image

Historia ya Nabii Nuhu katika Quran

Katika somo hili utakwenda kujifunza historia ya Mtume Nuhu kulingana na melezo yaliyo kwenye Quran

NUHU(A.S) NA WATU WAKE NA UOVU WALIOKUWA WAKIUFANYA WATU WAKE

 

Mtume aliyemfuatia Nabii Idrisa(a.s)katika Mitume waliotajwa katika Qur-an ni Nabii Nuhu(a.s). Nuhu(a.s) ni miongoni mwa Mitume wa mwanzo mwanzo kabisa. Kutokana na mabaki ya kihistoria tunajifunza kuwa Nabii Nuhu na kaumu yake waliishi katika nchi ya Iraq.


 

Mazingira ya Jamii Aliyoikuta Nabii Nuhu (a.s)


Nabii Nuhu(a.s) aliwakuta watu wa jamii yake wakimshirikisha Allah(s.w)kwa namna mbali mbali nawalikuwa wakiabudia masanamu waliyoyachonga na kuyapa majina ya W adda , Suwa’a , Y aghuutha , Y a’uuka na Nasraa . Kama tulivyofahamishwa katika Qur-an kuwa viongozi wa jamii ya kishirikina ambao walikuwa ndio wapinzani wakubwa wa ujumbe wa Nabii Nuhu waliwanasihi wafuasi wao:


 


“Msiache miungu yenu, wala msiwache Wadda wala Suwa’a wala Yaghuutha na Ya’uka na Nasraa.” (71:23).


 

Mtume(s.a.w) anatufahamisha katika Hadith kuwa Wadda na wale waliotajwa pamoja naye walikuwa ni watu wacha-Mungu katika jamii yao. Walipofariki,watu wakaanza kuyazungukia


 

makaburi yao na shetani akakichochea kizazi kilichofuata kuunda sanamu za watu hao. Kwa kufanya hivyo walidhani wangeliweza kuwaiga vitendo vyao vyema kwa kuwa na taswira za watu hao daima katika akili zao. Kizazi cha tatu kilishawishika kirahisi sana kuwa watu hao walikuwa ni miungu wanaostahiki kuabudiwa badala au pamoja na Allah(s.w). Masanamu yote yanayoabudiwa yana historia ya namna hii.


 

Wito wa Nabii Nuhu(a.s) kwa Watu Wake


Nabii Nuhu(a.s) kama walivyofanya Mitume wote, aliwafundisha watu wake Tawhiid kuwa wamuamini Allah (s.w) kwa kuzingatia ishara mbali mbali zilizowazunguka, na kwamba wamuabudu yeye peke yake na wasimshirikishe na chochote. Aliwaonya juu ya adhabu kali itakayowafika iwapo hawatakoma kumshirikisha Allah(s.w) na miungu wengine.Juu ya wito wa Nuhu(a.s) kwa watu wake Qur-an inatufahamisha:


 


“Tulimpeleka Nuhu kwa watu wake, naye akasema: “Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila yeye. Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya siku (hiyo) iliyo kuu.” (7:59).

 

Msimamo wa Nabii Nuhu(a.s) Dhidi ya Makafiri

 

Pamoja na upinzani mkali alioupata kutoka kwa viongozi wa makafiri, Nabii Nuhu(a.s) aliendelea kwa hima kulingania Dini ya Allah(s.w) na kuuweka wazi msimamo wake kama ifuatavyo:

 


“Wasomee habari za Nuhu alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Ikiwa kukaa kwangu na nyinyi na kukumbusha kwangu Aya za Mwenyezi Mungu kunakuchukizeni, basi mimi nategemea kwa Mwenyezi Mungu. Nanyi kusanyeni mambo yenu na hao washirika wenu. (Kusanyikeni mje kunidhuru, mimi sijali).

 

Tenashauri lenu hilo lisifichikane kwenu (fanyeniu kwa dhahiri; mimi sijali tu). Kisha mpitishe kwangu (hilo mnalotaka kupitisha). Wala msinipe nafasi (hata kidogo. Mimi sijali, namtegemea Mwenyezi Mungu tu).” (10:71)

 

Nabii Nuhu(a.s) aliendelea kuwausia watu wake na kudhihirisha msimamo wake.

