasiopenda kuona Allah(s.w) anatiiwa ipasavyo katika kuendea kila kipengele cha maisha ya kila siku. Na adui mkubwa kwa waumini ni shetani ambaye huingia katika nyoyo za watu na kuwahadaa kwa kuwapambia mambo maovu na kuyafanya mazuri kama Ibilis (mkuu wa mashetani) alivyo wahadaa wazazi wetu kwa kuwaambia


 

“Ewe Adamu, Je! Nikujulishe mti wa umilele na wa Ufalme usiokoma?(20:120),aidha aliwaambia:“Mola wenu hakukukatazeni mti huu ila msije kuwa Malaika au kuwa miongoni mwa wakaao milele (wasife)” (7:20).

Shetani hakuishia hapo, bali aliwaapia kwa kuwaambia:


“..................Kwa yakini mimi ni mmoja wa watowao shauri njema kwenu.” (7:21).

Hivyo waumini pamoja na jitihada zao za kuhuisha Uislamu na kuusimamisha katika jamii, hawana budi kuwa makini sana na adui

shetani ambaye daima huwajia watu kwa hadaa, tashwishi na ahadi za uongo. Mashetani ambao ni miongoni mwa majini na watu, huwapotosha watu na njia ya Allah(s.w) kupitia udhaifu wa matashi waliyo nayo; kwa mfano kama mtu anatamani kupata vitu vizuri kwa urahisi bila ya kuvifanyia juhudi stahiki,shetani atampambia aviendee vitu hivyo kwa njia ya kumuasi Mola wake japo anaweza pia asivipate kama si katika makadirio ya Allah(s.w). Tamaa ya kuwa Malaika au kuishi milele ndiyo iliyowaponza wazazi wetu, Adam na Hawwah. Tujue kuwa shetani hanauwezo wa kumlazimisha mtu kumuasi Mola wake kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:


 

“Akasema (Iblis): Mola wangu! Kwa Sababu umenihukumu kupotea, basi nitawapambia (wanaadamu upotevu) katika ardhi na nitawapoteza wote. (15:39)


 


Isipokuwa waja wako waliosafika kweli kweli. Akasema (Mwenyezi Mungu) Hii njia yao ya (kuja) kwangu imenyooka. Hakika waja wangu, wewe hutakuwa na mamlaka juu yao; isipokuwa wale wenye kukufuata (kwa khiari zao) katika hao wapotofu.” (15:40-42)

Wanaharakati wa kuhuisha Uislamu katika jamii wataepukana na hadaa za sheitwani kwa kufanya harakati kwa Ikhlas na kufuata vilivyo Qur-an na sunnah pamoja na kuomba msaada wa Allah(s.w) na kujikinga kwake na sheitwani kama Qur-an inavyotuongoza:


 


“Sema: Najikinga na Bwana Mlezi wa watu, Mfalme wa watu, Mola wa watu, na shari ya mwenye kutia wasiwasi, mwenye kurejea nyuma, atiaye wasiwasi nyoyoni mwa watu ambaye ni katika majini na watu.” (114:1-6).


au kuleta dua ifuatayo:


 


“.........Mola wangu! Najikinga kwako uniepushe na wasiwasi wa mashetani. Najikinga kwako Mola wangu, ili wasinihudhurie”(23:97-98)

Pamoja na kujikinga na sheitwani, hatunabudi kujiepusha na tabia za kishetani kama kuwa na kibri, majivuno na chuki binafsi dhidi ya watu pasina sababu ya msingi.

