Is-haq(a.s) ni mtoto wa pili wa Nabii Ibrahiim(a.s), mama yake akiwa Sarah. Habari njema ya kumzaa Is-haq ilimjia Nabii Ibrahim(a.s.) mara tu baada ya kufuzu mtihani wa kumchinja mwanae mkubwa, Ismail(a.s). Alipongezwa kwa kubashiriwa kuzaliwa kwa Is-haq(a.s.):
Amani kwa Ibrahim. Hivi ndivyo tunavyowalipa watendao mema. Bila shaka yeye alikuwa miongoni mwa waja wetu walioamini (kweli kweli).Tena tukambashiria (kumzaa) Is-haq, Nabii miongoni mwa watu wema (kabisa). (37:109-112).
Maelezo ya kuzaliwa Is-haq na hatimaye Ya‘aquub(a.s.) yanapatikana katika kisa cha Malaika waliompa Nabii Ibrahiimu habari za kuangamizwa watu waovu wa Nabii Lut(a.s) na zile za yeye kupata mtoto katika uzee wake.
Na mkewe (Ibrahim - bibi Sarah) alikuwa kasimama wima, akacheka. Basi tukampa habari njema ya (kuwa watazaa mtoto wamwite) Is-haq na baada ya I’shaq (watapata mjukuu wamwite) Yaaquub.(11:71)
(Mkewe Ibrahim) akasema: “Ee mimi we! Nitazaa na hali mimi ni mkongwe, na huyu mume wangu ni mzee sana? Hakika hili ni jambo la ajabu.”(11:72)
Wakasema (wale Malaika): Je, unastaajabia amri ya Mwenyezi Mungu? Rehema ya Mwenyezi Mungu na Baraka zake ziko juu yenu, enyi watu wa nyumba hii! Hakika Yeye (Mwenyezi Mungu) ndiye anayestahiki kusifiwa na kutukuzwa.” (11:73)