 


“Na enyi watu wangu! Mimi sikuombeni mali juu ya (jambo) hili; sina ujira wangu ila kwa Mwenyezi Mungu; na mimi sitawafukuza walioamini (kama mnavyotaka kwangu niwafukuze hao madhaifu ndipo msilimu nyinyi watukufu. Sitafanya hivyo); maana wao watakutana na Mola wao (awalipe kwa mema yao na mabaya yao). Lakini mimi nakuoneni nyinyi ni watu mnaofanya ujinga. (Mnakataa kuifuata haki kwa kuwa imefuatwa na madhaifu)! (11:29).

 

Kwa ufupi tunajifunza kuwa:

• Nabii Nuhu(a.s) hakumchelea yeyote au chochote katika kulingania Dini ya Allah(s.w), bali alimtegemea Allah(s.w).
• Alilingania Dini ya Allah kwa kutarajia malipo kutoka kwake tu.
• Aliwapokea na kuwakumbatia wote waliomuamini bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

 


Ushindi wa Nabii Nuhu(a.s) na Wale Walioamini Pamoja Naye.

 

Nabii Nuhu(a.s)alilingania Uislamu katika mazingira magumu ya upinzani mkubwa bila ya kukata tamaa kwa muda wa miaka 950.

Alipoona kuwa viongozi wa makafiri wanazidi kuweka mikakati ya kuzuia watu kusilimu kila uchao na kuwashinikiza kurudi kwenye ukafiri hata wale walioamini kwa kuwafanyia vitimbi mbalimbali, Nabii Nuhu(a.s) alilazimika kuomba msaada wa Allah(s.w) dhidi ya makafiri kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:

 

“Na (wakumbushe) Nuhu alipotulingania zamani (kutuomba) nasi tukamuitikia, na tukamuokoa yeye na watu wake katika shida (msiba) kubwa hiyo.(21:76)

 


Na tukamnusuru juu ya watu waliozikadhibisha aya zetu. Hakika wao walikuwa watu wabaya. Basi tukawatotesha (gharikisha) wote.” (21:77)

 

Kabla yao kama tulivyoona watu wa Nuhu walikadhibisha nao. Walimkadhibisha mja Wetu na wakasema ni mwendawazimu; na akawa anatolewa maneno makali. Ndipo akamuomba Mola wake (akasema): “Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru.(54:9-10)

 

 

Mara tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayomiminika (kwa nguvu kabisa). Na tukazibubujisha maji chemchem zilizo katika ardhi; na maji (ya juu na chini) yakakutana kwa jambo lililokadiriwa (na Mungu).(54:11-12)

 


Na Tukamchukua (Nabii Nuhu) katika ile(jahazi) iliyotenge nezwa kwa mbao na misumari. Ikawa inakwenda mbele ya macho, (hifadhi) Yetu. Hii ni tunzo (tuzo) kwa yule aliyekuwa amekataliwa (amekanushwa). (54:13-14)

 

Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa Nabii Nuhu(a.s) pamoja na waumini wachache aliokuwa nao walipata ushindi mkubwa juu ya makafiri waliokuwa wengi na uwezo mkubwa kwa msaada wa Allah(s.w). Allah(s.w) alitumia jeshi la “maji” kuwaangamiza makafiri na akawanusuru waumini kwa jahazi. Hii inatukumbusha kuwa:

 

“Na majeshi ya mbingu na ardhi ni ya Mwenyezi Mungu; na
Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye hikima.” (48:7)

 

Waliomuamini Nabii Nuhu(a.s)

 

Waliomuamini Nuhu(a.s) walikuwa watu wachache tena wale waliokuwa wanyonge na dhaifu katika jamii. Uchache na udhaifu wa waumini ilitumiwa na makafiri wa wakati wake kama hoja ya kumkataa Nuhu kuwa si Mtume wa Allah(sw).


