HISTORIA YA NABII YUSUFU(A.S.)


Mtume Yusufu(a.s) alikuwa mtoto wa Mtume Ya’aquub bin Is- haq bin Ibrahiim. Kwa hiyo Yusufu(a.s) ni kijukuu cha (mjukuu wa mtoto wa) Mtume Ibrahiim(a.s) na mjukuu wa Mtume Is-haqa(a.s.).

Mtume Ya’aquub(a.s) alikuwa na watoto 12. Nabii Yusufu(a.s) alichangia mama na mmoja wa hao. Wengine 10 walikuwa na mama zao.


Ndoto ya Nabii Yusufu(a.s) Maisha ya Nabii Yusufu(a.s) yanaanza kusimuliwa ndani ya Qur’an pale alipomwambia babake kuwa:Yusufu alipomwambia baba yake “Ewe babaangu! hakika nimeona katika ndoto nyota kumi na moja na jua na mwezi. Nimeviona hivi vikinisujudia(12:4)Mtume Ya‘aquub, kwa ilimu aliyopewa na Mola wake alifahamu tafsiri ya ndoto ile kwamba inabashiri kuwa Yusufu atakuja kuwa mtu mwenye hadhi kubwa na Mtume. Akamtahadharisha kuwa:Akasema (baba yake): “Ewe mwanangu! Usiwasimulie ndoto yako (hii) nduguzo wasije wakakufanyia vitimbi (kwa ajili ya husuda). Hakika Shetani kwa mwanadamu ni adui aliye dhahiri.(12:5)
Namna hivi Mola wako atakuchagua na kukufundisha hakika ya mambo. Na atatimiza neema zake juu yako na juu ya kizazi cha Ya‘aquub, kama alivyoitimiza zamani juu ya baba zako Ibrahim na Is-haqa. Bila shaka Mola wako ni Mjuzi na Mwenye hikima: (12:6).