atika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Musa
Nabii Musa(a.s) ni Mtume aliyeandaliwa na Allah(s.w) kuwakomboa Bani Israil (Waisraili) waliofanywa kuwa watumwa nchini Misri. Waisraili ni kizazi cha Nabii Ya‘aquub(a.s),Nabii Yusufu(a.s) ndiye alianza kukaa Misri kisha wakafuatia wazazi na ndugu zake wote wakati alipokuwa kiongozi nchini humo.
Allah(s.w) alimtuma Nabii Musa(a.s) kuwakomboa Bani Israil kwasababu haki yao ya kuwa huru ambayo Allah(s.w) amempa kila mwanadamu, iliporwa! Maadamu Bani Israil waliporwa haki hii kuu ya msingi; Allah(s.w) kwa uadilifu wake akamtuma Nabii Musa(a.s) kutekeleza jukumu zito la kuwakomboa na kuwarejeshea haki zao za kibinadamu walizonyang’anywa.
Hakika Firauni alitakabari katika ardhi, na akawafanya watu wa huko makundi mbalimbali. Akalidhoofisha kundi moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wakiume na kuwa acha hai watoto wao wa kike. Hakika yeye alikuwa miongoni mwa waharibifu (28:4)
Aya hii zimeweka wazi ukiukwaji wa haki za binadamu walioufanya watawala wa Misri. Lengo la kuhalalisha ukatili na mauwaji hayo lilikuwa kuwadhoofisha wananchi wenye nasaba ya Nabii Yusufu(a.s) wasipate nafasi ya kuongoza tena.
Musa(a.s) alizaliwa wakati bado msako unafanywa na askari wa Firauni kumwua kila mtoto wa kiume wa Kiisrail anayezaliwa. Kwa rehema zake Allah(s.w) mama yake Musa alijifungua bila kutambulika kwa askari wa Firauni. Na ili kumlinda zaidi Allah(s.w) alimteremshia Wahy mama yake Musa.
Ya kwamba mtie sandukuni, kisha litie mtoni, na mto utamtupa ufukoni ili amchukue adui yangu na adui yake (amlee kwa vizuri Naye ni Firaun). Na nimekutilia mapenzi yatokanayo kwangu (ili upendwe na watu wote), na ili ulelewe machoni mwangu.(20:39)
Baada ya kumtupa mtoni, mama yake akamtuma dada yake Musa kufuatilia:
Akamwambia dada yake: “Mfuate”. Basi yeye akamwangalia kwa mbali bila wao kumjua (28:11)
Kitoto Musa kiliokotwa na kufikishwa kwa Firaun. Mkewe Firaun akamrai mumewe kuwa wasimuue bali wamfanye mtoto wao wa kulea.
Na mkewe Firauni akasema (Kumwambia mumewe) “Usimuuwe, atakuwa kiburudisho cha macho kwangu na kwako; na msimuuwe;huwenda atatunufaisha, au tumpange kuwa mtoto wetu,walisema haya hali ya kuwa hawatambui(kuwa atakuwa adui yao)”(28:9)
Watu wa Firauni walipomwokota Musa bila shaka walitambua kuwa ni mtoto wa Kiisrail na walimpeleka kwa Firauni ili auawe kama watoto wengine Wakiisrail. Lakini mke wa Firauni alivutiwa na uzuri wa mtoto Musa. Ambaye kwa kweli Allah(s.w) alimfanya awe ni mwenye kupendeza machoni kwa watu. Allah(s.w) Ajaalia Musa(a.s) Kunyonyeshwa na Mama Yake Mzazi
Kwa uwezo wake, Mwenyezi Mungu aliharamisha Musa asinyonyeshwe na yeyote yule isipokuwa mama yake. Hivyo, dada yake Musa alijitokeza nyumbani kwa Firauni na kupendekeza:
“.........Basi akasema: Je nikuonesheni watu wa nyumba watakaomlea kwa ajili yenu, na pia watakuwa wema kwake? (28:12)
Dada yake Musa(a.s) alimpendekeza mama yake ambaye Firauni hawakumjua kuwa ndiye mama mzazi wa Nabii Musa(a.s). Ombi hilo lilikubaliwa na Musa(a.s)alirejeshwa kwa mama yake:
Basi tukamrejesha kwa mama yake ili macho yake yaburudike, wala asihuzunike; na ajue ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli, lakini watu wengi hawajui (28:13)
Allah(s.w) Amruzuku Musa(a.s) Elimu
Ili kuweza kutekeleza jukumu la kutetea haki za binadamu na kuwaongoza watu katika njia iliyonyooka, Mwenyezi Mungu akamjaalia Musa elimu ya kutosha na akili yenye upeo mkubwa wa kupembua mambo. Tunafahamishwa kuwa:
Na Musa alipofikia baleghe yake na kustawi, tulimpa akili na elimu, na hivi ndivyo tunavyowalipa watu wema (28:14)
Mchana wa siku moja Musa(a.s) alimuona mtu wa Firauni amemuelemea Muisrail akimtwanga makonde mazito. Musa alichukizwa na kitendo kile, hivyo alipoombwa msaada alijikuta amemtwika Mmisri huyo ngumi nzito na kumuuwa palepale. Hapo Musa(a.s) akashituka na kuleta toba:
Mola wangu! Bila shaka nimedhulumu nafsi yangu, basi nisamehe; naye (Allah) akamsamehe. Kwa hakika yeye ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kurehemu. (28:16)
Akasema: Mola wangu! Kwa kuwa umenineemesha, basi sitakuwa kabisa msaidizi wa watu wabaya. (28:17)
Habari ile ya kuuliwa mtu na Musa(a.s) ilifika kwa Firaun na ikatoka shauri kuwa Musa(a.s) akamatwe na kuuliwa. Musa(a.s) alipopata habari za kuaminika kutoka kwa mtu mwema,kuhusu hukumu ile, aliamua kutorokea nchini Madian katika mji awa Al-Bid uliopo kilometa 480 hivi mashariki ya Misr. Alipofika Madian hakuwa na pakwenda bali alijipumzisha kisimani ambapo aliwasaidia wasichana wawili kuwanywesha wanyama wao. Wasichana wale hawakuweza kupigana vikumbo na wanaume katika kunywesha wanyama wao, wakawa tu wanabakia pembeni wanaangalia. Kitendo kile kilimfurahisha Mzee wa Madian na akaagiza Musa(a.s) aitwe ili apate ujira wa kazi ile.
Basi akamjia mmoja katika (wasichana) wale wawili, anakwenda na huku anaona haya, akasema: “Baba yangu anakuita ili akulipe ujira wa kutunyweshea..........(28:25)
Musa alipofika kwa yule mzee alimsimulia hali halisi kuhusu dhulma, ukandamizaji na ukiukwaji wa haki za binadamu uliopo nchini Misri, pamoja na kisa kilichompelekea yeye kuhamia Madiani. Yule mzee akamtuliza Musa(a.s), akasema: Usiogope umekwisha kuokoka na watu madhalimu (28:25)
Akasema: Mimi nataka nikuoze mmoja wapo katika binti zangu hawa wawili kwa kunitumikia miaka minane na kama ukitimiza kumi hiari yako, lakini mimi sitaki kukutaabisha utanikuta Inshaa-Allah miongoni mwa watu wema .(28:27)
Musa(a.s) aliafiki suala hilo, na mmoja katika wale mabinti aliridhia kuolewa na Musa(a.s) kwa mahari ya kutoa nguvukazi:
“Akasema(Musa: “Mapatano) hayo yamekwisha kuwa baina yangu na baina yako; muda mmoja wapo nitakaoumaliza, basi nisidhulumumiwe; na Mwenyzi Mungu ni Mlinzi juu ya haya tunayoyasema.”(28:28)
Musa alipotimiza muda, alifunga safari na ahali zake kurejea Misri. Njiani aliona moto upande wa mlimani akawaambia ahali zake:
............Ngojeni hakika nimeona moto; labda nitakujieni na habari za huko au kijinga cha moto ili muote (28:29)
Basi alipofika, aliitwa: “Ewe Musa! Hakika Mimi ndiye Mola wako. Basi vua viatu vyako. Hakika wewe uko katika bonde takatifu la Tuwa. (20:11-12)