 


“Wakasema: Je, tukuamini wewe hali ya kuwa wanyonge ndio wanaokufuata? (26:111)


 

Uchache wa waumini waliokuwa pamoja na Nabii Nuhu(a.s) unadhihiri vizuri pale walipo weza kuenea kwenye safina ndogo iliyosheheni mizigo yao na jozi za wanyama mbali mbali kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:


 


“Hata ilipokuja amri yetu na ardhi ikaanza kufoka maji tulimwambia (Nuhu) Pakia humo (jahazini) jozi moja katika kila (nyama, jike na dume) na wapakie watu wako wa nyumbani kwako isipokuwa wale ambao imewapitia hukumu (ya Mwenyezi Mungu). Na (wachukue wote) walioamini.” Na hawakuamini pamoja naye ila wachache tu.” (11:40)


 

 

Wapinzani wa Ujumbe wa Nabii Nuhu(a.s) na Vitimbi Vyao

 

Waliokuwa mstari wa mbele katika kupinga ujumbe wa Nabii
Nuhu(a.s), ni viongozi wakuu wa jamii yake.


 

Wakuu wa watu wake wakasema: Sisi tunakuona umo katika upotofu (upotevu) ulio dhahiri (kwa kutukataza haya tuliyowakuta nayo wazee wetu)” (7:60)


 

Katika kukataa ujumbe wa Nabii Nuhu(a.s), viongozi wa makafiri walitoa hoja dhaifu zifuatazo:




 

“Na hapa wakasema wakubwa wa wale waliokufuru katika kaumu yake. Hatukuoni ila ni mtu tu sawa nasi; wala hatukuoni ila wamekufuata wale wanaoonekana dhahiri kuwa ni dhaifu (wanyonge) watu, (wamekufuata) kwa fikira ya mawazo tu (bila kupeleleza vizuri) wala hatukuoneni kuwa mnayo ziada juu yetu; bali tunakuoneni kuwa ni waongo. (11:27)


 


Wakasema wale wakuu waliokufuru katika watu wake: “Hakuwa huyu (Nuhu) ila ni mtu kama nyinyi. Anataka kujipatia ubora juu yenu. Na kama Mwenyezi Mungu angependa (kukufundisheni), kwa yakini angateremsha Malaika. Hatukusikia haya kwa wazee wetu wa mwanzo.” (23:24)


 

Hakuwa huyu ila ni mtu mwenye wazimu. Basi mngojeeni hata muda (wake atakufa).” (23:25)


 

Kwa mujibu wa aya hizi makafiri walikataa Utume wa Nabii
Nuhu(a.s) kwa Sababu:


 

Alikuwa mtu kama wao. Walitarajia kutumiwa Malaika.

Waliomuamini walikuwa watu dhaifu kiuchumi na hadhi.

Kwa upande mmoja, hawakuona faida yoyote iliyopatikana

kwa waumini kutokana na kuamini kwao na kwa upande mwingine, hawakuona hasara yoyote waliyoipata kutokana na huko kukufuru kwao.

Walimuita Nabii Nuhu mwenda wazimu:


 

Kabla yao watu wa Nuhu walikadhibisha nao. Walimkadhibisha mja wetu na wakasema ni mwendawazimu, na akawa anatolewa maneno makali”. (54:9)

Na walimtishia kumuua:

“Wakasema: Kama hutaacha, Ewe Nuhu (nasaha zako hizi), bila shaka utakuwa miongoni mwa wanaorujumiwa (wanaopigwa kwa mawe mpaka wafe)”. (26:116)

 

Kuangamia kwa Mtoto na Mke wa Nuhu(a.s)

Tukirejea Qur’an (11:36-48) na (23:26 -29) tunapata maelezo juu ya mchakato wa kuangamizwa makafiri na kuokolewa waumini katika kaumu ya Nabii Nuhu(a.s). Pamoja na Nabii Nuhu(a.s) kuahidiwa kuwa watu wake wa nyumbani watakuwa miongoni mwa watakaookolewa na gharka, mtoto wake alikataa kuingia kwenye jahazi(safina) na akawa ni miongoni mwa wenye kuangamia kama tunavyo jifunza katika aya zifuatazo.