 

 

Kibri cha Ibilis na Uadui Wake Dhidi ya Binadamu

 

Ibilis ni katika jamii ya majini aliyekuwa pamoja na Malaika wakati amri ya kumsujudia Adam inatolewa. Iblis alitarajiwa kutii

amri hiyo ya Mola wake pamoja na Malaika, lakini hakufanya hivyo bali alitakabari kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:


 


“Basi Malaika wakatii (amri ya kusujudu) wote pamoja isipokuwa Ibliis, akajivuna na akawa katika makafiri.” (Allah) akamuuliza: “Ewe Ibilis! Kipi kilichokuzuia kumtii yule niliyemuumba kwa mikono yangu?” Je! Umetakabari au umo miongoni mwa wakubwa (kweli)? (38:73-75)


 


Akasema (Ibilis katika kujibu): “Mimi ni bora kuliko yeye, kwani mimi umeniumba kwa moto na yeye umemuumba kwa udongo” (38:76)

Ibilis badala ya kuzingatia amri ya Mola wake na kutii, amepeleka fikra zake kwenye asili ya umbile la Adam(a.s) na kuanza kujifananisha naye na kuona kuwa asili ya umbile lake ni bora kuliko ile asili ya umbile la Adam(a.s). Hatakama ingelikuwa kweli kuwa moto ni bora kuliko udongo, Iblis asingelipaswa kukataa kumsujudia Adam(a.s) kwa sababu si Adamu aliyetaka asujudiwe, bali aliyetoa amri ya kumsujudia Adam ni Allah(s.w) ambaye ni Muumba wa Adam na Ibilis.

Baada ya Ibilis kuvunja amri ya Mola wake kwa takaburi kiasi hicho, alilaaniwa na kubaidishwa (kufukuzwa) na rehema za Mola wake:


 

(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi toka humo kwani umetengwa na rehema. Na hakika laana yangu itakuwa juu yako mpaka siku ya malipo.”(38:77-78)

Badala ya Ibilis kukiri kosa lake na kumuelekea Mola wake kwa toba ya kweli, alielekeza lawama zake kwa Adam(a.s) na kuapa mbele ya Allah (s.w) kuwa atalipiza kisasi kwa Adam(a.s) na kizazi chake kwa kukipoteza na njia ya Allah(s.w):


 

“Akasema (Ibilis) Naapa kwa haki ya utukufu wako, bila shaka nitawapoteza wote (hao watoto wa huyu adui yangu – Adam)” (38:82)


 


“Akasema: “Kwa kuwa umenihukumia upotofu (upotevu) basi nitawakalia (waja wako). Katika njia yako iliyonyooka (ili niwapoteze) kisha nitawafikia kwa mbele yao na nyuma yao na kuumeni kwao na kushotoni kwao, wengi katika wao hutawakuta ni wenye kushukuru.(7:16-17)


 

Akasema (Mwenyezi Mungu). Toka humo, hali ya kuwa ni mwenye kudharauliwa na mwenye kufukuzwa. Atakayekufuata miongoni mwao (nitamtia motoni) niijaze Jahannamu kwa nyinyi nyote.”(7:18).

Iblis mwenyewe alikiri kuwa hataweza kuwapoteza wale waja wema waliomshika sawa sawa Mola wao kama tunavyojifunza katika Qur’an:


 

“Akasema Mola wangu! kwa sababu umenihukumu kupotea, basi nitawapambia(upotofu) katika ardhi na nitawapoteza wote. Isipokuwa wale waja wako waliosafika kweli kweli. Mwenyezi Mungu akasema: Hii njia yao ya kuja kwangu imenyooka wanaweza kunijia wakati watakao. Hakika waja wangu wewe hutakuwa na mamlaka juu yao isipokuwa wale wenyue kukufuata kwa khiari zao katika hao wapotofu.(15:39-42).

 

 

Adam na Hawah Kushushwa Ardhini


(Wakumbeshe watu khabari hii) wakati Mola wako alipowaambia

Malaika: “Mimi niteleta Khalifa kukaa katika ardhi” (2:30).