Nami nimekuchagua, (uwe Mtume). Basi yasikilize unayoelezwa kupitia wahy. Kwa yakini Mimi ndiye Mwenyezi Mungu, hakuna aabudiwaye kwa haki ila Mimi, Basi niabudu na usimamishe swala kwa kunitaja (20:13-14)
Nabii Musa(a.s)alimuomba Allah(s.w) amsaidie(amuwezeshe) kulimudu jukumu zito alilompa na pia alimuomba amfanye Harun(a.s) awe msaidizi wake. Harun alikuwa ndugu yake Musa(a.s)
Akasema: Ewe Mola wangu! Nipanulie kifua changu(nipe subira). Na unifanyie wepesi katika kazi yangu. Na ufungue fundo lililo katika ulimi wangu. Wapate kufahamu maneno yangu. Na unifanyie waziri katika jamaa zangu. Ndugu yangu Harun. Nitie nguvu kwa huyu. Na umshirikishe katika kazi yangu hii. Ili tukutukuze sana. Na tukutaje kwa wingi. Hakika Wewe unatuona (20:25-35)
Allah(s.w) alilikubali ombi la Nabii Musa (a.s), akamfanya Harun(a.s) kuwa Nabii pamoja naye. Allah(s.w) akasema kumwambia Musa: Hakika umekubaliwa maombi yako, Ewe Musa (20:36)
Jukumu kubwa la kwanza walilokabidhiwa Musa(a.s) na Harun(a.s) lilikuwa kumwambia Firauni amwamini Allah(s.w) na awache kukiuka haki za binadamu kwa kuwapa Waisraili uhuru wao. Basi wakamkabili Firaun wakamwambia:
...................Kwa hakika sisi ni Mitume wa Mola wako. Basi waachie wana wa Israili watoke pamoja nasi, wala usiwaadhibu. Hakika tumekuletea ishara zitokazo kwa Mola wako. Na amani itakuwa kwa wale wanaofuata uongofu (20:47)
Firauni kwa jinsi alivyokuwa amezama katika siasa za kidhalimu na unyonyaji hakupenda kabisa kuona Wana Israil wanarejeshewa haki zao za kibinadamu za kuwa huru. Akasema Firauni kwa kibri na jeuri kubwa kuwa: ............Enyi wakuu! Simjui kwa ajili yenu, mungu asiyekuwa mimi............(28:38)
Akasema: Mimi ndiye mola wenu mkuu. (79:24)
Nabii Musa(a.s.) alijitahidi kumuelimisha Firauni na watu wake juu ya Mungu mmoja anayekataza dhulma, ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu. Lakini Firauni kwasababu ya kupenda sana dhulma, akazusha uongo akiwatangazia watu kwa kuwaambia:
Bila shaka Mtume wenu aliyetumwa kwenu ni mwendawazimu(26:27)
Pamoja na kujibiwa kwa dharau na kukashifiwa, Musa aliendelea kufafanua zaidi juu ya Mwenyezi Mungu anayemiliki ulimwengu mzima.
.........(Allah ndiye) Mola wa Mashariki na Magharibi na vilivyomo baina yake ikiwa (mna akili) mfahamu (26:28)
Aliposhindwa kujibu hoja hiyo, Firauni akapandwa na hasira na kuanza kumtishia Musa(a.s):
Firauni akasema: Kama ukishikilia (kuwa kuna) Mungu mwingine badala yangu, kwa hakika nitakufanya miongoni mwa wenye kufungwa gerezani(26:29)
Lakini Musa(a.s) hakutishika kabisa kwa hizo kauli za Firauni. Badala yake akataka kumdhihirishia kuwa Allah(s.w) ana nguvu na uweza wa kufanya mambo makubwa ya kutisha zaidi kuliko hayo magereza yake.
Basi(Musa) akatupa fimbo yake, mara ikawa nyoka aliye dhahiri. Na akatoa mkono wake, na mara ukawa mweupe (kweli kweli) kwa watazamao(26:32-33)
Hapo Firaun akatishika na alidhani kuwa ile miujiza aliyokuja nayo Nabii Musa(a.s) ni sawa na mazingaombwe au viinimacho wanavyofanya wachawi.