 


Na akasema(Nuhu):”Pandeni humo, kwa jina la Mwenyezi Mungu kuwe kwenda kwake na kusimamma kwake. Hakika Mola wangu ni mwingi wa kusamehe na mwingi wa kurehemu.


Ikawa hiyo (jahazi) inakwenda nao katika mawimbi kama milima. Na Nuhu akamwita mwanawe aliyekuwa mbali amekataa kuingia jahazini: “Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi wala usiwe pamoja na makafiri”. Na akasema (huyo mtoto)” “Nitaukimbilia Mlima utakaonilinda na maji” Akasema(Nuhu): “Hakuna leo wa kulindwa na amri ya Mwenyezi Mungu isipokuwa yule atakayemrehemu (Mwenyezi Mungu).” Mara mawimbi yakaingia baina yao na akawa miongoni mwa waliogharikishwa. (11:41-43)


 

Baada ya Gharika

Baada ya gharika kuisha, Nabii Nuhu(a.s) Ilibidi amuelekee Mola wake kutaka kujua ni vipi mwanawe amekuwa miongoni mwa walioangamia.


 


Na Nuhu alimuomba Mola wake (alipomuona mwanawe anaangamia) akasema: Ewe Mola wangu! Mwanangu ni katika watu wa nyumbani kwangu (mbona anaangamia)? Na hakika ahadi Yako ni haki; nawe ni mwenye haki kuliko mahakimu (wote).”Akasema (Mwenyezi Mungu): “Ewe Nuhu! Huyu si miongoni mwa watu wako. Yeye ni (mwenye) mwenendo usiokuwa mzuri. Basi usiniombe ambayo huyajui. Mimi nakunasihi usiwe miongoni mwa wajinga.” (Nuhu) Akasema: Ee Mola wangu! Mimi najikinga kwako nisije kukuombatena nisiyoyajua; na kama hutanisamehe na kunirehemu nitakuwa miongoni mwa watakaopata khasara.”(11:45-47)


 

Pia tunahamishwa juu ya kuangamia mke wa Nuhu(a.s) katika aya ifuatayo:


 


Mwenyezi Mungu amepiga (anapiga)mfano wa wale wabaya waliokufuru, ni mkewe Nuhu na mkewe Luti. Walikuwa chini ya waja wetu wema wawili hao miongoni mwa waja wetu (wema)’ lakini(wanawake hao), waliwafanyia khiana (waume zao watukufu hao) na (waume zao hao) hawakuweza kuwasaidia


 

chochote mbele ya Mwenyezi Mungu na ikasemwa: “Uingieni
Moto pamoja na hao wanaouingia.” (66:10)


 

Kuangamia kwa mtoto na mke wa Nuhu(a.s) pamoja na mke wa Lut(a.s) tunajifunza kuwa mtu hataokoka na ghadhabu ya Allah(s.w) kutokana a unasaba alioonao na watu wema na wala hata faidika na malipo ya amali njema walizofanya wengine. Kinyume chake hataadhibiwa mtu mwema kwa kuwa na unasaba na watu waovu maadamu anawafikishia ujumbe na wakamkanusha kama tunavyopigiwa mfano wa mke wa firaun,aliyekuwa mcha-mungu.


 


Na Mwenyezi Mngu amepiga, (anapiga) mfano wa wale walioamini kweli, ni mkewe Firauni, aliposema; “Ee Mola wangu! Nijengee nyumba Peponi karibu yako na uniokoe na Firauni na amali zake (mbovu), na Niokoe na watu madhalimu”(66:11)

 

Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Nabii Nuhu(a.s)

 

(i) Tuanze kulingania kwa Tawhiid – kumjua Allah(s.w)fika na kumuabudu ipasavyo.


 

(ii) Tulinganie kwa kutumia hoja na mbinu mbalimbali kulingana na mazingira na wakati.


 

(iii) Tutumie hoja kuonesha udhaifu wa hoja za makafiri dhidi ya Uislamu.


 

(iv) Tusimchelee yeyote au chochote katika kulingania na kusimamisha Dini ya Allah(s.w).


 

(v) Tulinganie Uislamu kwa kutaraji malipo kutoka kwa
Allah(s.w)pekee.