Hivyo bustani aliyowekwa ilikuwa ni mapito tu. Awamu ya kwanza ya maisha ya mwanaadamu ilikuwa ni peponi, awamu ya pili ni maisha ya hapa ardhini awamu ya tatu maisha ya Barzakh (kaburini) na awamu ya nne baada ya hukumu (Siku ya Kiyama),

maisha ya milele, peponi au motoni. Mwanzo wa mwanaadamu kuishi katika ardhi unabainishwa na aya zifuatazo;

 


Akasema (Mwenyezi Mungu): “Shukeni (katika ardhi), nyinyi kwa nyinyi ni maadui. Na makao yenu yatakuwa katika ardhi, na starehe yenu (pia) mpaka muda (niutakao mimi mwenyewe)”.Akasema (Mwenyezi Mungu): “Mtaishi humo na mtafia humo, na mtatolewa humo (mtafufuliwa kwenda Akhera kulipwa)” (7:24-25).


Mwongozo wa Allah kwa Wanaadamu.
Allah(s.w) hakumuacha Khalifa wake aanze maisha gizani. Bali alimpa mwongozo wa namna ya kuutekeleza Ukhalifa wake. Tunasoma katika Qur’an:

 


Tukasema: “Shukeni humo nyote, na kama ukikufikieni mwongozo utokao kwangu basi watakaofuata uongozi wangu huo haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika, lakini wenye kukufuru na kuyakadhibisha maneno yetu, hao ndio watakaokuwa watu wa motoni, humo watakaa milele” (2:38-39).

Utaratibu wa Allah unaobainishwa na aya hizi wa kuleta mwongozo unafanya kazi toka binaadamu wa mwanzo, Adam, hadi wa mwisho wa maisha haya ya duniani. Ni ahadi aliyoichukua Allah(s.w) kuwaletea waja wake mwongozo. Mwongozo ambao unakusudiwa watu waufuate wasibuni mifumo ya maisha kinyume na ule aliouleta Allah(s.w). Na zipo njia mbili tu za kuujua mwongozo wa Allah(s.w).
 

Ama mtu kuletewa Wahyi (Mitume) au kusoma kutoka kwa walioletewa Wahyi. Ndio maana tunaona Allah(s.w) ameleta Mitume pamoja na vitabu kuubanisha mwongozo huo.

Mwongozo huo umeletwa hatua kwa hatua, hadi kufikia kwa Mtume wa mwisho. Ni mwongozo unaokigusa kila kipengele cha maisha kwa mtu binafsi, taifa, na kimataifa katika ngazi zote, hali zote, mahali popote na wakati wowote. Hapana anachokihitajia mwanaadamu ila kimebainishwa katika mwongozo wa Allah(s.w)

 

Historia ya Watoto Wawili wa Nabii Adam .

“Na wasomee khabari za watoto wawili wa Adam kwa kweli, walipotoa sadaka, ikakubaliwa ya mmoja wao na ya mwingine haikukubaliwa Akasema (yule asiyekubaliwa sadaka yake): “Nitakuua”. Akasema (yule aliyeahidiwa kuuawa): “Mwenyezi Mungu huwapokea wamchao tu”. “Kama utanyoosha mkono wako kwangu kuniua, mimi sitanyoosha mkono wangu kukuuwa. Hakika mimi ninamuogopa Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu .


“Mimi nataka ubebe dhambi zangu na dhambi zako, na kwa hivyo uwe miongoni mwa watu wa motoni. Na haya ndiyo malipo ya madhalimu”.“Basi nafsi yake ikamwezesha kumwua nduguye, na akawa miongoni mwa wenye kukhasirika”. Hapo Mwenyezi Mungu akamleta Kunguru anayefukua katika ardhi ili amwonyeshe jinsi ya kuificha maiti ya ndugu yake. Akasema: (yule ndugu aliyeua) “Ole wangu: Nimeshindwa kuwa sawa na kunguru huyu na kuficha maiti ya ndugu yangu”? Basi akawa miongoni mwa wenye kujuta. Kwa sababu ya hayo tukaawandikia wana wa Israel ya kwamba atakayemuua mtu bila ya yeye kuua mtu, au bila ya kufanya fisadi katika nchi, basi ni kama ameua watu wote, na mwenye kumwacha mtu hai (kumsaidia kuishi) ni kamaH amewaacha hai watu wote. Bila shaka Mitume waliwafikia na hoja zilizo wazi; kisha wengi katika wao baada ya haya walikuwa waharibifu sana katika nchi” (5:27-32).


