Njama za Kumuua Nabii Yusufu(a.s)


Kwa tabia zake njema Yusufu(a.s) alipendwa sana na baba yake. Ndugu zake Yusufu(a.s) wakajawa chuki na husuda wakijadiliana kuwa;


...............Hakika Yusufu na nduguye wanapendwa sana na baba kuliko sisi, hali sisi ni kundi lenye nguvu. Hakika baba yetu yumo katika upotofu ulio wazi.(12:8)



Wakapanga njama za kumhujumu Yusufu (a.s) kwa kumuua ili mapenzi ya baba yao yawageukie wao. Wakapanga na kuazimia kuwa:



Muueni Yusufu au mtupeni nchi za mbali ili uso wa baba yenu ukuelekeeni na baada ya haya mtakuwa watu wema. (12:9)



Hatimaye wakakubaliana kumtumbukiza kisimani badala kumwua,wazo hili lilitolewa na mmoja wao ambaye angalau aliogopa kubeba dhima ya kufanya dhambi kubwa ya kuiua nafsi pasina haki. Akasema;



Msimuue Yusufu lakini mtupeni Yusufu katika(jiwe la ndani) ya kisima kirefu, watamuokota baadhi ya wasafiri, kama ninyi mnataka kufanya kitu.(12:10)



Yusufu anatumbukizwa kisimani

Kutumbukizwa Yusufu(a.s) Kisimani Pamoja na kuwa na dhamira ile mbaya ya kutaka kufanya kosa la kuua mtu asiyekuwa na hatia , wakaongeza kosa lingine la kusema uwongo. Wakasema:


........Ewe baba yetu, mbona hutuamini juu ya Yusufu, hakika sisi ni wenye kumtakia mema. Mruhusu kesho pamoja nasi atakula kwa furaha na kucheza; hakika sisi tutamlinda (12:11-12)



Ingawa mzee Ya’aquub(a.s) alionesha wasiwasi,lakini hatimaye aliwaruhusu waandamane naye. Walimtumbukiza Yusufu(a.s) kisimani kama walivyo dhamiria na wakaichukua kanzu yake na kuipakaza damu za uwongo, kisha wakamuongopea baba yao:



Ewe baba yetu! Hakika sisi tulikwenda kushindana mbio na tukamuacha Yusufu penye vyombo vyetu, basi mbwa mwitu akamla; lakini hutatuamini ingawa tunasema kweli (12:17)

Ya‘aquub(a.s.) alikuwa na mategemeo makubwa ya kupata mrithi bora atakayeendeleza kazi yake. Hata hivyo hatumwoni mzee Ya’aquub akikata tamaa kwa kufadhaika au kukufuru. Yeye akawajibu;

......



“..............Nafsi zenu zimekushawishini jambo. Basi (langu mimi ni) subira njema; na Mwenyezi Mungu ndiye aombwaye msaada kwa haya mnayoyasema” (12:18).

Hii ndio tabia ya Muislamu. Kurejea na kumtegemea zaidi Allah(s.w) afikwapo na msiba.