Akasema, kuwaambia wakuu waliomzunguka: Hakika huyu ni mchawi ajuae sana. Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake; basi mnasemaje? (26:34-35)
Allah(s.w) alimjaalia Nabii Musa(a.s) miujiza ya kuthibitisha Utume wake. Miujiza si viinimacho kama ilivyo mazingaombwe. Muujiza ni jambo halisi lisilola kawaida ambalo hutokea kwa idhini ya Allah(s.w). Musa alipoulizwa na Allah(s.w) kuwa ameshika nini alisema:
.............Akasema: “Hii ni fimbo yangu, ninaiegemea na ninaangushia majani kwa ajili ya wanyama wangu. Tena ninaitumia kwa mambo mengine.(20:18)
Inadhihirika hapa kuwa Nabii Musa alikuwa na fimbo ya kawaida kabisa, lakini Allah(as) anaigeuza kuwa muujiza.
Allah(s.w) akasema: Itupe, ewe Musa”. Akaitupa. Mara ikawa nyoka anayekwenda mbio. Allah akasema: “Ikamate wala usiogope, sasa hivi Tutairudisha hali yake ya kwanza.(20:19-21)
“Na uambatanishe mkono wako katika kwapa lako; utatoka ukiwa mweupe sana pasipo na ubaya wowote. Huu ni muujiza mwingine. Ili Tukuoneshe miujiza mingine mikubwa (20:22-23)
Inabainika wazi kuwa chanzo cha miujiza yote aliyokuwa nayo Musa na Mitume wengine, ni Allah(s.w). Hakuna Mtume au Nabii aliyefanya miujiza kwa uweza wake mwenyewe!
Mawaziri waliokuwa washauri wakuu wa Firauni wakataka wakusanywe magwiji waliobobea katika uchawi nchi nzima, kisha wapambanishwe na Nabii Musa(as).
Basi walipofika wachawi, wakamwambia Firauni: Je, tutapata ujira tukiwa sisi ndio tutakaoshinda. Akasema: Naam, na pia mtakuwa miongoni mwa wale wanaowekwa mbele katika (Serikali) (26:41-42)
Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firauni sisi tutakuwa ndio wenye kushinda (26:44)
Kisha Musa akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza(vyote) walivyozusha wachawi (26:45)
Wachawi walipoona vitu vyao vya kichawi(viini macho) walivyovitupa uwanjani vimemezwa vyote na nyoka(wa muujiza), walisalimu amri na kutoa shahada:
Hapo wachawi walipinduka wakasujudu. Wakasema: Tumemuamini Mola wa walimwengu wote. Mola wa Musa na Harun (26:46-48)
Firaun aliwatishia wachawi kuwapa adhabu kubwa kwa kusilimu kwao pasina idhini yake (Qur’an 26:49). Inabainika hapa kuwa uchawi si sawa na muujiza,na ndio maana wachawi walishindwa. Hakika uliwadhihirikia ukweli kwamba Musa(a.s) ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Ndio maana Firauni alipotangaza kuwa atawasulubu kwa kuwakata miguu na mikono yao kwa sababu wamesilimu pasina ridhaa yake; hawakuyumba katika imani yao.