 

Katika ya hizi majina ya watoto hawa wa Adam hayakutajwa. Bali majina hayo yamechukuliwa kutokana na maandishi mengi ya historia hasa historia ya Mayahudi. Wafasiri wengi wa Qur’an wanataja katika kuzitafsiri aya hizi kuwa, Habil na Kabil ni watoto wa moja kwa moja wa Adam na Hawwa. Na sio imetajwa kwa ishara tu kwa kuzingatia kuwa watu wote wametokana na Adam na Hawwa. Kwa mujibu wa maelezo ya Sheikh A. S. Farsy, hiki ndicho kisa cha awali cha mtu kumuua mwenziwe. Na aliyeuawa ndiye mwanaadamu wa mwanzo kufa. Kwa sababu hiyo basi aliyefanya mauaji hakujua nini la kufanya na yule maiti. Ndipo Allah(s.w) akamleta kunguru kumwonyesha namna ya kuhifadhi maiti ya ndugu yake.


 

Ili kuyafahamu vyema mafundisho ya kisa hiki cha watoto wa Adam(a.s) ni vyema tuyazingatie mazingira na wakati ziliposhuka aya za kukielezea kisa chenyewe. Tunafahamu kuwa awali Allah(s.w) aliwachagua Mayahudi na kuwapa ujumbe wake ili watekeleze wao wenyewe na kisha waufikishe kwa watu. Kwa hiyo akawatuma Mitume wengi miongoni mwa Mayahudi. Kutokana na neema hii waliyopewa kuletewa mwongozo na kupewa jukumu la kuusimamia, wakawa ni watu wenye hadhi kubwa.


 

“Enyi kizazi cha Israil (Mayahudi); Kumbukeni neema zangu nilizokuneemesheni na nikakutukuzeni kuliko viumbe wengine (wa wakati huo)” (2:47).

Hata hivyo Mayahudi hawakuithamini neema hii ila wachache tu. Zaidi ya wao wenyewe kutokufuata mwongozo waliwaua mitume na kufuata baadhi ya kitabu huku wakiacha sehemu nyingine. Hii iliwapelekea kupata laana ya Allah(s.w).

Aidha Mayahudi waliobashiriwa kuja kwa Mtume(s.a.w) na waliahidi kuwa watamfuata. Bali alipokuja walimkataa.


 


Na(wakumbushe)aliposema (Nabii) Isa bin Maryam(kuwaambia Mayahudi): Enyi wana wa Israil! Mimi ni mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, nisadikishaye yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na kutoa habari njema ya Mtume atakayekuja nyuma yangu ambaye jina lake litakuwa Ahmad(Muhammad). Lakini alipowajia na hoja zilizo wazi walisema: Huu ni udanganyifu ulio dhahiri. (61:6)


 

Mayahudi hawakuishia kumkataa tu Mtume(s.a.w) walidhamiria kumwua pia. Hapakuwa na jingine lililowapelekea kufanya hayo, bali ni husuda na kibri. Ilikuwa wao baada ya kunyan’ganywa neema ya kuwa wafikishaji wa ujumbe wa Allah, watanabahi na kufanya mema ili Allah aweze kuwasamehe. Lakini wao walimwonea husuda Mtume(s.a.w) na wakawa wanafanya njama za kumwuua.


 

Ni katika mazingira haya Allah(s.w) anabainisha kisa hiki cha watoto wa Adam(a.s) ili kuwaonya Mayahudi na sisi sote kuwa: Tusiwe na husuda juu ya Neema na amali njema za watu weninge hata tukaingia kwenye makosa kama ya mtoto wa Adam. Bali nasi tuzitakase nafsi zetu kwa kutenda mema asaa Allah(s.w) nasi akatuinua daraja.


