HISTORIA YA NABII ISMAIL(A.S)


Ismail(a.s) ni mtoto wa kwanza wa Mtume Ibrahim(a.s.). Alizaliwa wakati uzee umekwishamfikia Ibrahim(a.s). Kama Qur’an inavyobainisha, katika umri huo wa uzeeni, MtumeIbrahiim(a.s) alimuomba Mola wake ampe mtoto mwema atakaendeleza harakati za Kiislamu.“Ee Mola wangu! Nipe (mtoto awe) miongoni mwa watenda mema.” Ndipo tukampa habari njema ya (kuwa atapata) mtoto mpole. (Basi akapata. Naye ndiye Nabii Ismail).” (37:100-101).Mtume Ibrahim(a.s.) aliletewa mitihani migumu miwili juu ya mtoto huyu. Mosi ni kule kuamriwa kumwacha yeye pamoja na mama yake katika bonde kavu lisilo na watu wala maji. Hilo lilikuwa bonde la Makka. Maji ya kisima zamzam yaliyo katika Msikiti wa Makka, aliyabubujisha Allah(s.w) kwa ajili ya Ismail na mama yake. Chem-chem hiyo imedumu hadi leo. Aidha, vilima vya Safa na Marwa vimepata umaarufu na kuwa miongoni mwa alama muhimu katika Uislamu, kutokana na kitendo cha mama yake Ismail Hajirah, kukimbia baina ya vilima hivyo katika jitihada za kumtafutia mwanae Ismail maji.Mtihani mwingine alioupata MtumeIbrahiim(a.s) juu ya Ismail(a.s) ni kule kuamrishwa amchinje. Huu haukuwa ni mtihani kwa baba tu, lakini pia mtoto Ismail(a.s). Hebu fikiri ungekuwa katika hali gani, kama ungekuwa mahali pa Ismail(a.s). Baba yako anakwambia ameamrishwa na Allah(s.w.) akuchinje! Hakika ni mtihani mgumu ila kwa wale wanaonyenyekea kikweli kweli kwa Muumba wao.Qur’an yatufahamisha kuwa Ismail alikuwa mpole na mnyenyekevu kwa Mola wake. Kwa hiyo hakusita kutoa nafsi yake kwa ajili ya Muumba wake. Bali alimhimiza baba yake amchinje kama Allah(s.w) alivyomuamrisha.Basi alipofikia (makamu ya) kwenda na kurudi pamoja naye akamwambia: “Ee mwanangu! Hakika nimeona katika ndoto ya kwamba ninakuchinja. (Na ndoto ya Mitume ni Wahayi). Basi fikiri,waonaje?”Akasema:“Ee baba yangu! Fanya unayoamrish wa, utanikuta Inshallah miongoni mwa wanaosubiri”.(37:102).Utii na unyenyekevu huu wa Nabii Ismail(a.s) ni kielelezo muhimu kwetu. Kwamba, amri ya Allah(s.w) ni lazima itiiwe kwa gharama yoyote ile ikiwa ni pamoja na roho zetu.