HISTORIA YA NABII MUSA(A.S) NA HARUN(A.S)

Nabii Musa(a.s) ni Mtume aliyeandaliwa na Allah(s.w) kuwakomboa Bani Israil (Waisraili) waliofanywa kuwa watumwa nchini Misri. Waisraili ni kizazi cha Nabii Ya‘aquub(a.s),Nabii Yusufu(a.s) ndiye alianza kukaa Misri kisha wakafuatia wazazi na ndugu zake wote wakati alipokuwa kiongozi nchini humo.



Allah(s.w) alimtuma Nabii Musa(a.s) kuwakomboa Bani Israil kwasababu haki yao ya kuwa huru ambayo Allah(s.w) amempa kila mwanadamu, iliporwa! Maadamu Bani Israil waliporwa haki hii kuu ya msingi; Allah(s.w) kwa uadilifu wake akamtuma Nabii Musa(a.s) kutekeleza jukumu zito la kuwakomboa na kuwarejeshea haki zao za kibinadamu walizonyang’anywa.




Hakika Firauni alitakabari katika ardhi, na akawafanya watu wa huko makundi mbalimbali. Akalidhoofisha kundi moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wakiume na kuwa acha hai watoto wao wa kike. Hakika yeye alikuwa miongoni mwa waharibifu (28:4)



Aya hii zimeweka wazi ukiukwaji wa haki za binadamu walioufanya watawala wa Misri. Lengo la kuhalalisha ukatili na mauwaji hayo lilikuwa kuwadhoofisha wananchi wenye nasaba ya Nabii Yusufu(a.s) wasipate nafasi ya kuongoza tena.