KUHUISHA UISLAMU WAKATI WA TABIINA
Utangulizi
Pamoja na kuporomoka kwa dola ya Kiislamu, waumini wa kweli wamekuwepo na kujitahidi hapa na pale, kwa mmoja mmoja na katika vikundi, kwa kadiri ya uwezo wao kuurudisha Uislamu katika ile hali aliyoiacha Mtume(s.a.w). Kwa mfano, pamoja na kuporomoka kwa Dola ya Kiislamu na maadili yake katika utawala wa kifalme wa Banu Umayyah, ulioasisiwa na Mu’awiya, aliibuka ‘Umar bin Abdul Aziz aliyekuwa Muislamu mcha Mungu, ambaye alipopata tu fursa ya kuteuliwa kuwa Kiongozi wa Dola, aliirejesha dola kwenye Uislamu. Pia walitokea maimamu mashuhuri wa fiqh ambao walifanya jitihada kubwa na kuyatoa muhanga maisha yao yote katika kuurudisha Uislamu katika nafasi yake ya kutawala kila kipengele cha maisha yakibinafsi na kijamii. Maimamu hawa ni: Abu Hanifa, Maliki, Shafii na Hambali. Tabiin niwafusi wa maswahaba.
Khalifa ‘Umar bin Abdul Aziz
Wakati watu wakiendelea kukata tamaa na utawala mbaya wa Banu Umayya aliibuka Umar bin Abdul Aziz mwaka 99
A.H(717A.D). ‘Umar alizaliwa mwaka 61 Hijriya. Wakati wa utawala wa Suleiman Ibn Abdul Malik, akawa gavana wa Madina. Alikuwa kijana mtanashati na mwenye tabia nzuri. Kwa vile uongozi ulikuwa ukienda kiukoo, ‘Umar hakuwa miongoni mwa waliotarajiwa kushika Ukhalifa. Hata hivyo Suleiman hakuwa na mtoto mkubwa hivyo ikatokea Umar kupendekezwa kuchukua uongozi na akakubalika.
Baada ya kushika uongozi, ‘Umar alibadili maisha yake yakawa rahisi zaidi na ya uadilifu. Aliwaondoa magavana wote waliokuwa katili. Akarejesha hadhi ya Baitul-Mal, ikawa fedha ya umma inakusanywa na kutumiwa kwa uadilifu. Pamoja na yeye mwenyewe kujichunga katika kutumia Baitul-Mal, alikuwa mkali pia kufuatilia maafisa waliofuja mali ya umma. ‘Umar bin Abdul Aziz hakuishia hapo, alitoa amri na kusimamia marekebisho ya vipimo(mizani, ili raia wasipunjwe). Aidha ardhi ambayo ilitengwa kwa ajili ya wakubwa aliichukua na kuwagawia raia. ‘Umar bin Abdul Aziz alikuwa kiongozi rahim na mtu mpenda watu, asiye na makuu. Alikuwa karibu na watu akisikiliza maoni yao juu ya uendeshaji wa dola, akitatua shida na matatizo ya raia. Kabla yake, Serikali zilizotangulia hazikujali hali wala hisia za raia. Zilikusanya kodi na kuendesha dola kwa misingi ya kujali zaidi familia na koo za wakuu. Hazikuwa zikijishughulisha kubadili tabia na mienendo ya watu. Kadhalika hazikuwa zikiwajenga watu kimaadili. Kazi hiyo waliachiwa masheikh. Uongozi wa ‘Umar ulibadili mtazamo huo potofu wa kutenganisha Dini na Serikali badala yake ukasimamia kikamilifu kazi ya kuamrisha mema na kukataza maovu huku ukiboresha hali na maisha ya watu. Kauli ya kukumbukwa ya ‘Umar bin Abdul Aziz juu ya wajibu wa kiongozi wa kiislamu ilikuwa: “Muhammad alitumwa kama Mtume sio mkusanya kodi”. Akiwa na maana wajibu wa kiongozi wa dola ya kiislamu haukomei katika kukusanya kodi tu bali anawajibika pia kuangalia maadili ya jamii.