 

Allah hawaongoi na kuwapokelea maombi watu madhalimu. Aidha uongofu haupatikani kwa kumwonea husuda na kijicho mwenye kufanya mema. Bali kwa kujitakasa na kufanya amali njema.


……….Akasema (yule asiyokubaliwa sadaka yake) nitakuwa” Akasema (yule aliyeaahidiwa kuuawa) “Mwenyezi Mungu huwapokealea wamchao tu.” (5:27)


 

Vile vile Uislamu unatutaka tusiwe ni wenye kulipiza ubaya juu ya ubaya tunaotendewa. Mtu anatakiwa ajitetee na awatetee wengine dhulma inapotaka kufanyika. Lakini asipike uovu dhidi ya wengine. Bali amuogope Allah(s.w) na kushika njia iliyo sawa:


 

“Kama utanyosha mkono wako kwangu kuniua; mimi sitakuyooshea mkono wangu kukuua, hakika mimi namwongopa Mwenyezi. Mola wa walimwengu pia.” (5:28)

 

 

Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Adam(a.s)

(i) Utukufu wa mtu katika Uislamu hautokani na nasaba, rangi,kabila,utajiri ila uwajibikaji kwa Allah(s.w)unaolandana na Elimu sahihi.

(ii) Tujiepushe na tabia ya kiiblis ya kumtukuza au kumdharau mtu kutokana na nasaba, rangi, sura, hali yake kiuchumi, n.k.

(iii) Tujiepushe na tabia ya Kiiblis ya kuwa na chuki binafsi dhidi ya watu wasio na hatia yeyote.

(iv) Tujiepushe na tabia ya Kiiblis ya kibri na majivuno.

(v) Tuwe na msimamo katika kutekeleza amri za Allah(s.w) na Mtume wake na tusiwe tayari kuyumbishwa na hadaa za shaitwani.

(vi) Tunapofikwa na tashwishi za kishetani tujikinge kwa Allah(s.w).


 

“Na kama shetani akikushawishi kwa tashwishi (zake), wewe jikinge kwa Mwenyezi Mungu (kwa kusema: A’uudhubillah Minash-shaytwanir-Rajiim). Yeye ni mwenye kusikia mwenye kujua.” (41:36)

Au ujikinge kwa kusema:


 


Sema: najikinga kwa Bwana mlezi wa watu. Mfalme wa watu. Muabudiwa wa watu. Na shari ya mwenye kutia wasiwasi mwenye kurejea nyuma. Atiaye wasiwasi nyoyoni mwa watu. Ambaye ni katika majini na watu. (114:1-6)

Au kuleta Dua ifuatayo:


 


“...... Mola wangu! Najikinga kwako uniepushe na wasiwasi wa mashetani. Na najikinga kwako, Mola wangu, ili wasinihudhurie”. (23:97-98)


(vii) Muda wote Waislamu hawana budi kuchukua tahadhari kwani kiasili (tangu mwanzo wake) Uislamu ni dini yenye maadui miongoni mwa mashetani wa kijini na watu.


 

................

“Na namna hii tumemfanyia kila Nabii maadui, (nao ni) mashetani katika watu na majini. Baadhi yao wanawafunulia wenziwao maneno ya kupamba pamba ili kuwadanganya…..........” (6:112)


(viii)Mwanaadamu tangu mwanzo wa kuumbwa kwake amekusudiwa kuwa Khalifa katika ardhi na nyenzo kuu ya kumuwezesha kuwa Khalifa ni elimu ya mazingira na ya mwongozo.

(ix) Tujiepushe na kuwahusudu watu juu ya meema walizotunukiwa na Allah(s.w) bali tumuelekeeAllah(s.w) kwa unyenyekevu na
k umuomba atuneemeshe kama wale aliowaneemesha.