 

(vi) Waumini hawana budi kushikamana pamoja katika kulingania na kusimamisha Uislamu katika jamii.


 

(vii) Mlinganiaji awe na subira na kutowakatia tamaa wale anaowalingania – Nabii Nuhu(a.s) alilingania miaka 950 na kupata wafuasi wachache sana bila ya kukata tamaa.


 

(viii) Mlinganiaji amuombe Allah(s.w) na kutegemea msaada kutoka kwake.


 

(ix) Hatanusurika mtu muovu na adhabu ya Allah(s.w) kutokana na nasaba yake na Mitume wa Allah(s.w) na watu wema.


 

(x) Hatima ya makafiri ni kuhiliki katika maisha ya dunia na akhera.


 


“Wala wale waliokufuru wasifikiri kwamba wao wamekwi shatangulia (mbele, Allah hawapati), la, wao hawatamshinda (Mwenyezi Mungu). (8:59).


 

(xi) Hatima ya waumini wanaharakati ni kuwashinda maadui zao hapa ulimwenguni na kupata pepo huko akhera.


 

(xii) Kushindwa na kuhiliki kwa makafiri wenye nguvu kubwa za kijeshi na kiuchumi na waumini wachache na dhaifu kijeshi nakiuchumi ni alama ya kuwepo Allah(s.w) aliyoahidi kuwatawalisha katika ardhi waumini wanaharakati.(Qur-an 24:55).


 

(xiii) Siku zote wanaoongoza katika upinzani ni viongozi wa kikafiri(matwaghuti).


 

(xiv) Hatuna mtu atakaye epukana na ghadhabu za Allah(s.w) na kupata pepo kwa amali njema alizofanya mtu mwingine hata akiwa na unasaba au urafiki wa karibu kiasi gani. Mtoto na mke wa Nuhu(a.s) waliangamia kutokana na matendo yao maovu.


 

(xv) Hakuna mtu atakaye adhibiwa kwa maovu ya mwingine na huku akiwa ni muumini mtenda mema. Mkewe Firaun ni miongoni mwa wanawake wema waliotajwa katika Qur’an.





           

Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Rajabu Tarehe 2024-06-25 20:48:38 Topic: visa vya Mitume Main: Masomo File: Download PDF     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 611


Sponsored links
👉1 Kitabu cha Afya     👉2 Madrasa kiganjani     👉3 kitabu cha Simulizi     👉4 Kitau cha Fiqh     👉5 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)     👉6 Simulizi za Hadithi Audio    

Post zifazofanana:-

Historia ya Nabii Nuhu katika Quran
Katika somo hili utakwenda kujifunza historia ya Mtume Nuhu kulingana na melezo yaliyo kwenye Quran Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Yahya
Katika somo hili uatkwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Yahya Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Ya'qub
Katika somo hili utawenda ujfunz ahstoraya Nabii Ya'qub na familia yake Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Ibrahimu
Katika post hii utakwenda kujifunza historia ya Mtume Ibrahim katika quran Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Ilyasa
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Ilyasa Soma Zaidi...

hHistoria ya Nabii Dhul-kifl
Katika makala hii tutakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Dhul-kifl Soma Zaidi...

Historia ya Nabii Musa
atika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu historia ya Nabii Musa Soma Zaidi...

Hstora ya Nabii Adam
ata post h utawenda ujfunza hstora ya Nabii Adam ulngana na Quran navyoeleza Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Lut
Katika somo hili utakwenda kujifunza historia yaMtume Lut kutoka katika Quran Soma Zaidi...

Hstoria ya Nabi Daud
Katika somo hili utawenda ujifunza uhusu historia ya Mtume Daud Soma Zaidi...

Historia ya Mtume Muhammad (s.a.w) wa ufup
Huu n ufupisho wa Historia ya Mtume Muhammad s.a.w. Tumekuandalia histori hii kwa urefu zaidi kwenye Makala zetu zinazofuata Soma Zaidi...

Historiaya Nabii Isa
Katika somo hili utakwenda kujifunza kuhusu Historia ya Nabii Isa Soma Zaidi...