HISTORIA YA NABII SALIH(A.S)


Nabii Salih(a.s) alifuatia baada ya Hud(a.s) na alitumwa kwa watu wa kabila (Taifa) la Thamud. Makazi yao yalikuwa kaskazini mwa Arabia sehemu iliyojulikana kama al-Hijr Mada’in Salih.

Thamud waliongoza katika teknolojia ya kuchonga majabali na kuyafanya majumba ya fahari kama tunavyofahamishwa katika Qur-an:......

“Na kumbukeni (Allah) alivyokufanyeni makhalifa baada ya ‘Ad na kukuwekeni vizuri katika ardhi; mnajenga majumba makubwa ya kifalme katika nyanda zake, na mnachonga majumba katika majabali (yake).........” (7:74)

Baada ya muda kupita Thamud nao waliacha mafundisho ya Mtume Hud(a.s) kama walivyofanya akina ‘Ad hapo zamani, wakawa wanaabudia masanamu na kufisidi katika ardhi. Ndipo Allah(s.w) akamtuma Nabii Salih(a.s) kulingania Uislamu kwa wakazi wa Hijr.Ujumbe wa Nabii Salih(a.s) kwa Watu Wake


Nabii Salih(a.s) aliwalingania watu wa kaumu yake, wamwamini Allah(s.w) na kumuabudu ipasavyo, watubie na waombe msamaha kwa dhambi zao:
“Na kwa Thamud tukampelekea ndugu yao, Salih, akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Allah; nyinyi hamna Mungu ila yeye. Yeye ndiye aliyekuumbeni katika ardhi, na akakukalisheni humo. Basi muombeni msamaha, kisha mrejee kwake. Hakika Mola wangu ni karibu (na waja wake) anapokea (maombi yao).” (11:61)

Nabii Salih aliendelea kuwalingania“Mcheni Mwenyezi Mungu na nitiini.” “Wala msitii amri za wale maasi, (wenye kupindukia mipaka ya Mungu).” “Ambao wanafanya uharibifu tu katika ardhi wala hawaitengenezi.” (26:150-152)