Wala msitamani vile ambvyo MwenyeziMungu amewafadhilisha badhi yenu (kwa vitu hivyo) kuliko wengine. wanaume wanayo sehemu (kamili) ya vile walivyovichuma; na wanawake nao wanayo sehemu(kamili) ya vile walivyovichuma na mwombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.(4:32)

(x) Allah(s.w) huwaongoza na kupokea maombi ya wale wajitakasao:
........

“...... Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubu na kuwapenda wanaojitakasa” (2:222)

(xi) Muislamu muumini anatakiwa ajihidi kuondosha ubaya au alipize ubaya aliofanyiwa kwa wema,yaani kumsamehe aliyemkosea kumpa aliyemnyima na kumchangamkia aliye mkasirikia. Tunahimizwa katika Qur’an:


 

“Mambo mazuri na mabaya hayawi sawa. Ondosha (ubaya uliofanyiwa kwa wema), tahamaki yule ambaye baina yako na baina yake kuna uadui atakuwa kama ni jamaa (yako) mwenye kukufia uchungu. Lakini (jambo hili) hawatapewa ila wale wanaosubiri wala hawatapewa ila wenye hadhi kubwa (mbele ya Mwenyezi Mungu)”(41:34-35)

(xii) Tunapoteleza na kumkosea Allah(s.w),tumuelekee kwa unyenyekevu kwa kuleta toba ya kweli kama alivyofanya Adam(a.s) na mkewe.

(xiii) Kumkosea Allah(s.w) kwa kibri kama alivyofanya Iblis ni jambo baya mno la hatari kwani humpelekea mtu kupigwa muhuri moyoni mwake kiasi cha kumfanya asione haja yoyote ya kuleta toba. Tunakumbushwa hili katika Qur’an.


 

“Hakika wale waliokufuru (kwa ukaidi tu na inadi) ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye hawataamini. Kama kwamba Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya ya nyoyo zao na juu ya masikio yao; na juu ya macho yao pana kifuniko; basi watakuwa na adhabu kubwa.”(2:6-7)

 

Mwisho:

Katika somo linalofuata utajifunza uhusu hstora ya Nabii  Idrsa (a.s)





           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Rajabu Tarehe 2024-06-25 17:48:50 Topic: visa vya Mitume Main: Masomo File: Download PDF     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 553


Sponsored links
👉1 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)     👉2 Simulizi za Hadithi Audio     👉3 Kitabu cha Afya     👉4 kitabu cha Simulizi     👉5 Kitau cha Fiqh     👉6 Madrasa kiganjani    

Post zifazofanana:-

Histora ya Nabi Zakariya
Katika somo hili utakwenda ujfunza kuhusu hslistoria ya Nabi Zakariya Soma Zaidi...

Historiaya Nabii Isa
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu Historia ya Nabii Isa Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Adam
ata post h utawenda ujfunza hstora ya Nabii Adam ulngana na Quran navyoeleza Soma Zaidi...

hHistoria ya Nabii Dhul-kifl
Katika makala hii tutakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Dhul-kifl Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Ibrahimu
Katika post hii utakwenda kujifunza historia ya Mtume Ibrahim katika quran Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Ismail katika quran
KKatika somohili utakwenda kujifunzahistoriaya Mtume Ismail Mtoto wa Nabii Ibrahim Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Al-yasa’a
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Mtume Al-yasa'a Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Lut
Katika somo hili utakwenda kujifunza historia yaMtume Lut kutoka katika Quran Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Yahya
Katika somo hili uatkwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Yahya Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Swaleh (Salih)
Katika post hii utakwenda kujifunza historia ya Mtume Swalehe katikaQuran Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Idrisa
Katika somohili utakwenda kujifunza historia ya Nabii Idrisa (amani iwe juu yake) Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Ilyasa
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Ilyasa Soma Zaidi...