Katika kujenga udugu miongoni mwa raia wake, Serikali ya ‘Umar ilipiga marufuku mila zote za kijahili ikiwa ni pamoja na mishikamano ya kikabila na kiukoo. Baadhi ya waliokuwa machifu wa makabila wakati wa utawala wa Banu Umayya walipotaka kufufua mila zao, ‘Umar bin Abdul Aziz aliwakemea vikali kwa kuwaambia: “Mila hizo za ukabila zinavuruga maana ya udugu wa kiislamu na mshikamano wa kijamii uliojengwa miongoni mwa raia (Waislamu). Akisisitiza msimamo huo, ‘Umar alionya kuwa yeyote ambaye angekutwa na tabia hiyo angekabiliwa na adhabu.Katika waraka wake kwa Dhahaakak Ibn Abdul Rahaman, Amiril Muuminina ‘Umar bin Abdul Aziz aliandika:
“Shukrani zote anastahiki Allah na rehema iwe kwa Mtume wake. Baada ya hayo, mnapaswa kujua kwamba Allah haikubali dini nyingine yoyote zaidi ya Uislamu ambayo amewachagulia waja wake wema. Mwenyezi Mungu ameitukuza dini hii ya Uislamu kwa kuiwekea mwongozo unaoitofautisha na dini nyingine. Mwenyezi Mungu mtukufu amempa utume Muhammad na amemfunulia kitabu. Nyie Waarabu, kama mnavyojua, mliishi kwenye ujahili, ushirikina na kila aina ya uchafu, mambo ambayo yalikuzamisheni kwenye ufukara, vurugu na machafuko ya mara kwa mara miongoni mwenu. Mlikuwa watu wa kudharauliwa mbele ya wengine, uhai wenu ukiwa chini ya ujahili na ushirikina ambapo umauti wenu usingekuwa na mafikio mengine ila motoni. Mwenyezi Mungu amewaokoeni kutoka lindi la maovu, kuabudu masanamu na umwinyi, kuchukiana na migongano miongoni mwenu. Ingawa wengi miongoni mwenu mlimkataa Mtume wa Mwenyezi Mungu lakini aliendelea kuwaita katika uongofu. Mtume wa Mwenyezi Mungu ameondoka katika ulimwengu akiwa amekamilisha ujumbe aliotumwa na Allah.........”
“Nimeelezwa kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakijikusanya kimakabila wa kujisaidia wao kwa wao kama ilivyokuwa zama zilizopita. Wanafanya hivyo wakijuwa wazi kuwa Mtume(s.a.w) alipiga marufuku ushirikiano huo. Mtume amesema hakuna utaifa au ukabila katika Uislamu. Hakuna mtu kutukuza eneo analotoka juu ya wengine. Zama za ujahili, watu walikuwa wakishirikiana hata katika mambo maovu bila ya kujali athari kwa wasio na mahusiano nao. Watu walikuwa wakikandamizana, kubaguana, kuchukiana na kufanyiana machafu kwa sababu ya tofauti hizo. “Namuasa kila atakayesoma au kusikia waraka huu ajipambe na vazi la Uislamu na asiwe na ndugu ila na yule aliyeshikamana na Allah na Mtume wake. Narudia tena kuonya kwa kumshuhudisha Mwenyezi Mungu dhidi ya atakayekiuka maamrisho hayo ya Allah na Mtume wake, kwani Mwenyezi Mungu ni mwenye uwezo na yuko karibu na yeyote kuliko mshipa wake mkuu wa damu”.
Kwa upande wa uchumi Amiril Muuminina ‘Umar bin Abdul Aziz alisimamia nguzo ya zaka na ukusanyaji wa kodi mbali mbali. Kutokana na uadilifu uliokuwepo katika ukusanyaji na utumiaji wa mapato ya umma, ilifikia mahali ndani ya dola ya Kiislamu kukawa hakuna maskini wa kupewa zaka.
UchaMungu wa Ibn Abdul Aziz ulijitokeza hata alipokuwa akiyaamuru majeshi yake kupambana na maadui. Hakuwa tayari kuona askari wa kiislamu akikiuka mipaka kwa kisingizio cha “vita haina macho”. Moja ya maelekezo yake kwa makamanda walioongoza misafara ya kijeshi, ‘Umar Abdul Aziz aliwataka wajiegemeze kwa Allah(s.w) katika kila wanapokabiliana na maadui. Aliwataka wasipindukie mipaka katika kushambulia. Sehemu ya Waraka wake mrefu kwa makamanda wa Jeshi hilo umenukuliwa kama ifuatavyo:
“Haya ni maelekezo kutoka kwa mja wa Allah na kamanda wa Waumini kwenda kwa Mansur Ibn Ghalib kamanda wa jeshi la kiislamu. Kamanda wa Waumini(Umar bin Abdul Aziz) anamuamuru Mansur kumpiga vita yule anayesimama kupambana naye. Aidha Mansur anaamriwa kumcha Mwenyezi Mungu katika kutekeleza wajibu huo na hiyo ndiyo stratejia na nguvu halisi ya kijeshi. Dhambi ni hatari zaidi kuliko silaha ya adui. Kamanda wa Waumini anamuamuru Mansur badala ya kumuhofu adui anapaswa kuhofu kukiuka mipaka ya Allah.Tumekuwa tukiwashinda maadui zetu vitani si kutokana na uhodari mkubwa wa kijeshi tulionao bali ni kutokana na dhambi na maovu yao, ingelikuwa si hivyo tusingekuwa na ujasiri wa kupambana nao. Hatuwezi kuwa na jeshi linalolingana na lao kiidadi na kisilaha. Kwa hiyo iwapo tutakuwa watenda maovu kama maadui zetu bila shaka watatushinda kwa mapambano ya silaha. Tambueni, iwapo hatutamcha Mwenyezi Mungu hatutaweza kuwashinda maadui zetu kivita.
