Kuinua Kuta za Ka’bah.


Kama tulivyoona katika maisha ya Mtume Ibrahim(a.s.), Nabii Ismail (a.s.) alishirikiana na baba yake kuinua kuta za Ka’abah ambayo ndiyo nyumba kongwe ya kufanyia Ibada na kituo kikuu cha kwanza cha harakati za Kiislamu duniani.


“...........Na tulimwusia Ibrahim na Ismail (tukawaambia): Itakaseni nyumba yangu kwa ajili ya wale wanaoyoizunguka kwa ajili ya kutufu na wanaokaa hapo na (kwa ajili ya) wanaorukuu na kusujudu hapo pia” (2:125).“Na (kumbukeni khabari hii) Ibrahim alipoinua kuta za nyumba (hii ya Al-Ka’bah) na Ismail (pia) (wakaomba, wakasema): “Ee Mola wetu! Tutakabalie (amali yetu hii ya kujenga huu msikiti). Hakika wewe ndiwe Mwenye kusikia, na Mwenye kujua”. (2:127).Ismail(a.s) na Taifa la Waarabu


Nabii Ismail(a.s) ndiye chimhuko la kabila la Quraysh. Baada ya kuachwa katika bonde la Makka lililokavu, Allah(s.w) alijaalia kupatikana maji na hatimaye watu kuhamia pale. Uhai wa mji ukaanza na kutokana na kizazi cha Ismail(a.s) wakapatikana Waarabu wa Hijaz (Saudi Arabia) ambao hufahamika kwa jina mashuhuri Banu Quraysh. Qur’an imemtaja Ismail(a.s) kuwa alikuwa Mtume mkweli wa ahadi aliyewausia watu wake swala na zakat.
“Na mtaje katika kitabu (hiki) Ismail. Bila shaka yeye alikuwa mkweli wa ahadi, na alikuwa Mtume, Nabii. Na alikuwa akiwaamrisha watu wake Sala na Zakat na alikuwa mridhiwa mbele ya Mola wake”. (19:54-55).Qur’an hapa haimtaji Ismail kwa wema kwa vile alikuwa mtoto wa Mtume Ibrahim(a.s.), bali kwa vile alikuwa mtumishi wa Allah aliye mkweli, muamrisha mema na mkataza maovu. Nasaba hapa haikutajwa kabisa.Baada ya MtumeIbrahiim(a.s) na mwanae Ismail kujenga upya Ka’bah na kutangaza Hija, walimwomba Allah(s.w) alete Mtume atokanaye na kizazi chao ambaye ataendeleza harakati za Kiislamu kama walivyofanya wao. Aidha walikiombea kizazi chao kiwe ni cha watu wanyenyekevu:
“Ee, Mola wetu! Utufanye tuwe wanyenyekevu kwako. Na miongoni mwa kizazi chetu (pia ufanye) umma mnyenyekevu

kwako. na utuonyeshe njia ya Ibada yetu na utusamehe. Bila shaka Wewe ndiye Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.(2:128)
“Ee, Mola wetu! Waletee Mtume anayetokana na wao, awasomee Aya zako, na kuwafundisha kitabu (chako) na hikma na awafundishe kujitakasa (na kila mabaya). Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima” (2:129).Dua hii ilikuwa kabuili. Ilipofika zama za kuletwa Mtume wa mwisho, Allah(s.w.) akamleta kupitia kizazi cha Bani Quraysh ambao wanatokana na Ismail(a.s). Ndiye Mtume wetu Muhammad (s.a.w.).