Wakasema: Haidhuru, hakika sisi sote tutarejea kwa Mola wetu. Kwa yakini sisi tunatumai ya kwamba Mola wetu atatusamehe makosa yetu, maana sisi tumekuwa wa kwanza wa wenye kusilimu hapa (26:50-51)
Kuangamizwa Firauni na Majeshi Yake
Baada ya ushindi alioupata Musa(a.s) dhidi ya wachawi, umati wa watu waliokuwa wamekusanyika kushuhudia mapambano baina ya haki na batili, waliona ukweli kuwa Musa(a.s) ndiye kiongozi halali anayepaswa kutiiwa, na haifai kabisa kutiiwa Firauni dhalimu. Kuanzia hapo waliomuamini Musa wakapata adha na mateso zaidi kutoka kwa Firauni. Ndipo Allah(s.w) alipomuamuru Musa(a.s):
“Nenda na waja wangu wakati wa usiku(mtoke nchini Misri), bila shaka mtafuatwa (26:52)
Na yalipokutana majeshi mawili. Watu wa Musa walisema. Hakika tutakamatwa. Musa akasema: La, kwa yakini Mola wangu Yu pamoja nami bila shaka ataniongoza.(26:61-62)
WanaIsrailwalikuwa wamekwama kuendeleana safari kutokana na kuzuiwa na bahari hali ya kuwa Firauni na majeshi yake yamekwisha wakaribia. Kwa huruma na rehema zake, Allah(s.w) akamuongoza Musa kwa kumwambia:
Bahari iligawanyika sehemu mbili na kuwacha njia ambayo Nabii Musa alipita na watu wake kwa salama. Lakini majeshi ya Firaun yalipofika katikati,maji ya bahari yalirudi katika nafasi yake na kuangamizwa yote. Firaun akawa anatapatapa, akijitupa huku na kule na akaona kuwa hapana nusra ila kutoka kwa Allah(s.w) ndipo akatoa shahada kuwa:
...............Naamini ya kwamba hakuna Mola aabudiwaye kwa haki ila Yule wanayemuamini wana wa Israeli, na mimi ni miongoni mwa wanaotii (10:90)
(Malaika wakamwambia)” Sasa (ndio unaamini)! hali uliasi kabla ya hapo na ukawa miongoni mwa waharibifu. Basi leo tutakuokoa kwa kuuweka mwili wako ili uwe dalili kwa ajili ya wa nyuma yako. Na watu wengi wameghafilika na ishara zetu.(10:91-92)
Huo ukawa ndio mwisho wa utawala wa kifirauni.
Kutokana na Historia ya Nabii Musa na Harun(a.s) tunajifunza yafuatayo:
(i) Tunajifunza kuwa ni muhimu kuweka mipango katika kuhuisha na kusimamisha Uislamu katika jamii. Allah(s.w) anauwezo wa kukiamrisha kitu “kiwe” na kikawa pale pale, lakini bado tunaona ameweka mpango wa muda mrefu wa
(ii) Vile vile mpango huu wa Allah(s.w) wa kuwakomboa Bani Israil,unatufunza kuwa kuibadilisha jamii ya kijahili kuwa ya Kiislamu ni jambo linalohitaji muda na subira.
(iii) Elimu na siha ni nyenzo muhimu za kumuwezesha mtu kuwa khalifa katika ardhi. Nabii Musa alipewa siha nzuri na kuruzukiwa akili na elimu.
(iv) Hakuna hila wala nguvu zinazoweza kuzuia jambo analotaka Allah(s.w) liwepo au lisiwepo katika jamii, yeye anazo namna nyinyi za kumlinda mja wake na vile vile anaweza kumuangamiza mbabe yeyote awaye.
(v) Tabia njema na kuwatendea watu wema ni nyenzo muhimu katika harakati za kusimamisha Uislamu katika jamii. Nabii Musa(a.s)kwa wema wake aliletewa taarifa ya mipango ya Firaun dhidi yake; pia kwa huruma yake alipata hifadhi kwa mzee wa Madian.
(vi) Hakuna binaadamu asiyeteleza na kumkosea Allah(s.w), lakini muumini anakuwa mwepesi wa kurejea kwa Allah (s.w).Musa(a.s) aliteleza kwa kuingilia ugomvi asioujua na kumuua mtu,alirejea kwa Mola wake haraka haraka–Qur-an (28:16).
(vii)Muumini wa kweli hanabudi kuchukia vitendo vya dhuluma na kuwa tayari kuwatetea wanaodhulumiwa haki zao kwa kadiri ya uwezo wake.
(viii)Ni muhimu kuwekeana mikataba ya kazi tunapoajiri au kuajiriwa. Nabii Musa(a.s) aliwekeana mkataba wa kazi na mzee wa Madian.
(ix) Nyenzo muhimu ya kutuwezesha kusimamisha Uislamu katika jamii baada ya Elimu ni kusimamisha Swala za Faradh na sunah,Qiyamullayl na kuleta dhikiri kwa wingi – Qur-an(20:14), (73:1-10), (74:1-7).
(x) Miujiza ni katika dalili za kuwepo Allah(s.w).