Tuwe waangalifu zaidi wa matendo yetu. Msijiweke kwenye aibu ya kukiuka mipaka ya Allah. Kuweni wakarimu na wenye huruma, mkizingatia kuwa mmewaacha wapenzi wenu na majumba yenu kwa ajili ya Allah. Msijifakharishe mbele ya maadui zenu. Kamanda wa Waumini vile vile anamtaka Mansur Ibn Ghalib awaongoze wapiganaji kwa upole na kujali hisia zao. Asiwe mkali na katili kwao. Na iwapo Mansur hatajali ubinadamu itakuwa nafasi nzuri kwa maadui kupata ushindi dhidi yake. Kamanda wa waumini anawaelekezeni kuwa waangalifu katika maeneo ya maadui, wekeni wapelelezi miongoni mwa maadui baada ya kuwachunguza na kuwaona ni waaminifu kwenu ili mpate ripoti kutoka upande wa adui. Hata hivyo, ripoti zilizo na udanganyifu ni za hatari kwenu katika uchukuaji wa hatua, lazima muhakiki ripoti zao. Watakaowapeni habari kutoka kambi ya adui lazima nao muwatazame kama wapelelezi dhidi yenu. Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yenu”.
Kwa uadilifu na utendaji wake mzuri katika kuendesha Serikali, ‘Umar alifananishwa na Abubakar na aliitwa Khalifa wa tano wa Dola ya Kiislamu. ‘Umar bin Abdul Aziz alifariki mwaka 101Hijriya baada ya kutawala kwa miaka miwili na miezi mitano. Baada ya kufariki ‘Umar Abdul Aziz, ulifuatia msururu wa utawala wa Kifalme.
Je! umeipenda hii post?
Ndio Hapana Save post
Rajabu Tarehe 2024-05-10 14:53:23 Topic: Sira Main: Post File: Download PDF Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 1073
Sponsored links
👉1 Simulizi za Hadithi Audio
👉2 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w)
👉3 Kitabu cha Afya
👉4 kitabu cha Simulizi
👉5 Kitau cha Fiqh
👉6 Madrasa kiganjani
Adam na Hawah Kushushwa Ardhini
Soma Zaidi...
Msimamo wa Nabii Hud(a.s) Dhidi ya Makafiri wa Kaumu Yake
Pamoja na kwamba alipingwa na nguvu za Dola ya makafiri wa kaumu yake, Mtume Hud(a. Soma Zaidi...
HISTORIA YA NABII NUHU
Soma Zaidi...
Ujumbe wa Nabii Ibrahiim(a.s) kwa Mfalme Namrudh
Soma Zaidi...
Je, Nabii Isa(a.s) ni Mtoto wa Mungu?
Mwenyezi Mungu si kiumbe. Soma Zaidi...
Mawazo Tofauti Kuhusiana na Uchaguzi wa Abubakar
Soma Zaidi...
Sababu ya uislamu kuwa ndiyo dini sahihi pekee
Dini anayostahiki kufuata mwanadamu (EDK form 2: dhana ya elimu ya uislamu) Soma Zaidi...
Historia ya Dhana ya Kudhibiti Uzazi
Soma Zaidi...
Bani Israil Kuabudu Ndama
Wakati Nabii Musa(a. Soma Zaidi...
Msafara wa vita vya Tabuk Dhidi ya Warumi
Ukombozi wa mji wa Makka (Fat-h Makka) mwaka 8 A. Soma Zaidi...
Mafunzo yatokanayo na Historia ya Nabii Yunus(a.s)
(i) Allah(s. Soma Zaidi...