(xi) Katika harakati za kusimamisha Uislamu katika jamii tunatakiwa tusimvamie tu kila mtu na kumuingiza kwenye harakati, bali tuanze na ndugu, jamaa na rafiki wa karibu ambao tunajua fika tabia na mwenendo wao. Nabii Musa (a.s) aliomba ndugu yake Harun awe msaidizi wake si kwa kuwa alikuwa ndugu yake tu, bali alimfahamu fika kwa ucha Mungu wake.
(xii)Muumini mwanaharakati hahongeki kwa fadhila atakazofanyiwa na madhalimu ili arudi nyuma katika kusimamisha uadilifu. Musa(a.s) alilelewa katika nyumba ya mfalme,lakini hakuacha kudhihirisha kwa matendo udhalimu wa Firaun na serikali yake ikawa ndio sababu ya kuhukumiwa kifo.
(xiii)Ni kawaida ya matwaghuti kufanya propaganda dhidi ya wanaharakati na kuwapachika majina mabaya. Firaun na serikali yake alimpakazia Nabii Musa(a.s) uwendawazimu na uchawi.
(xiv)Hapana yeyote wa kumchelea katika kutekeleza amri ya Allah(s.w) ya kusimamisha Uislamu katika jamii. Musa na Harun(a.s) walimkabili Firaun na wakuu wake wa Dola waliozungukwa na majeshi na kuwafikishia ujumbe wa Allah(s.w).
(xv)Hapana yeyote mwenye uwezo wa kutweza au kutengua maamuzi ya nafsi ya mwanaadamu.Wachawi walipobainikiwa na Haki na wakasilimu, Firaun hakuweza kuwaritadisha pamoja na adhabu kali aliyoitoa dhidi yao – Qir-an (26:49-51).
(xvi)Toba inayokubalika ni ile inayoletwa haraka kabla ya kufikwa na mauti – Qur-an (4:18).
(xvii)Kuishi nje ya shahada na kutarajia kufa ndani ya shahada ni muhali. Allah(s.w) ametuamrisha tuishi na shahada na tujitahidi kubakia nayo mpaka kufa kwetu– Qur-an (3:102).
Jifunze zaidi, na wasiliana nasi ukiw ana App yetu. Bofya liln hapo chini kuweza ku download
Download NowJe! umeipenda hii post?
Ndio Hapana Save post
Rajabu Tarehe 2024-06-27 13:57:54 Topic: visa vya Mitume Main: Masomo File: Download PDF Share On Facebook or Whatsapp Views 582
Sponsored links
👉1
Kitabu cha Afya
👉2
Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)
👉3
Simulizi za Hadithi Audio
👉4
Madrasa kiganjani
👉5
Kitau cha Fiqh
👉6
kitabu cha Simulizi
Hstora ya Nab Ishaqa katika quran
Katika post hii tutakwenda kujifunza historia ya Mtume Ishaqa Soma Zaidi...
Hstora ya Nabii Yahya
Katika somo hili uatkwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Yahya Soma Zaidi...
hHistoria ya Nabii Dhul-kifl
Katika makala hii tutakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Dhul-kifl Soma Zaidi...
Hstoria ya Nabi Daud
Katika somo hili utawenda ujifunza uhusu historia ya Mtume Daud Soma Zaidi...
Historia ya Nabii Shu'aib
atika makala hii utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Shu'aib katika Quran Soma Zaidi...
Historia ya Mtume Hud katika Quran
Katika makala hii utakwenda kujifunzahistoria ya Mtume Hud katika Quran Soma Zaidi...
Historia ya Mtume Lut
Katika somo hili utakwenda kujifunza historia yaMtume Lut kutoka katika Quran Soma Zaidi...
Historia ya Mtume Swaleh (Salih)
Katika post hii utakwenda kujifunza historia ya Mtume Swalehe katikaQuran Soma Zaidi...
Histora ya Nabi Zakariya
Katika somo hili utakwenda ujfunza kuhusu hslistoria ya Nabi Zakariya Soma Zaidi...
Historia ya Nabii Ya'qub
Katika somo hili utawenda ujfunz ahstoraya Nabii Ya'qub na familia yake Soma Zaidi...